TAARIFA
KWA UMMA
KANUSHO: PROFESA MUHONGO
KUCHANGISHA SHILINGI 40,000 KWA AJILI YA TETEMEKO KAGERA
Gazeti la Mwananchi
la tarehe 23 Septemba, 2016 katika ukurasa wake wa Tano imeandikwa habari yenye
kichwa cha habari “Harambee ya Profesa
Muhongo yakusanya Sh 40,000 Bukoba”.
Mwandishi wa Habari
hiyo ameandika kuwa ziara aliyoifanya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo katika Kata ya Hamugembe, Bukoba wakati akikagua miundombinu ya
umeme, iligeuka kuwa harambee baada ya waathirika wa tetemeko la ardhi kudai
msaada wa chakula na mahema.
Tunapenda kuuarifu
Umma wa Watanzania kuwa, siyo kweli kwamba Profesa Muhongo aliitisha harambee
ya kuchangia maafa hayo kama ilivyoandikwa na Mwandishi ambaye kwa sababu zake
binafsi aliamua kupindisha ukweli na kueleza kuwa, “ilimlazimu Profesa Muhongo
kuitisha mchango wa fedha kutoka kwa maofisa aliokuwa ameambatana nao na
kufanikiwa kupata shilingi 40,000 na kuwakabidhi wakazi hao”.
Ikumbukwe kuwa Waziri
wa Nishati na Madini alikuwa mkoani Kagera kukagua shughuli za kiutafiti
zinazofanywa na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) na Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM) baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi tarehe 10 Septemba, 2016
na kusababisha athari mbalimbali ikiwemo kwa miundombinu ya umeme.
Hivyo, taarifa kuwa Profesa
Muhongo aliitisha harambee ya kuchangisha fedha za kusaidia waathirika wa maafa
siyo sahihi kwani Profesa Muhongo hakuomba wala kuagiza Maofisa alioambatana
nao kuchangia fedha kama ambavyo mwandishi anataka kuwaaminisha wananchi.
Akiwa katika kata ya
Hamugembe mkoani humo ambapo alikwenda kukagua nyumba ambazo zimekatiwa huduma
ya umeme kwa sababu ya kuathiriwa na tetemeko hilo, baadhi ya wananchi walidai
kuwa shida yao ni chakula na malazi, na mmoja wa wananchi alisema kuwa Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kagera aliyeambatana
na Profesa Muhongo, alishafika kata hiyo na kuwasaidia kiasi cha fedha.
Hata hivyo, Profesa
Muhongo aliwaeleza wananchi hao kuwa, yeye alikwenda hapo kwa ajili ya kushughulikia
masuala ya kitaalam anayoyasimamia na kwamba kilio chao kuhusu kucheleweshewa
huduma atakifikisha kwenye Kamati inayoshughulikia Maafa aliyokutana nayo tarehe
22 Septemba, 2016.
Baada ya wananchi
kumtaja Meneja wa TANESCO wa Mkoa Kagera aliyewahi kuwasaidia wananchi hao fedha
kutokana na tetemeko hilo, Meneja huyo aliamua
kuongeza kiasi cha Fedha na kumpa mmoja wa wananchi hao, tofauti na
ilivyoandikwa kwenye gazeti kuwa Waziri wa Nishati na Madini ndiye aliyekabidhi
pesa kwa wananchi. Tunawaasa waandishi
wa habari kuzingatia ukweli na usahihi katika uandishi wa habari ili kupeleka
habari sahihi kwa wananchi.
Imetolewa
na;
WIZARA
YA NISHATI NA MADINI
23
SEPTEMBA, 2016
0 comments:
Post a Comment