Rais John Magufuli
Dar
es Salaam. Rais John Magufuli ameahidi kuzikata fedha wizara zote
zinazodaiwa fedha na kampuni ya magazeti ya Uhuru Publications Ltd ili
aweze kulipa deni la Sh1.6 bilioni ambalo limelimbikizwa kwa muda mrefu.
Rais
Magufuli alitoa ahadi hiyo jana alipofanya ziara ya kushtukiza katika
ofisi ndogo za CCM zilizopo Mtaa wa Lumumba na baadaye katika kampuni ya
Uhuru inayochapisha magazeti ya Uhuru na Mzalendo ambako aliagiza
apelekewe orodha ya wizara zote zinazodaiwa na kampuni hiyo ili azikate
yeye mwenyewe.
Dk
Magufuli ambaye alifanya ziara kama mwenyekiti wa CCM, alitoa ahadi
hiyo baada ya kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi kwamba hawajalipwa
mishahara yao kwa kipindi cha miezi saba sasa tangu Februari mwaka huu
sababu ikiwa ni deni la Sh1.6 bilioni zilizoko mikononi mwa wizara.
Wafanyakazi
hao walimweleza Rais Magufuli kuwa wanaidai kampuni malimbikizo ya
mishahara ya miezi saba ambayo imefikia kiasi cha Sh 607 milioni hali
iliyowasababisha kufanya kazi katika mazingira magumu. Kaimu
Mhariri mtendaji wa kampuni hiyo, Ramadhani Mkoma alimweleza Rais
Magufuli kuwa sababu ya kushindwa kuwalipa wafanyakazi hao mishahara yao
inatokana na wizara kutolipa deni lililofikia kiasi cha Sh1.6 bilioni.
Ziara
Rais
Magufuli alifanya ziara hiyo ya kushtukiza katika ofisi za chama hicho
saa 3.30 asubuhi na akatia saini katika kitabu cha mahudhurio kisha
alikwenda ofisini kwake ambako alikutana na Katibu Mkuu wa chama hicho,
Abdulrahman Kinana na msemaji wa chama hicho, Christopher Ole Sendeka.
Hata
hivyo haikuweza kufahamika kilichozungumzwa kati yake na viongozi
wengine wa chama hicho. Alitoka ofisi kwake saa 6.28 mchana na akaenda
kukutana na wafanyakazi na waandishi katika chumba cha habari cha
magazeti ya Kampuni ya Uhuru.
Miongoni
mwa wafanyakazi walioelezea kwa kina hali ya kampuni, kero za mishahara
na kuuzwa kinyemela kwa mtambo ni Mkoma, mwandishi Selina Wilson na
Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi tawi la Uhuru, Moses Makambi.
Mahojiano
Mkoma:
Mheshimiwa Rais biashara ya magazeti imekuwa siyo nzuri kwa sababu
hatujalipwa madeni ya Sh1.6 bilioni tunazozidai wizara zote.
Rais Magufuli: Sasa naomba uniorodheshe wizara zote zinazodaiwa leo hii (jana) nizipate na mimi nitawakata mwenyewe.
Wilson: Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wafanyakazi wa kampuni ya Uhuru hatujalipwa mishahara yetu sasa ni mwezi wa saba.
Rais Magufuli: Kwa hiyo mnaishije kama hamlipwi mishahara?
Wilson: Tunaishi kwa kudra za Mwenyezi Mungu.
Makambi:
Mheshimwa Mwenyekiti tunaishi katika mazingira magumu. Tunashindwa hata
kusomesha watoto wetu katika shule nzuri kwa kukosa fedha, kwa kweli
tuna hali ngumu. Tulikuwa na mtambo (Mordern Newspaper Printers Limited)
wetu wa kuchapisha magazeti lakini umeuzwa kinyemela kama chuma chakavu
na sasa tunaenda kuchapisha magazeti yetu katika kampuni ya Jamana kwa
gharama ya Sh52 milioni kwa mwezi.
Rais Magufuli: Umeuzwa wapi? Na nani aliuza? Eti katibu mkuu unazo hizi taarifa?
Kinana: Mheshimiwa Rais, mtambo huu uliuzwa tangu mwaka 2011. Ulikuwa haufanyi kazi kwa kipindi cha miaka saba.
Rais Magufuli: Sasa huo mtambo ulikuwa hautengenezeki mpaka mkaamua kuuza kama chuma chakavu?
Mkoma:
Mheshimiwa Rais mtambo huo ulikuwa hautengenezeki kwa sababu ulikuwa
mbovu na ulikuwa unaiingizia hasara kampuni. Kutokana na hali hiyo bodi
ilikaa na kupendekeza mtambo huo ulionunuliwa kwa Sh200 milioni kutoka
Bulgaria uuzwe kama chuma chakavu kwa Sh 6milioni.
Rais Magufuli: Mwenyekiti wenu wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni hii ni nani?
Mkoma: Mheshimiwa Adam Kimbisa
Rais Magufuli: Anafahamu hili na mwenyekiti huyu wa bodi anateuliwa na nani?
Kinana: Mheshimiwa Rais anateuliwa na Kamati Kuu na pia Kamati Kuu ndiyo inatengua wadhifa wake.
Rais Magufuli: Basi nikikaa na Kamati Kuu nitaweza kuteua mwenyekiti.
Pia,
wafanyakazi hao waliichongea bodi hiyo kwa Rais Magufuli kuhusu
wafanyakazi watano waliosimamishwa kazi kwa muda wa miezi mitatu lakini
mpaka sasa wanaendelea kulipwa mishahara hivyo kuisababishia hasara
kampuni kiasi cha Sh40 milioni kutokana na kuendelea kulipwa kwa mwaka
sasa.
“Mwenyekiti
kuna wafanyakazi watano walisimamishwa kazi na bodi kwa muda wa miezi
mitatu, lakini mpaka sasa wamefikisha mwaka mmoja bado wanaendelea
kulipwa mshahara na kuisababishia hasara kampuni ya Sh40 milioni,”
alisema Rhoda Kangelo ambaye ni Ofisa Rasilimali Watu.
Wafanyakazi
hao walimwambia Rais Magufuli kuwa wanataka wapatiwe mkurugenzi mpya
ambaye ataendesha kampuni hiyo kwa faida tofauti na sasa ambapo kampuni
hiyo inajiendesha kwa hasara.
Walidai
kuwa mkurugenzi aliyekuwepo alisimamishwa kazi baada ya kumsimamisha
mmoja wa wafanyakazi wa kitengo cha matangazo aliyebainika kuwa aliibia
kampuni Sh 900,000.
“Mheshimiwa
Mwenyekiti, hapa tunaongea ukweli, lakini majina yetu tayari
yameandikwa kwa ajili ya kufukuzwa kazi baada ya kuongea hali halisi
ilivyo katika kampuni yetu,” alisema mmoja wa wafanyakazi huku wengine
wakishangilia na kupiga makofi.
Walidai
tatizo kubwa katika kampuni hiyo ni uongozi mbaya na hivyo walishauri
mwenyekiti aunde menejimenti mpya ambayo itafanya kazi vizuri.
Wafanyakazi hao walisema zaidi ya Sh800 milioni hazijapelekwa NSSF tangu
mwaka 2011 hadi sasa.
Maagizo manne
Baada
ya kusikiliza matatizo na changamoto zinazowakabili wafanyakazi wa
kampuni hiyo, Rais Magufuli alitoa maagizo ambayo ni kuhakikisha kuwa
wafanyakazi hao wanalipwa malimbikizo yote yao ya mshahara wanaodai.
“Nataka
malimbikizo ya mshahara wa hawa wafanyakazi yalipwe mwezi huu, watu
hawawezi kufanya kazi, wanajitolea halafu wasipewe mshahara wao,”
alisema Rais Magufuli.
Pili,
aliagiza apelekewe orodha ya wizara zinazodaiwa na yeye atalifanyia
kazi suala hilo ikiwemo kukata fedha zinazodaiwa wizara hizo ili
zikatumike kuboresha kampuni hiyo. “Nataka orodha hii ije leo… niipate
leo na iwe ya ukweli,” alisema Rais Magufuli.
Rais
Magufuli aliwataka wafanyakazi hao wamwachie yeye suala la utawala
kwani atakwenda kukutana na bodi ya wakurugenzi wa kampuni hiyo na huko
atatoa uamuzi.
“Mimi
ndio JPM, niachieni haya matatizo nitayafanyia kazi na mimi haya yote
matatizo nilikuwa nayajua hata kama msingeniambia najua,” alisema Rais
Magufuli.
Agiza la nne aliahidi kuwanunulia gari kwa ajili ya kurahisisha usafiri kwa waandishi wa habari na wafanyakazi wote kwa ujumla.
Nje ya ofisi Japokuwa
Rais alikuwa katika eneo hilo shughuli mbalimbali ziliendelea kufanyika
kama kawaida huku magari yakipita katika barabara ya Lumumba bila
kuzuiwa kama ilivyozoeleka kiongozi wa nchi anapopita.
Wakati anaondoka saa 7.10 mchana, nje ya ofisi za CCM na Uhuru wananchi walikuwa wamejipanga kandokando ya barabara wakimsubiri. Abdallah
Swaleh na Ester Lazaro waliliambia gazeti hili kuwa walifurahishwa na
hali iliyokuwepo kwani walidai kuwa hiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa rais
kufika kwenye ofisi hizo.
Source:- Mwananchi Blog
0 comments:
Post a Comment