SAKATA LILIVYOANZA
Awali
kabla ya Ntibenda kuachishwa kazi na Rais Dk. John Magufuli, Cathy
aliilalamikia Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, ambayo huwa chini ya
mkuu wa mkoa, kwamba imeshindwa kudhibiti suala la shule kuchomwa moto
mkoani humo kila kukicha. Lakini baadhi ya watu wakasema, Cathy
anamtuhumu Ntibenda kwa sababu walikuwa na uhusiano wa karibu sasa
umetibuka. Lakini kuhusu madai hayo, Cathy alisema:“Haiwezekani shule
zikawa kila siku zinaungua, hapa kuna tatizo, Kamati ya Mkoa ya Ulinzi
na Usalama inapaswa kuwajibika, maana inaonekana haifanyi kazi yake kwa
ufasaha.” Alipoulizwa kuhusu madai ya kuhusika kwake katika kuondolewa
kazini kwa Ntibenda, Cathy alisema yeye alizungumza kuhusu kamati hiyo
kushindwa kuwajibika, hivyo haifai na kwamba kama kwa kusema hivyo
kumesababisha aondolewe, ni sawa maana alitimiza wajibu wake kama
kiongozi. “Haiwezekani bwana kila siku shule zinachomwa, ukiuliza kamati
ya ulinzi na usalama inafanya nini? Hakuna majibu ya kueleweka.
Tunataka kupeleka misaada lakini tunashindwa maana hata ukipeleka, shule
zinachomwa katika staili ileile. “Mimi nilisema kama mzazi na nilisema
hadharani kama kiongozi. Kama ametimuliwa kwa sababu ya yale niliyosema
pia ni sawa tu,” alifunguka Cathy.
HAPO NDIPO NTIBENDA UZALENDO ULIPOMSHINDA
Lakini
Ntibenda ambaye wiki iliyopita kwenye Risasi Jumamosi hakuweza
kupatikana na hivyo gazeti kuficha utambulisho wake, safari hii
alipatikana kupitia simu yake ya mkononi, lakini awali alikuwa mgumu
kuzungumzia suala hilo, akidai hataki tena kujihusisha na siasa za
Arusha zaidi ya kuwa mjasiriamali. “Kama unataka kuzungumza na mimi
kuhusu masuala ya ujasiriamali karibu, lakini kama ni mambo ya siasa za
Arusha mimi siko tayari kuzungumzia,” alisema Ntibenda ambaye wakati huo
alisema yupo jijini Dar kwa shughuli zake za kijasiriamali. Wakati
kiongozi huyo akikata simu alisisitiza msimamo wake, mwandishi wetu
aliamua kumtumia ujumbe mfupi wa maandishi, uliosomeka:
“Kuna
taarifa tumepata kwamba kuondolewa kwako kule kwenye ukuu wa mkoa
kumesababishwa na mbunge Cathy Magige, ni kweli?” Muda mfupi baadaye,
Ntibenda alirudi hewani na kuamua kutoa dukuduku lake, akimtupia tuhuma
mbunge huyo kuwa yeye, pamoja na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM
(UVCCM) Mkoa wa Arusha, Lengai Ole Sabaya, walikuwa wakiendesha kampeni
za kumhujumu ili aonekane hawezi kufanya kazi. ‘Yeye (Cathy) anawajua
waliokuwa wakichoma mashule, juhudi zangu kama mkuu wa mkoa
zinajulikana, watu wanazijua, watu walifanya vile ili nionekane sifai.
“Kwani yeye mkimuuliza anasemaje? Muulizeni yeye (Catty) alifanya nini
na kwa nini hadi mimi nikafukuzwa. Maana yeye alikuwa akisema anakula
na wakubwa na kwamba ananipa siku na kweli nikaondolewa kazini. “Maana
mimi najua yeye anajua kila kitu, alikuwa akishirikana na Mwenyekiti wa
Umoja wa Vijana (UVCCM) wa , Sabaya), walikuwa wanaelewana, muulizeni
yeye atawapa majibu.”
VIPI KUHUSU MISAADA MASHULENI?
Kuhusu
madai ya Cathy kuwa kuchomwa kwa shule hizo kulimzuia yeye kutoa
misaada, Ntibenda alisema Cathy hakuwa akitoa msaada wa aina yoyote.
“Cathy hakuwa akitoa msaada wowote. Mimi ndiye niliyekuwa nikitoa
misaada. Muulizeni vizuri (Cathy), yeye ndiye anajua,” alisema Ntibenda.
HUYU HAPA MWENYEKITI WA UVCCM
Lengai Ole Sabaya, Mwenyekiti wa UVCCM Arusha, alipatikana kupitia simu yake ya
mkononi
na baada ya kumsomea tuhuma zote dhidi yake zilizotolewa na kiongozi
wake huyo wa zamani, alifunguka: “Alifukuzwa kazi kwa sababu ya uzembe,
uzembe wa kwanza ni kushindwa kuwatambua watu waliokuwa wakichoma moto
mashule, kama anasema mimi na Cathy tunawajua, basi utakuwa ni uzembe
mwingine wa pili kwa sababu alishindwa kutukamata wakati anajua sisi
tunawajua. “Mwambie Ntibenda, tuna ushahidi wa mambo yake mengi
aliyokuwa akiyafanya ikiwa ni pamoja na kukihujumu chama, huyu alikuwa
akikutana na madiwani wa upinzani na kuweka nao mikakati, ndiyo maana
baada ya kutimuliwa, Chadema walikuwa wa kwanza kulalamika.”
KUHUSU MAPENZI
Katika
gazeti la Risasi Jumamosi iliyopita, Mbunge huyo wa Arusha kupitia viti
maalum, alitoa ufafanuzi wa madai ya watu kwamba alikuwa akitoka
kimapenzi na mkuu huyo wa mkoa, wakidai ndicho kilikuwa chanzo cha
tofauti zao za sasa. Hata hivyo, Cathy alikanusha madai hayo, sambamba
na Ntibenda mwenyewe aliyesema hajawahi kujihusisha na mrembo huyo, kwa
vile mumewe ni rafiki yake na anamchukulia Catty kama shemeji yake.
“Mimi sijawahi kuwa na uhusiano na Cathy, kwanza mumewe ni rafiki yangu
mimi, tuko vizuri.”
CATHY TENA
Juzi, Risasi
Jumatano lilimpigia tena simu Catty na kumpa majibu ya Ntibenda ambapo
aliishia kusema: “Mimi ndiyo najua mimi! Muulizeni vizuri.” (akatata
simu). Habari hii ilitoka kwa mara ya kwanza katika gazeti la Risasi
Jumamosi, wiki iliyopita ikiwa na kichwa cha habari; MBUNGE CATHY
AFUNGUKA MAZITO
0 comments:
Post a Comment