Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuendeleza eneo la viwanda vya usindikaji mazao la Mkulazi Morogoro ili liwe kielelezo kikuu cha ukanda maalum wa kiuchumi (SEZ) unaoambaa sambamba na reli ya TAZARA.
Amesema wizara hiyo inapaswa ishirikiane kwa karibu na Mamlaka ya Uendelezaji Kanda Maalum za Kiuchumi (EPZA) pamoja na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Agosti 10, 2016) wakati akizungumza na watendaji wa EPZA na wafanyakazi wa kiwanda cha kushona nguo cha Tooku kilichopo eneo la Benjamin William Mkapa, Mabibo External jijini Dar es Salaam.
Pia amewataka wakuu wa mikoa sita ya Pwani, Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe kufanya kazi kwa karibu na EPZA kwa kuainisha maeneo yanayohitaji kuendelezwa kiuchumi ambayo yanafikika kwa urahisi kwa reli ya TAZARA.
“Wekeni mipango yenu kwa umakini ya kuanzishwa kwa kanda maalum za kiuchumi katika maeneo yenu ya kiutawala na mipango hii ijitokeze kwenye mipango ya maendeleo ya mikoa yenu, onesheni mikakati ya uendelezaji viwanda inayoendana na Mpango wa Pili wa Miaka Mitano wa Maendeleo wa Taifa,” amesema.
Amewataka wakuu hao wa mikoa kuhakikisha wanaweka mfumo utakaoimarisha ulinzi wa miundombinu ya reli hiyo ili isiharibiwe na watu wenye nia mbaya.
0 comments:
Post a Comment