VMMU.80Vol.1/46 14/08/2016
TAARIFA
YA UMOJA WA VIJANA WA CCM KWA VYOMBO VYA HABARI KUFUATIA TAARIFA YA
UCHUNGUZI NA MAAZIMIO YALIYOTOLEWA NA KIKAO CHA BARAZA KUU LA UVCCM
LILILOKUTANA TAREHE 13/08/ 2016 MJINI DODOM
Karibuni sana katika
mkutano wetu muhimu tunaofanya leo tukiwa hapa Dodoma mara baada ya
kumalizika kwa kikao cha juu cha Jumuiya yetu yaani Baraza Kuu la Umoja
wa Vijana wa CCM Taifa.
Tarehe 10 Agost mwaka huu kilianza kikao
cha Sekretarieti ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa kikafuatia kikao cha
Kamati ya Maadili, kufuatia kikao cha Kamati ya Utekelezaji ya Baraza
Kuu la UVCCM Taifa na baadaye Baraza Kuu la UVCCM Taifa. Jumla ya Agenda
tisa (9) zilijadiliwa.
Baraza Kuu limeridhika na taarifa kadhaa
kuhusiana na agenda mbali mbali na kupokea taarifa moja nyeti na muhimu
kwa Jumuiya. “Ripoti ya uchunguzi wa Shamba la UVCCM Na. 454 MBYLR lenye
ekari 210” lililopo Igumbilo Wilaya ya Iringa mjini Mkoani Iringa
ambalo limeuzwa kwa Ndugu Suhail Ismail Thakore kinyume na taratpia pia
viwanja hivyo kuuzwa kwa watu mbali mbali na kuwahusisha Viongozi
kadhaa wenye dhamana ndani ya Jumuiya yetu.
Baada ya kupata
taarifa za uuzaji wa shamba hilo Mali ya UVCCM, kwa Mamlaka iliyonayo
Kamati ya Utekelezaji Taifa Ibara 91 (d), ilimwachia Mamlaka Mwenyekiti
wa UVCCM Taifa kuunda na kuteua wajumbe watatu wa Kamati ya Utekelezaji
ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa kuenda kufanya uchunguzi wa kadhia hiyo.
Nichukue nafasi hii kuishukuru kwa dhati Kamati ya uchunguzi iliyoongozwa na;
Ndugu Mariam Chaurembo - Mwenyekiti Ndg Juma Homela - Katibu Ndg AmirMkalipa Mjumbe Ndugu Ally Nassor Mjumbe
Kwa kufanikisha kazi waliyopewa na Jumuiya na hatimaye kuwasilisha
ripoti yao ambayo ilibaini mambo kadhaa machafu kinyume na miongozo ya
Chama na Jumuiya yetu.
Kikao cha Kamati ya Utekelezaji Mkoa wa
Iringa kilichoketi Februari 27, 2015 kilipitisha agenda Namba saba
kuhusu shamba la Igumbilo na kukubaliana kuuza ekari 20 hadi 30 kwa Shs.
3,000,000/= kwa eka moja, fedha zitakazopatikana zitumike katika
Matumizi mbali mbali kwa ajili ya shamba hilo.
Machi 2, 2015
UVCCM Mkoa wa Iringa ilipokea barua toka kwa Ndugu Suhail Ismail Thakore
kuomba kununua shamba hilo ekari 30 eneo la Igumbilo kwa bei ya Shs.
3,000,000/= kwa eka ambapo ni sawa na Shs. 90,000,000/=. Machi 4, 2015
Mkataba kati ya UVCCM Mkoa wa Iringa na mnunuzi ulisainiwa rasmi.
Mnamo April 13,17 na 24 Ndugu Suhail aliweka kiasi cha Shs. 90,000,000/= katika Akauunti ya UVCCM Mkoa wa Iringa Tawi la CRDB.
Shamba la UVCCM Igumbilo ambalo lilikuwa na ekari 210, ekari 85
zilipimwa na kubaki ekari 125. Ekari 85 zilitoa viwanja 170 kwa ukubwa
tofauti ambapo ukubwa wa chini sqm 319 na ukubwa wa juu sqm 32,007
ambapo katika viwanja 170 viwanja 25 vikawa miliki ya Ndugu Suhail
ambavyo vimetokana na ekari 30 kufuatia mauziano ya sehemu ya shamba
hilo kabla ya kupimwa.
Februari 27, 2015, Kamati ya Utekelezaji
Mkoa wa Iringa iliketi na kupitisha ili ipatikane fedha kwa taratibu za
upimaji na kuomba Hati iliyopo irejeshwe kwa ajili ya kuwasilishwa
Halmashauri ya Mji wa Iringa.
Aidha Machi 9 mwaka 2015 UVCCM Mkoa
wa Iringa iliandika barua kwenda Makao Makuu ya Umoja wa Vijana wa CCM
kuomba kupatiwa Hati ya UVCCM ya umiliki wa shamba la Igumbilo kutoka
Makao Makuu ambapo April mwaka 2015 aliyekuwa Katibu Mkuu Ndugu Sixtus
Raphael Mapunda aliandika barua kwa Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini na
kumpeleka nakala Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi ili
kuikabidhi Hati ya Shamba la Igumbilo.
Machi 29 mwaka 2015
“Special; Resolution Letter” ilisainiwa kati ya Mwenyekiti wa Baraza la
Wadhamini Dk. Emmanuel Nchimbi na aliyekuwa Katibu Mkuu wa UVCCM Ndugu
Sixtus Mapunda ili kuonesha “deed of surrender of right of occupancy”.
UTARATIBU WA UUZAJI WA MALI ZA JUMUIYA NGAZI YA MKOA
Umoja wa Vijana wa CCM una taratibu zake za uuzaji wa Mali ngazi za
Mkoa. Kamati ya Utekelezaji Mkoa itaketi kwa niaba ya Baraza Kuu la Mkoa
kuomba kuuza sehemu walioafikiana katika kikao na kuomba ushauri na
miongozo vikao vya juu.
Kamati ya Utekelezaji Taifa
italichanganua pendekezo na kuona kama kuna umuhimu huo na kupendekeza
kwa Baraza la Wadhamini. Baraza la Wadhamini litaangalia na kukubaliana
au kukataa na kurudisha majibu hayo kwa Mkoa husika.
Katika
kadhia hii kilichofanyika ni Kamati ya Utekelezaji Mkoa wa Iringa
walikaa na kupendekeza kuomba wapatiwe Hati Makao Makuu ratibu za
kubadilisha matumizina si uuzaji wa eneo kama walivyokubaliana wao
kuuza.
Wakati wakiyafanya hayo hapakuwa na kikao cha Sekretarieti
ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa, Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu wala
Baraza la Wadhamini vilivyoketi kwa ajili ya utoaji wa Hati au kubariki
uuzaji wa eneo la Igumbilo Mkoani Iringa.
Aliyekuwa Katibu wa
UVCCM Mkoa wa Iringa Ndugu Ali Nyawenga aliandika barua kwa aliyekuwa
Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa kuhusu ombi la mgawanyo wa viwanja ambapo
kuanzia kitalu Na. EE 217 – 242 vitakuwa chini ya umiliki wa Ndugu
Suhail likiwa na viwanja 25 vyenye ukubwa tofauti.
Kuanzia Kitalu
Nambari EE Namba 161 – 216 viliuzwa kwa wananchi mbali mbali, baadhi ya
watumishi wa Chama, Jumuiya na Makao Makuu huku Kamati ya uchunguzi
ikapata idadi ndogo ya watu waliouziwa kwa uthibitisho wa Risiti na
Mikataba.
Kutokana na mapungufu hayo Baraza Kuu la UVCCM Taifa limeamua yafuatayo:-
Kumsimamisha nafasi zote za uongozi ili kupisha uchunguzi Ndugu Seki
Kasuga Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa na
Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa kutokea Mkoa wa Iringa.
Kumsimamisha nafasi zote za uongozi Ndugu Omar Sleiman Mkuu wa Idara ya
Uchumi, Uwezeshaji na Fedha wa UVCCM Taifa na Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya
ya Mjini – Zanzibar.
Kumfukuza Kazi Ndugu Ally Nyawenga kwa
kuuza viwanja vya UVCCM na kuzigawa fedha alizozikusanya kwa baadhi ya
viongozi wa Chama Cha Mapinduzi mkoa UVCCM Taifa.
Katibu Muhtasi
Upendo Kinyunyu, kwa makusudi aliamua kupotosha taarifa zote alizotoa
kwa kamati ya uchunguzi ili kamati ishindwe kubaini ukweli . Aliweza
kufuta taarifa na kuficha nyaraka zote ndani ya kompyuta ili kupoteza
ushahidi. Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa imeiagiza
Sekretarieti ya UVCCM Taifa kumfukuza Kazi Ndugu Upendo.
Kamati
ya Utekelezaji ya UVCCM Taifa imewairudisha Kazini Makatibu wa UVCCM
Wilaya zote za Mkoa wa Iringa waliokuwa wamesimamishwa kwa tuhuma ya
kupewa viwanja. Kamati imejiridhisha hawakuwa na hatia.
Ndugu
Elisha Mwampashi aliyekuwa Katibu wa UVCCM Mkoa, ambaye sasa ni Katibu
wa CCM Wilaya ya Iringa Mjini, amekiuka Kanuni za uuzwaji wa eneo la
shamba la Igumbilo akiwa Msimamizi Mkuu wa Kanuni ya UVCCM Mkoa Iringa
kwa wakati huo.
Hakutoa ufafanuzi wa wazi juu ya matumizi ya
fedha zilizoingizwa kwenye Akiba ya UVCCM Mkoa Iringa, ameratibu uuzwaji
na upimaji wa eneo la shamba bila kupata idhini ya vikao vya juu ilihal
akijua kuwa kufanya hivyo ni ukiukaji wa Kanuni, Maadili na Katiba ya
CCM.
Amekataa kukabidhi Ofisi kwa wakati baada ya kuteuliwa kuwa
Katibu wa wilaya ya Iringa Mjini kwa lengo la kuendelea kujinufaisha na
mali za jumuiya, akiuza viwanja baada ya upimaji huku akijua anakiuka
kanuni za jumuiya, alipokea fedha taslim kinyume na utaratibu, akitoa
risiti za uuzwaji viwanja vya UVCCM hali ya kuwa yeye ni Katibu wa CCM
na si Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM.
Baraza Kuu la UVCCM Taifa
baada ya kuonekana mapungufu na ukiukwaji wa maadili ya Utumishi,
Baraza Kuu limeamua tuhuma zao zifikishwe kwa Katibu Mkuu wa CCM ili
naye azifikishe kwenye vikao husika kwa hatua zaidi.
Ndugu Hassan
Mtenga Baraza Kuu la UVCCM Taifa limebaini kuwa amekubali kuuzwa sehemu
ya eneo la shamba, akiwa mjumbe wa kikao huku akijua kanuni
hazikufuatwa, kutosimamia jumuiya na Chama ngazi ya Mkoa kuhusu mali za
UVCCM, amekubali kupokea zawadi ya kiwanja Kitalu EE 242 kutoka kwa
Ndugu Suhail ambaye ndiye mnunuzi wa sehemu ya shamba hilo, akashindwa
kuwalisha taarifa wakati wa uuzaji wa viwanja kwa aliyekuwa Katibu wa
UVCCM MkoaIringa Ndugu Nyawenga na pia kushiriki kupokea fedha za mauzo
ya viwanja.
Baraza Kuu la UVCCM Taifa baada ya kupokea Taarifa
ya Kamati ya uchunguzi imeonyesha mapungufu na ukiukaji wa Maadili ya
kiutumishi na kupendekeza tuhuma hizo zifikishwe Ofisi ya Katibu Mkuu wa
CCM kwa hatua zaidi.
Ndugu Sixtus Rapheal Mapunda Baraza limebaini mambo yafuatayo:
Kuchukua Hati ya UVCCM bila idhini ya kikao husika. Hakutoa taarifa
rasmi kwa Mwenyekiti au kikao cha Kamati ya Utekelezaji Taifa kuhusu
maombi ya UVCCM Mkoa wa Iringa ya kubadilisha matumizi ya eneo.
Hakutoa taarifa ingawa kulikuwa na vikao vingi vya Kamati ya Utekelezaji na sekretariet kuhusu shamba la Igumbilo.
Alipokea fedha za mgao wa mauzo toka kwa aliyekuwa Katibu wa UVCCM Mkoa wa Iringa Ali Nyawenga
Kutojibu barua ya maombi kutoka Mkoa wa Iringa kwa maandishi japokuwa barua zililetwa Makao Makuu.
Kuamua kupeleka Hati ya shamba Mkoani Iringa bila vikao vya maamuzi kuvishiriskisha na kuamua.
Alishindwa kutimiza wajibu wake kikanuni kwa kutosimamia majukumu yake ya kila siku akiwa na dhamana ya Katibu Mkuu.
Kuna upotevu mkubwa wa nyaraka husika ndani ya Ofisi yake wakati akiwa na wadhifa wa Katiba Mkuu.
Kutumia vibaya madaraka aliokuwa hayo, akiwashawishi walio chini yake
kuvunja kanuni na taratibu za CCM pamoja na kuihujumu jumuiya na mali
zake akiwa na dhama ya Katibu Mkuu wa UVCCM huku akiwa na dhamana ya
usimamizi na utunzaji Mali za Jumuiya.
Baraza Kuu la UVCCM
Taifa limeamua baada ya kuona kuna ukiukaji wa Maadili na taratibu
uliosababisha sakata la shamba huko Igumbilo, tuhuma hizo dhidi yake
zifikishwe kwa Katibu Mkuu wa CCM kwa hatua zaidi.
Ndugu Suhail
Ismail Baraza Baraza Kuu la UVCCM Taifa limeamua juu ya eneo alilouziwa
kimakosa na Viongozi wa UVCCM Mkoa wa Iringa ambalo analimiliki Kisheria
(ana Hati halali) ya eneo hilo lenye viwanja 25.
Baraza Kuu la Umoja wa Vijana Taifa limeamua kurudisha umiliki wa eneo hilo Kisheria.
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi tunawaomba tunawashauri na
tunasisitiza kwa Chama Cha Mapinduzi watimize wajibu wao katika
kuwachukulia hatua kali za kinidhamu wale wote waliohusika na kadhia hii
ambao wako kwenye mamlaka yao ili kurudisha heshima na nidhamu ya
Chama.
Ndugu Waandishi wa habari
Umoja wa Vijana wa CCM
kuanzia mwezi wa Desemba, 2015 ulianza kujitathimini na kuweka mikakati
ya kufanya mabadiliko ya kimfumo, kiutawala na kiuendeshaji ili kukidhi
haja ya muda tulionao katika kuiongoza Taasisi hii kitaalamu zaidi.
Umoja wa Vijana iliunda Kamati ndogo ndogo kutathimini miradi yake
ambayo ilionekana kuna upotevu mkubwa wa fedha za Jumuiya kama
ifuatavyo:-
Kinondoni Malipo ya mafao ya Watumishi (NSSF) Kupitia migogoro ya ucheleweshaji wa utekelezaji mikataba mbalimbali na kadhalika.
Ripoti za Kamati hizo zinaendelea kufanyiwa kazi hatua kwa hatua.
Katika Hatua ya awali Umoja wa Vijana wa CCM uliomba kwa Katibu Mkuu wa
CCM kupatiwa wakaguzi wa hesabu ili kukagua miradi yote ya UVCCM
Taifa. Awamu ya kwanza ya ukaguzi umeanza katika miradi ya:
Majengo pacha ya uwekezaji Makao Makuu Dar es Salaam
Mradi wa Uwekezaji wa Vibanda vya Kinondoni
Kukagua matumizi ya Malipo mbali mbali (Watumishi, Mishahara na shughuli zote za Utawala)
Awamu ya pili ukaguzi wa hesabu unaendelea katika miradi wa Uwekezaji Darajani Zanzibar Mradi wa Gymkhana Zanzibar Shamba la Vijana Tunguu Shamba la Vijana Ihemi Matumizi ya Mkutano Maalum wa ushirikiano kati ya UVCCM na nchi rafiki uliofanyika Arusha Miradi yote midogo midogo
Sambamba na hilo UVCCM inaendelea na zoezi la uhakiki wa watumishi wake
wote na Mali zake ngazi ya Taifa hadi Wilaya na baada ya kukamilika
ripoti zote zitawasilishwa kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli.
Ndugu Waandishi wa Habari
Mwisho kwa upande wa Baraza la kuu UVCCM Taifa kwa ujumla liliazimia yafuatayo:
Baraza kuu la Umoja wa Vijana wa CCM Taifa, tunampongeza Mwenyekiti wa
CCM Rais Dk John Magufuli na Serikali yake kwa Kazi kubwa, Utendaji
unaotia matumaini wenye lengo la kuwahudumia wote bila ya kujali itikadi
za kisiasa, rangi, kabila au jinsia.
2. Baraza Kuu la UVCCM ,
tunaiagiza Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, kupitia Wizara yenye
dhamana, itenge maeneo maalum kwa ajili ya vijana ili waweze kufanya
shughuli za uzalishaji mali na biashara bila kupata bughudha au
usumbufu wowote.
Baraza Kuu la UVCCM Taifa tunaigiza serikali
kwamba, Halmashauri yoyote nchini ambayo itashindwa kutoa asilimia 5 ya
Mapato yatokanayo na Vyanzo vya Mapato kwa makundi ya Wanawake na Vijana
katika mpango wa kuwapatia mikopo, ipewe Hati chafu ili kuzihimiza
Halmashauri nyingine kutambua umuhimu wa kutenga asilimia 5.
Aidha Baraza Kuu la UVCCM, limewaagiza Viongozi wa Jumuiya hiyo katika
ngazi zote nchini, wasikilize kero za Vijana, kusaidia katika
kukabiliana nazo na kuziwakilisha katika ngazi husika kwa ajili ya
kuzitafutia utatuzi. Aidha viongozi wote wawe karibu na vijana katika
maeneo yao kwa dhumuni la kubaini kwa haraka changamoto zinazowakabili
na kuwatatiza.
Baraza kuu la UVCCM, tunatoa wito kwa viongozi
wote kuwahamasisha vijana ili wajiunge katika vikundi na kufuata
taratibu za kisheria ili kupata usajili, wawasimamie ili kufungua
Akaunti Benki hatimaye fedha zitakazotolewa na serikali kwa ajili ya
kupatiwa mikopo ziende kwenye vikundi hivyo na kuwa rahisi kukopesheka
hususan baada ya kupata elimu ya mikopo na ujasiriamali.
Baraza kuu la UVCCM liamizia mali zote za jumuiya zikaguliwe zitambuliwe na zioneshe jinsi zinavyonufaisha taasisi.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Shaka Hamdu Shaka (MNEC)
KAIMU KATIBU MKUU |
0 comments:
Post a Comment