Dar
es Salaam. Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi namna benki ya NBC tawi
la Corporate ilivyopokea Sh 9,985,000 kutoka benki ya NMB tawi la
Msasani na kuziingiza katika akaunti ya mteja lakini ikazitoa siku
iliyofuata.
Kamanda
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliliambia
Mwananchi kuwa wanafuatilia jambo hilo kubaini mazingira hayo tata ya
mteja kuingiziwa fedha lakini siku ya pili akajulishwa kupitia ujumbe
mfupi wa simu kuwa zimetolewa.
“Jambo hilo lipo, lakini nawaombeni mnipe muda zaidi, kwani bado nipo kwenye uchunguzi,” alisema Kamanda Sirro.
Alipofuatwa
Meneja wa NBC tawi la Corporate, Mariam Kombo ili aeleze mkasa huo
alishauri mwandishi anayefuatilia sakata hilo awasiliane na Meneja
Uhusiano, William Kallaghe ambaye alisema hawawezi kutoa siri za mteja
wao kwa sababu maadili hayaruhusu.
Mteja
wa benki hiyo aliyekumbwa na sakata hilo ni Bertha Edward Gama ambaye
aliingiziwa Sh 9,985,000 katika akaunti yake iliyopo NBC tawi la
Corporate jijini Dar es Salaam lakini alipotaka kuzichukua aliambiwa
zimetolewa. Kwa mujibu wa Bertha fedha ziliingizwa Agosti 18 mwaka huu
na zilitolewa na watu wasiojulikana Agosti 19.
Hata
hivyo, benki hiyo imesema fedha hizo zinaendelea kutunzwa na benki hiyo
baada ya kubaini kuwa hundi iliyotumika kuingizia fedha katika akaunti
hiyo ilikuwa na dosari hivyo wao hawahusiki. Baada ya Bertha kufuatilia
hatima ya fedha hizo bila mafanikio alikwenda kuripoti polisi na tayari
Kamanda Sirro amesema wanafuatilia.
Mkasa ulivyokuwa
Bertha
ambaye ni Ofisa Masoko wa Ema Investment Company iliyopo Mtaa wa
Kitumbini katikati ya jiji aliliambia Mwananchi kuwa Agosti 17, akiwa
ofisini alipokea simu kutoka kwa mteja akitaka kununua bidhaa mbalimbali
kwenye kampuni yao.
Alisema
mteja huyo alijitambulisha kwa jina moja la Hemed, akidai kuwa yupo
mjini Morogoro na alitaka apatiwe katoni za pampers 15 na katoni 500 za
tambi vyote vikiwa na thamani ya Sh 9,985,000.
Ofisa
huyo alisema kuwa mteja wao huyo aliomba atumiwe namba ya akaunti ya
kampuni ili aweze kuweka fedha hizo na kwamba angependa zaidi akaunti
hiyo iwe ya benki ya NBC kwa sababu kampuni yake ina akaunti katika
benki hiyo.
Bertha
alisema walimtumia mteja huyo akaunti iliyoko Eco Bank, lakini alikataa
akisisitiza apewe ya NBC ili hela ziingie haraka na yeye apate mzigo
mapema. Alisema walimjibu kuwa ofisi haikuwa na akaunti NBC lakini ili
wasikose fedha hizo uongozi uliamua zipitie kwenye akaunti yake iliyopo
NBC tawi la Corporate.
Alisema
baada ya kumtumia akaunti hiyo, saa 11.45 Agosti 18, 2016 alipokea
ujumbe mfupi kutoka NBC ukisema amewekewa Sh 9,985,000 kwenye akaunti
yake.
Bertha
alisema baada ya kupata ujumbe huo baadaye kidogo alipigiwa simu na
mteja huyo akimweleza kuwa ameshaweka fedha hizo kwenye akaunti na
akasema atamtuma dereva kuchukua mzigo asubuhi ya siku iliyofuata.
Bertha
alisema kesho yake asubuhi dereva aliyetumwa kuchukua mzigo alifika
akachukua mzigo lakini saa 7.09 mchana alipokea ujumbe mwingine kutoka
NBC ukimtaarifu kuwa fedha zimetolewa.
Alisema
baada ya kupata ujumbe huu uongozi wa kampuni hiyo ulishtuka na kuamua
kwenda kufuatilia kulikoni na walipofika waliripoti jinsi walivyopata
taarifa ya kuingia fedha kwenye akaunti na baadaye kutolewa.
Kwa
mujibu wa Bertha, benki iliwapa majibu kwa maandishi kuwa fedha hizo
ziliingizwa kwenye akaunti yake kwa hundi kutoka benki ya NMB tawi la
Msasani jijini Dar es Salaam na zilitoka katika kampuni moja (jina
linahifadhiwa). Kwamba uamuzi wa NBC kuziondoa fedha hizo kwenye akaunti
ya Bertha ulitokana na tofauti ya saini kwenye hundi.
Barua
hiyo ya Agosti 19, 2016 ilisainiwa na Kombo ikieleza kuwa fedha hizo
zimehifadhiwa na benki kama sheria zinavyotaka. Bertha alipohoji kwa
nini fedha ziingie kwenye akaunti halafu ziondolewe, utaratibu wa hundi
ya benki moja kwenda benki nyingine ukoje aliambiwa aandike barua ya
malalamiko.
Baada
ya kuandika barua na kuikabidhi benki, uongozi wa benki hiyo uliwajibu
kwa barua Agosti 20, 2016 kuwa wanafanya uchunguzi na kwamba watatoa
jibu baada ya siku 10.
Barua
iliyosainiwa na Mkuu Huduma kwa Wateja, Ngwitika Mwakahesya inaeleza
kuwa walitoa fedha hizo baada kupata taarifa kutoka Benki ya NMB
ikiwaeleza kuwa hundi hiyo ilikuwa na dosari.
Benki ya NBC
Alipopigiwa
simu Meneja Uhusiano, William Kallaghe ili atoe ufafanuzi alisema:
“Suala hilo linahusu mteja wetu itakuwa si vema kutoa siri za mteja kwa
sababu maadili hayaruhusu na pili tumepata taarifa kwamba amepeleka
suala hilo polisi.”
Benki NMB. Alipofuatwa
kwa ufafanuzi, Maneja wa Tawi la Msasani Mary Ngallawa alisema
analifahamu suala hilo lakini hivi sasa limeshafikishwa polisi kwa hatua
zaidi. “Nakuomba uende polisi unaweza kupata ufafanuzi zaidi, mimi
siwezi kulizungumzia zaidi,” alisema Ngallawa.
Source:- Mwananchi Blog
0 comments:
Post a Comment