Posted by Williammalecela.com on Wednesday, August 24, 2016
 |
TAARIFA YA MHE. FREEMAN AIKAELI MBOWE KUHUSU MADAI YA NHC.
Nimepata taarifa ya mkutano wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la
Taifa (NHC) na Waandishi wa habari kuhusu kilichoitwa "wadaiwa sugu"
wa
NHC ambapo katika orodha hiyo kampuni ambayo nina hisa ya Mbowe Hotels
Co.Ltd imeorodheshwa kama mdaiwa anayedaiwa zaidi ya Shilingi Bilioni
moja.
Nakiri kuwepo kwa mgogoro wa kibiashara wa miaka mingi
baina ya Kampuni hii na NHC. Aidha kampuni hii imekuwa ikilipa kodi
stahiki kwa NHC kwa mujibu wa makubaliano yetu ya kibiashara.
Kumekuwepo na ukakasi wa muda mrefu kuhusiana na mkataba wetu wa
umiliki, uendelezaji na uendeshaji wa jengo hili unaochagizwa na
msimamo wangu wa kisiasa.
Haki na Uhuru wetu wa kufanya biashara
kama raia wengine umekuwa ukiingiliwa mara kwa mara katika mazingira
yanayoambatana na Vitisho kiasi ambacho Maamuzi kadhaa hayafanyiki kwa
hofu ya kisiasa kwamba "Itakuwa kumwongezea nguvu Mpinzani".
Hivyo, ningependa umma wa Watanzania uelewe kuwa sidaiwi na Shirika la Nyumba la Taifa(NHC).
Kufuatia utata huu wanasheria wa Kampuni wanashughulikia jambo hili kwa taratibu za kibiashara na kisheria.
Naomba kuweka wazi kwa yeyote anayehusika. Sitafungwa fikra, sitafungwa
mdomo na sitaacha kuutetea Ukweli, Haki na Demokrasia katika nchi hii
kwa misingi ya "kulinda kinachodhaniwa ni maslahi yangu ya kibiashara".
Wafanyabiashara wengi wanafungwa fikra na midomo ndani ya nchi hii kwa kuogopa hila na ghiliba za watawala.
Ni heri kufa masikini nikiwa nimesimamia ukweli, kuliko kuishi tajiri niliyetawaliwa na ubinafsi, woga, hofu na ubatili.
Natambua kuna jitihada za kutumia kila silaha na kila hila dhidi yetu katika Kipindi hiki.
Mwisho, Natoa rai kwa wanachama na wapenzi wa Haki katika Taifa hili,
wasiogope. Haki itaweza kucheleweshwa kwa muda tu, lakini kamwe haiwezi
kuzuiwa. Binadamu akikufungia mlango Mungu wa Haki atakufungulia
dirisha.
Ubatili ni wa mpito lakini Haki ni ya milele.
Imetolewa
Leo Jumatano Agosti 24,2016 Na:
Freeman Aikaeli Mbowe
Mfanyabiashara.
|
0 comments:
Post a Comment