Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Aron
Kagurumjuli amevunja Baraza la Madiwani rasmi baada ya serikali kuigawa
manispaa hiyo kuwa mbili. Kagurumjuli alilivunja baada ya
kumalizika kwa Baraza la Madiwani la kawaida.
Alipokuwa akitangaza kulivunja baraza hilo, Kagurumjuli alisema
amevunja baraza hilo kwa kuwa serikali imegawanya manispaa hiyo kuwa
wilaya mbili, ya Kinondoni na Ubungo hivyo kwa kuwa wilaya zote tayari
zina wakurugenzi, wakuu wa wilaya na makatibu tawala wa wilaya imempasa
kufanya hivyo. “Baraza la madiwani limevunjwa, kuvunjwa kwa baraza hili ni ukomo wa meya pia,” alisema.
Aliongeza kuwa wiki ijayo kutakuwa na uchaguzi wa meya katika manispaa hizo. Meya wa Manispaa ya Kinondoni alikuwepo kabla ya kuvunjwa kwa
baraza hilo ni Boniface Yakob ambaye amebaki nafasi yake ya udiwani. Kuvunjwa kwa baraza hilo kulikuwa kunatarajiwa baada ya serikali kugawanya manispaa ya Kinondoni kuwa mbili.

0 comments:
Post a Comment