Terehe 8/6/2016 Serikali kupitia Polisi
ilipiga marufuku mikusanyiko au maandamano ya Vyama vya siasa nchini kwa madai
ya kuwa na taarifa za kiintelinjisia za baadhi ya vyama vya siasa kutaka
kuvuruga amani nchini kwa kisingizo cha Demokrasia.
Demokrasia ni mfumo wa
Serikali ambao mamlaka kuu inakuwa na jukumu la kutekeleza maamuzi ya Wananchi
wake aidha moja kwa moja au kupitia mfumo wa Uwakilishi, lakini yote hufanyika
kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri. Kwa mujibu wa kipengele cha 5 Sheria ya Vyama
vya Siasa Tanzania ya Mwaka 1992 "Chama cha siasa"
maana yake ni
kikundi chochote kinachoundwa kwa kutumia Katiba ya Chama kile kwa lengo la kushindana
kuongoza Serikali, au Serikali za Mitaa katika Jamhuri ya Muungano, kwa njia ya
uchaguzi ambao Wananchi kupiga kura na kuchagua Chama cha Siasa wanachokitaka
kiwatawale. Katika Uchaguzi wa mwisho hapa nchini Wananchi wengi waliichagua
CCM kuwaongoza tena kwa Miaka 5 ikiwa sasa tuna miezi 10 tu toka uchaguzi huo
uishe, tayari kumetokea matukio mengi kutoka kwa walioshindwa uchaguzi huo
wakijificha nyuma ya mgongo wa Demokrasia. Kwamba eti Serikali iliyopo
madarakani sasa hivi haiheshimu Demokrasia na mara kwa mara wamekuwa
wakiitishia Serikali hii kuandamana au kutumia fujo ili kuona Serikali inatumia
Demokrasia katika kuishi nao yaani Wapinzani. Chokonoa chokonoa ya Wapinzani
iliipelekea Serikali kupiga marufuku mikutano au mikusanyiko yote ya vyama vya
siasa nchini kwa muda.
Mwenyekiti wa Chama cha Maarufu cha
Upinzani nchini TLP Mh. Augustine Mrema, aliwahi kusema "Demokrasia isiyothibitiwa
ni magofu. Hatupaswi kuruhusu hili kutokea katika nchi yetu ". Na kama
Mwanasiasa mashuhuri Duniani Norman Mailer alivyowahi kusema “Vita vyovyote
ambavyo vinahitaji wapiganaji kupoteza fahamu kwanza ndio wapigane ni vita
vibovu na havifai” Mrema kama Mailer wote wapo sawa katika maoni yao ambayo,
kwa hakika, yana anzisha somo muhimu katika vipengele muhimu vya mfumo wa vyama
vingi na somo zima la 'elimu ya siasa,demokrasia na uhuru' katika Taifa kama
letu hasa ukizingatia maneno mazito yaliyowahi kutamkwa na Mwenyekiti Mao
Tsetung kwamba “Bila utafiti, hakuna haki ya kuongea”. Vyama vingi vya siasa
nchini hasa vya Upinzani vimekuwa vikipingana na Serikali ya sasa kwa
kisingizio cha Demokrasia ambayo kiuhalisia vinakosa hoja nzito na za msingi.
Kwa mfano hata Marekani kunakoaminika kuwepo kwa Demokrasia ya kweli bado
ukivaa fulana inayomsifia Bin Laden unakuwa umevunja Sheria za Taifa hilo kubwa
Duniani. Rais wa zamani wa Marekani aliwahi kusema “Hakuna Demokrasia isiyokuwa
na mipaka” ingawa pia wote tunajua kimsingi kwamba kazi namba moja ya Wapinzani
ni kupingana na Serikali kistaarabu katika kuelekezana ili kulisaidia Taifa na
sio sababu nyingine yoyote.
Tukio hili la Serikali kupiga
marufuku maandamano na mikusanyiko sio geni Duniani, kwa mfano Tarehe 13/2/2015
Serikali ya Uingereza ambako tunaamini kuna Demokrasia iliyokomaa kwa miaka
zaidi ya 300 kuliko yetu yenye Miaka 50 tu iliwakatalia kina Mama wa “Million
Women Raise Demonstration” kwa kuhofia
vurugu kwenye maandamano hayo. Tarehe 15/4/2016 Manispaa ya Hollywood
ilimkatalia kibali cha mkusanyiko mgombea urais wa Marekani kwa Chama cha
Republican Donald Trump kwa sababu zile zile kama za Serikali ya Tanzania za
kuepusha vurugu, Meya wa mji huo Bw. Harvath alisema Polisi wake wanazo habazi
za kutosha za kiintelijisia za kupangwa kufanyika vurugu kwenye mkusanyiko huko
na kwamba kipengele cha Katiba ya nchi hiyo “The First Ammendment” ambacho
kinalinda matukio kama hayo bado hakina nguvu ya kuilazimisha Serikali ya
Manispaa kuruhusu mkusanyiko huo. Mwaka 1949 Serikali ya Marekani ilipiga
marufuku mkusanyiko au maandamano yoyote kufanyika kwenye eneo la Mahakama Kuu
ya nchi inayojulikana kwa jina maarufu kama “Supreme Court”.Mwanasiasa Maarufu
duniani Winston Churchhil aliwahi kusema ‘’Hoja bora dhidi ya demokrasia ni
dakika tano ya mazungumzo na wapiga kura wa kawaida kwa mujibu wa Katiba ya
Nchi.”
Ikiwa na maana kwamba kama Serikali inakosea ni muhimu sana kuwepo na ukumbushwaji
kutoka kwa wahusika ambao ni Upinzani lakini kwa njia ya kuheshimu Katiba ya
Nchi.
Watanzania kwenye uchaguzi uliopita
tulikuwa tunakubaliana kwa kauli moja kwamba tunataka mabadiliko, tulikuwa
tumechoshwa kabisa ya jinsi tulivyokuwa tukijitawala huko nyuma na kwa bahati
nzuri tukampata Rais Magufuli ambaye katika hotuba zake zote za Kampeni aliweka
wazi dhamira yake ya mabadiliko akiwa Rais. Sasa baada ya kuwa amekuwa
akijaribu sana kuliondosha Taifa kwenye matumizi yasiyokuwa na tija kama
kutumia mapesa mengi sana kwa ajili ya sherehe huku wananchi wakiteseka
mahospitalini na wanafunzi kukosa madawati shuleni. Pia Rais Magufuli alisitisha
tabia ya kuonyesha Bunge letu asubuhi kwenye TV ya TBC na badala yake kuonyeshwa
usiku kukwepa gharama ya kutumia pesa za Serikali Shillingi karibu Billioni 4
kila mwezi kwa sababu ya kuonyesha “Bunge live” tu. Katika kuhakikisha Bunge la
Wananchi linaendeshwa kwa heshima na nidhamu kama Sheria ya Bunge inavyotaka,
mamlaka ya Bunge imetoa adhabu nzito sana kwa Wabunge wote waliovunja Sheria
hizo ambapo pia kabla ya kupewa adhabu hizo Wabunge hao waliitwa na kupewa
nafasi ya kujietetea kama Demokrasia ya Dunia nzima inavyotaka. Haya yote ni
mabadiliko ambayo sisi wenyewe kwa kumchagua Rais Magufuli, tulikuwa tunajua
kwamba yanakuja.
Hakuna kitu kigumu katika maisha ya
mwanadamu kama Mabadiliko au “Change” na hasa kama ni mabadiliko kama ya siasa
yetu Tanzania ya kutoka kwenye kona ya kawaida kwenda kwenye kona mya
isiyojulikana au inayojulikana kwa Rais mpya aliyechaguliwa kama wetu ambaye
aliyaimba sana mabadiliko haya kwenye kampeni zake za urais. Mabadiliko ya
kweli kama tuliyonayo sasa hivi hapa nchini huwa yanakuja kwa wakati muafaka
kama tuliokuwa nao wakati wa uchaguzi na mabadiliko hayalazimishwi, na
haijawahi kutokea Duniani mabadiliko yakawa matamu. Siku zote Mabadiliko muhimu
na mazuri kwa maendeleo ya binadam huja na maumivu makubwa sana kwa wahusika
yaani Wananchi.
Na Ni jukumu sahihi la vyama vya siasa katika mazingira yetu
siasa kuhakikisha kwamba vinaiweka Serikali katika mstari wa Sheria kwenye
kutimiza mabadiliko haya kwa sababu historia nyingi zinaonyesha ni rahisi sana
kwa Serikali kwenda nje ya mstari wa Demokrasia kwenye kuleta mabadiliko kitu
ambacho bado Serikali ya Rais Magufuli haijakifanya bado pamoja na makelele
mengi ya Upinzani kwamba wanaiminya Demokrasia.
Kupigwa marufuku mikutano ya vyama
vya siasa inatakiwa uwepo wa 'uelewa wa siasa juu ya demokrasia na uhuru'
ambayo faida yake ni nadra sana kuipata tu kutoka kwa viongozi ambao
maslahi yao ni kujenga ghasia katika nchi yetu ya amani. Demokrasia
inaweza kukiukwa kwa bahati mbaya kwenye mchakato wa mabadiliko lakini huwezi
kuirekebisha Serikali kwa kutumia fujo na vurugu kwa sababu Katiba inaipa
nafasi Serikali kutumia vyombo vyake vya dola kuthibiti waleta vurugu.
Katiba
inatoa nafasi kwa vyama vyote husika kupiga kampeni kwa siku 60 na baada ya
uchaguzi kuisha bado Katiba inatoa nafasi ya malumbano ya kisiasa kuhamia
Bungeni baina ya watawala na Wapinzani. Sasa kama ukifikia kushindwa kutumia
jukwaa la Bunge kujenga hoja za kuirekebisha Serikali mpaka kufikia kuvunja
kanuni za Bunge na kuadhibiwa, maana yake ni kwamba aidha umefilisika kisiasa
au hujui sababu ya kuwepo kwako kwenye mfumo wetu wa siasa. Demokrasia
inaongozwa na Sheria na inapatikana kwa kutumia Sheria, lakini haiwezi
kupatikana au kurekebishwa kwa kutumia fujo na vurugu. Fujo na vurugu kwa
kutumia mgongo wa Demokrasia ni hatari kwa Taifa kwa sababu kikundi kidogo cha
Upinzani kwenye Taifa kikiruhusiwa kufanya vurugu na fujo kuonyesha
kutoridhishwa na nchi inavyoendeshwa ina maana ya kuwapa nafasi kundi kubwa la
Chama tawala linaloliridhika na nchi invyoendeshwa kufanya fujo na vurugu
kuwapinga Wapinzani. Serikali yoyote duniani haiwezi kukaa pembeni na kuruhusu
ukiukwaji huu wa Demokrasia, Serikali iheshimu sheria za jamhuri na vyama vya
siasa pia viheshimu Sheria mpaka sasa Serikali haijaonyesha kuvunja Sheria zake
za kuheshimu Demokrasia, lakini Wapinzani wanaonekana kukosa agenda ya kisiasa
kwa wananchi katika kipindi hiki cha mabadiliko tuliyoyataka wenyewe wananchi
wengi wa Tanzania.
MUNGU IBARIKI TANZANIA
William Malecela aka Le Mutuz
Nation Cell:- +255 717 618 997 Email:- willymalec@gmail.com

0 comments:
Post a Comment