TAMASHA la bendi za Tanzania lililofanyika Leaders Club Jumamosi usiku
ni habari njema kwa wapenzi wa muziki wa dansi, ni mwarubaini na nuru ya
kuukwamua muziki huo unaoonekana kudumaa.
Tamasha hilo lililojulikana kama Tanzania Band Festival, linapaswa
kuwaamsha wadhamini ambao wamekuwa wakiwekeza nguvu nyingi kwenye muziki wa
kizazi kipya ambao hutawaliwa zaidi na mfumo wa kutumia CD (Playback).
Muziki wa bendi (live) hususan ule wa dansi, ndiyo muziki wa ukweli,
muziki ghali, muziki unaotoa ajira kubwa, hivyo anapotokea mwandaaji kama Q
Plus umma wa wapenda dansi unastahili kushukuru na kuunga mkono hasa kutokana
na ukweli kuwa ‘wawekezaji’ (mapromota)
wengi hawaamini katika kuwekeza kwenye muziki wa dansi.
Q Plus walifanya kila njia kuhakikisha tamasha linanoga kuanzia
usalama wa eneo la tukio, mapambo ya kisasa, sound bab kubwa na jukwaa lenye
hadhi ya kimataifa …Lakini pamoja na yote hayo, pamoja na nia na dhamira nzuri
ya waandaaji, yapo mapungufu kadhaa ambayo Q Plus na washirika wao wanastahili
kuyafanyia kazi katika siku zijazo hasa kutokana na ahadi yao kuwa tamasha lile
litakuwa likifanyika kila mwaka. Nitataja mapungufu saba niliyoyaona.
Kwanza kabisa ni
kiingilio: Shilingi 15,000 kwa usawa wa leo si mchezo – unapozungumzia kiasi
hicho cha pesa maana yake mtu anapaswa kuwa na pesa isiyopungua elfu 25 ili
angalau aweze kuchukua usafiri wa boda boda wa kwenda na kuondoka Leaders Club,
awe na uwezo japo wa kunywa chupa moja ya soda. Nadhani shilingi 10,000
ingekuwa muafaka zaidi.
Muda wa onyesho: Kutangaza kuwa
onyesho lingeanza saa 5 asubuhi ilikuwa ni kosa la kiufundi, naamini wako wengi
waliohofia kwenda eneo la tukio saa 2 za usiku kwa kuamini kuwa nusu ya ratiba
itakuwa imewapita – onyesho lilianza saa 12 za jioni, tupunguze ushawishi usio
na tija na uliopambwa na chembe chembe za uongo.
Muda wa bendi
kukaa jukwaani: Hili nitaliesemea kwa urefu zaidi. Mwanzo tuliambiwa kila
bendi itakaa jukwaani kwa dakika 45, lakini baadae zikapungua hadi 30 na
mwishowe ikawa 20 – hii maana yake ni kwamba waandaji hawakupiga hesabu nzuri
za masaa ya onyesho lao kwa kugawanya na idadi ya bendi, matokeo yake kadri
muda ulivyokuwa ukienda ndivyo walivyoona kuwa ipo hatari ya bendi nyingine
kukosa kabisa muda wa kupanda jukwaani – suluhisho likawa kupunguza muda
katikati ya tamasha.
Hakukuwa na ulazima wa bendi zote kulingana muda wa kukaa jukwaani -
QS International Band kupata dakika 45 halafu FM Academia ipate dakika 20 halikuwa
jambo sahihi.
Tukubali tusikubali, katika katika tamasha lile, zilikuwepo bendi
ambazo piga ua ndiyo zilikuwa chambo cha kuleta wateja wengi (crowd puller) –
Nitazitaja bila woga: FM Academia, Twanga Pepeta, Msondo Ngoma, Sikinde, Yamoto
Band na Malaika ya Christian Bella ambayo haikuwepo Leaders kama matangazo
yalivyoashiria – hizi zilipaswa kupewa
kipaumbele katika muda wa kukaa jukwaani.
Wako watakaotaka kujua vigezo nilivyotumia kuzitaja bendi hizo kama
“crowd puller”. Nitafafanua: Matokeo ya show ya Twanga na FM pale Escape One
yanajulikana, matokea ya show ya miaka 37 ya Sikinde iliyosindikizwa na FM yanajulikana,
matokeo ya show za mpambano wa Sikinde na Msondo yanajulikana – yote yalifana
sana, moto wa Yamoto Band unajulikana.
Utitiri wa bendi: Kwa kuanzia,
tamasha kama hili halikupaswa kuwa na bendi nyingi, bendi sita au saba
zingetosha sana, hii ingetoa nafasi kwa bendi kutumbuiza kwa muda wa kutosha,
ingepunguza gharama za onyesho na hivyo kusaidia kupungua kwa bei ya kiingilio
- Wako pia mashabiki wanaokataa kwenda kwenye maonyesho yenye msururu wa bendi
nyingi kwa kuhofia kuwa bendi aipendayo haitatumbuiza kwa muda mrefu – kwamba
anaweza kulazimika kukaa hadi saa 9 za usiku kuisubiri bendi aipendayo na kisha
ikapiga wimbo mmoja tu.
Dhumuni la
tamasha halikueleweka: Wengi tulidhani ni tamasha la bendi za muziki wa
dansi, lakini inavyoelekea waandaaji walijali neno “BAND” bila kujali ni bendi
ya aina gani ya muziki, iwe dansi, reggae, chakacha, afro pop, haikujalisha.
Bendi kama B Band, Top Band na QS hazikuendana na dhana tuliowekewa
kichwani kuwa tamasha lilikuwa maalum kwaajili ya kunyanyua muziki wa dansi - sina
tatizo sana na Skylight Band ingawa huwezi kuitaja kama bendi ya dansi kwa
asilimia 100, sina tatizo na Yamoto Band ambayo licha ya kukaa ki-bongo fleva,
lakini wanachokifanya jukwaani ni muziki wa dansi kwa sana tu.
Promosheni: Waandaaji
walipaswa kujitanua zaidi kwa kutumia vituo vingi vya radio hususan vile
vinavyoutendea haki muziki wa dansi. Hili lina gharama lakini lingewezekana
kama waandaji wangepunguza baadhi ya mambo ikiwemo kupunguza msururu wa bendi
nyingi. Naiamini sana media iliyobeba show (Clouds Media), lakini ingependeza
zaidi kama matangazo yangepenya kwenye vituo vingine vya radio na hata
televisheni ikibidi.
Eneo la tukio: Kwasasa napata
shaka kuamini kuwa Leaders Club ni sehemu sahihi ya kufanyia matamasha ya
muziki wa dansi kulinganisha na sehemu kama TCC Club ambayo nina uhakika
gharama zake ni nafuu zaidi.


0 comments:
Post a Comment