Wednesday, August 17, 2016



Mwanafalsafa maarufu wa Ufaransa Baron De Montesquieu mtalamu wa Sheria pamoja na masuala ya utawala katika Ulaya mnamo karne ya kumi na nane aliwahi kuainisha aina tatu za tawala katika Mataifa,
Aina ya kwanza ni tawala za Kifalme (Monarch) zinazoongozwa na Wafalme au Malikia, tawala za pili ni zile tawala za Kijamhuri (Republic) ambazo huongozwa na kiongozi mkuu wa nchi ambaye huchaguliwa na wananchi na aina ya tatu ni zile tawala za Kiimla au kidikteta (Depotism). 

Tanzania tunaongozwa kwa kutumia Tawala ya Kijamhuri ambapo Rais na Chama Tawala huchaguliwa kwa kura za Wananchi.  Pia tunajiongoza kwa kutumia Demokrasia ambayo mahali popote Duniani huongozwa na Sheria, na Serikali huongozwa na Taasisi inayoitwa Dola ambayo inahodhi mamlaka tatu muhimu Serikali, Bunge na Mahakama. Mihimili hii mitatu inaundwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 kuanzia Kipengele cha Pili mpaka cha Sita ambapo umetolewa ufafanuzi wa kina namna Mihimili hii inavyotakiwa kufanya kazi kwa uhuru bila kuingiliwa na mwingine kwa manufaa ya umma.


Tanzania pia tunajiongoza kwa kutumia Demokrasia ambapo kila mwananchi anakuwa na haki ya kusikia na pia kupewa haki zake zinazolindwa Katiba. Ndio maana Serikali yetu Mwaka 1977 kwa kutumia Katiba ya Jamhuri Kipengele Namba 129 iliunda rasmi Tume ya Haki za Binadam na Utawala bora (CHRAGG) kama chombo chake huru cha kulinda haki za wananchi na kusimamia utawala bora pamoja na kuchunguza malalamiko ya ukiukwaji wa haki za wananchi na hata kwenda kwenye Sheria inapobidi. Rais wa Tanzania ndiye Amiri Jeshi Mkuu ambaye moja ya kazi zake ni pamoja na kusimamia vyombo vya Dola na kuhakikisha Sheria zilizotungwa na Bunge zinatekelezwa kwa mujibu wa Katiba, kwenye kulitimiza hilo Rais huteuwa wasaidizi wa kumsaidia kwenye kazi hizo. Kwa hiyo linapotokea tatizo lolote la Kitaifa au Kisiasa linatakiwa kufikishwa aidha Mahakamani, Bungeni au kwenye Dola, lakini sio mahali popote pengine. Kama ni tatizo la Vyama vyetu vya siasa Katiba ipo wazi kwamba Msajili wa Vyama vya saisa atahusishwa namna ya kulimaliza au kuishauri Serikali namna ya kulimaliza kama kweli lipo tatizo.

 Kwa mantiki hii basi kitendo cha Tume ya Haki za Binadam na Utawala Bora kuwaita Mkuu wa Polisi na Mwanasheria Mkuu hakihalalishwi mahali popote kwenye Katiba yetu, na hata kuwaita CCM na Chadema waje meza moja bado sio kazi yao inatakiwa kuwa kazi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini. Kwa hiyo kitendo cha CCM, IGP na AG kutohudhuria kikao hicho ni halali kabisa kwa sababu IGP na AG ni wateule wa Rais au Mhimili wa Dola sasa Dola inaitwaje na Tume tu ni kichekesho kikubwa sana kwa utawala tunaofuata wa Demokrasia na mgawanyo wa madaraka kwa Mihimili Mitatu mikuu ya Taifa.Tume ya Haki za Binadam na Utawala Bora haina mamlaka Kikatiba ya kuwaita wateule wa Rais kwa ajili ya kuwahoji namna wanavyotekeleza wajibu wao kwaa melekezo ya Kikatiba chini ya Rais wa Jamhuri. Lakini Tume hiyo inaweza kwende mahakamani au kumshauri Rais iwapo itaona kuna tatizo la ukiukwaji wa haki za wananchi ambao mpaka sasa haujatokea bado isipokuwa kuna uvunjwaji mwingi wa sheria ambao umekuwa ukifanywa na Wapinzani kwa kisingizio cha kubanwa Demokrasia.


Na mwisho ni kwamba hakuna tatizo kama tatizo ambalo litashindwa kutatulika kwa kukataa kwa CCM, IGP na AG kuhudhuria kikao hicho cha Tume kuwakutanisha na Chadema, hapana lililopo ni uvunjwaji wa Sheria unaofanywa na Chadema ambao vyombo vya Dola vimekuwa imara sana kwenye kuthibiti tatizo hilo. Ninarudia tena kama lipo ni tatizo linalotakiwa kumalizwa na Sheria, lakini sio mkutano kama huo uliopangwa na Tume ya Haki ambayo huenda hapa inaweza kuwa imepitiliza mipaka yake ya kikazi Kikatiba. Iwapo wangekubali kuhudhuria kikao hicho basi Kikatiba ingeleta hata mgogoro wa Kikatiba kwa sababu ingemaanisha Tume hiyo kuwa juu ya Dola, Bunge na Mahakama vyombo vitatu vikuu ambavyo pekee tu ndio vina uwezo wa kuwaita wahusika wote hao lakini sio Tume ya Haki za Binadam na Utawala Bora kwa sababu hawana hayo mamlaka.

By:- William Malecela.

Imechapishwa Gazeti la Jambo Leo Tarehe 16/8/2016 na kila JUMANNE.


0 comments:

Post a Comment