Aliyekuwa
Waziri wa Fedha, Basil Mramba na Waziri wa Nishati na Madini, Daniel
Yona katika Serikali ya Awamu ya Tatu,
leo wanahitimisha kifungo cha
miaka miwili, ambacho kilichoambatana na kifungo cha nje cha kufanya
usafi. Mramba na Yona wanamaliza kifungo hicho
leo baada ya kufanya usafi kwa saa nne kila siku kwenye hospitali ya
Palestina, Sinza, Dar es Salaam, kama walivyopangiwa na baada ya hapo
watakuwa huru uraiani.
Awali mawaziri hao wa zamani walitumikia
kifungo cha miaka miwili jela, lakini baadaye walibadilishiwa kifungo
hicho na kuwa cha nje, baada ya kuonesha utiifu gerezani kwa kufanya
kazi walizopangiwa kwa bidii. Baada ya tathmini ya utii wao
iliyofanywa na Jeshi la Magereza kukamilika, Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu ilibariki uamuzi huo wa kupewa adhabu ya kifungo cha nje.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo,
Cyprian Mkeha alisema sheria ya huduma kwa jamii namba sita kifungu
namba 3(1) ya mwaka 2002, inasema mtu anayetiwa hatiani kwa kosa ambalo
adhabu yake ni miaka mitatu kurudi chini, Mahakama inaweza kumpa adhabu
ya kutumikia jamii. Mramba na Yona baada ya rufaa walibaki
na adhabu ya miaka miwili, ambapo walitiwa hatiani kwa kutumia madaraka
vibaya na walipaswa kumaliza kifungo mwezi huu.
Hakimu Mkeha alisema Magereza
walifikisha barua mahakamani hapo Desemba 5, mwaka jana, wakipendekeza
kifungo cha nje kwa mawaziri hao. Kwa mujibu wa hukumu hiyo ya Mkeha,
baada ya kupokea barua hiyo Mahakama iliamuru watu wa huduma za jamii
kuchunguza kama wanastahili kupewa adhabu hiyo na baada ya uchunguzi
walirudisha ripoti kwamba wanastahili.
Hakimu Mkeha alisema vigezo vya kupewa
adhabu hiyo ni umri mkubwa ambapo Mramba na Yona wana umri wa miaka 75
na kama wahusika ni wakosaji wa mara ya kwanza. Kigezo kingine ni kama watuhumiwa
walijutia kosa lao na kukubali kuitumikia jamii bila kulipwa, kuangalia
umbali wanakoishi na eneo wanalokwenda kufanyia shughuli za kijamii na
tabia za washitakiwa.
Hakimu Mkeha alisema sheria
haijapendekeza makosa yapi wasipewe kifungo cha nje, isipokuwa imetamka
kwa yeyote aliyefungwa kuanzia miaka mitatu kushuka chini. “Mramba na Yona baada ya kuridhika
kwamba wanashitakiwa, wamepangiwa kufanya usafi hospitali ya Palestina
Sinza kila siku na watatumikia hadi Novemba 5. Watakuwa wanafanya kazi
kwa saa nne,” alisema Hakimu Mkeha.
Julai 6, mwaka jana Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu iliwahukumu kwenda jela miaka mitatu na kulipa faini ya Sh
milioni tano, huku ikimwacha huru aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha, Gray Mgonja baada ya kumwona hana hatia.
Walikuwa wanakabiliwa na mashitaka ya
matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh
bilioni 11.7 kwa kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni ya kukagua madini ya
dhahabu ya M/S Alex Stewart ya Uingereza.
Hukumu hiyo ilitolewa na jopo la majaji watatu, Saul Kinemela, Sam Rumanyika na John Utamwa, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jopo hilo.
Kwa mara ya kwanza washitakiwa hao
walifikishwa mahakamani hapo mwaka 2008. Hata hivyo, Oktoba 2, mwaka
jana walipinga adhabu hiyo na kukata rufaa.
Katika rufaa waliyokata Mahakama Kuu
Kanda ya Dar es Salaam mbele ya Jaji Projest Rugazia, walipunguziwa
adhabu kwenye kuisababishia Serikali hasara, hivyo wakabaki na adhabu ya
kifungo cha miaka miwili jela kwa kutumia madaraka vibaya.
Source:- SwahiliTimes
0 comments:
Post a Comment