Aliyekuwa mfanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Samson Magoti
akizungumza na waandishi wa Mwananchi nyumbani kwake Yombo Dovya jijini
Dar es Salaam jana. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dar es Salaam. Haikuwa
kazi rahisi. Miaka 22 ya wafanyakazi 31 wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT)
kutafuta haki yao iligubikwa na umaskini, maradhi na vuta nikuvute ya
migogoro ya kisheria.
Hatimaye
haki hiyo imepatikana Oktoba 2 mwaka huu baada ya Mahakama ya Rufani
kuwarejesha ikisema walifukuzwa kazi mwaka 1993 bila kufuata sheria.
Kiongozi
wa wafanyakazi hao, Samson Magoti aliyesimama kidete kuhakikisha
wanapata haki yao, amezungumza na Mwananchi na kueleza maisha magumu
aliyopitia katika kipindi hicho ikiwamo kuugua kiharusi kutokana na
mawazo na kukimbiwa na mke.
“Haikuwa
kazi rahisi, lakini hatimaye Mahakama imetenda haki na kama si majaji
wanaosimamia maadili ya kazi yao, leo pengine tusingepata haki yetu,”
alisema Magoti.
Mazungumzo
haya na Magoti yalifanyika nyumbani kwake, Yombo Dovya, wilayani Temeke
tulipomkuta yeye na familia yake ya watoto wanne kati ya sita, mke
(mwingine) na mama yake mzazi, ajuza wa miaka 102. Magoti, mrefu kiasi na mweusi, anakuja kutupokea akiwa ameambatana na watoto wake watatu, wadogo; Happy, Eliza na Witi.
Tulipofika
nyumbani kwake, alitukaribisha kwenye banda la uani ambalo baadaye
alitueleza kuwa lilikuwa likitumika kufugia kuku lakini kutokana na
ugumu wa maisha, sasa ndiyo makazi ya familia hiyo. Robo ya banda hilo imejengwa kwa matofali na robo tatu iliyosalia ni maboksi (ceiling board).
Tulipowasili
nyumbani kwake, mke wa sasa wa Magoti, Naomi Samson alikuwa akijiandaa
kwenda kuuza ufuta katika Shule ya Msingi Buguruni na alipotukaribisha,
tuliuliza bei ya ufuta naye alitujibu: “Huu ni Sh100, una Bluetooth,
Whatssap na Memory card.”
Baada ya kununua ufuta wa Sh500, tulianza mazungumzo yetu na Magoti ambaye alifukuzwa kazi Machi, 29, 1993.
“Nilikaa
na mke wangu wa kwanza katika kipindi cha mwanzo tu wakati nina hela za
mafao, baada ya hapo hali ilianza kubadilika naye akabadilika,”
alisema.
Alisema
miaka mitatu tu, baada ya kufukuzwa kazi, migogoro ilianza kwenye ndoa
yake, mkewe alibadilika naye akawa hana sauti ndani ya nyumba.
“Kama
huna kazi unakuwa mnyonge, huna sauti, kwa sababu kila unalomwambia
atakujibu atakavyo na atasingizia anatafuta hela na wewe kweli huna.”
Baada ya migogoro hiyo, mke wake aliondoka na kumuachia watoto watatu.
Source:- Mwananchi Blog.
0 comments:
Post a Comment