ASKARI wa jeshi la Polisi mwenye cheo cha Koplo
Evarist Furaha wa Kibaha Mkoa amefariki Dunia mara baaada ya kujifyetulia
risasi kwa bahati mbaya akiwa kazini.
Kaimu Kamanda wa
Polisi mkoani Pwani, Blasius Chatanda ameyasema hayo jana kwa waandishi wa
habari alipokuwa akitolea ufafanuzi tukio hilo.
Chatanda amesema ajali hiyo ilitokea Novemba
28, mwaka huu saa moja usiku, Maili Moja eneo la Sokoni, Kata ya Maili Mmoja.
“Askari huyo alijipiga risasi kwa bahati mbaya
ambapo alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya
Tumbi,” amesema Chatanda.
Amesema, Furaha aliingia kazini jioni katika
Kituo cha Polisi Wilaya ya Kibaha na alikuwa amepangiwa lindo kwa Mkuu wa
Wilaya ya Kibaha.
“Alikutwa na mauti baada ya kujipiga risasi kwa
bunduki aina ya SMG akiwa anakwenda kwenye lindo alilopangiwa,” amesema na
kuongeza kuwa alikuwa anaenda lindoni akiwa amekaa mbele ya gari PT1732
lililokuwa likiendeshwa na Koplo Grayson, ndipo wakati anashuka bunduki
ilijifyatua na kumpiga kifuani upande wa kushoto.
0 comments:
Post a Comment