Aliyekuwa
Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi
(SACP) EX Peter Kakamba amefariki dunia alfajiri ya tarehe 30/11/2016 katika
hospital ya taifa Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu.
Kakamba
alizaliwa mwaka 1963 katika kijiji cha Kawajense Wilayani Mpanda, mkoa wa
Katavi. Alisoma shule ya msingi Shanwe Kawajense mwaka 1973 hadi
1980, Kidato cha kwanza hadi cha nne katika shule ya Sekondari Kantalamba mwaka
1981 hadi 1984 ambapo kidato cha tano na sita alisoma katika shule ya Sekondari
Umbwe mkoani Kilimanjaro mwaka 1985 hadi 1987. Mwaka 1992 hadi 1994 alisoma
Astashahada ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Marehemu
alijiunga na Jeshi la Polisi mwaka 1988 ambapo katika utumishi wake
alipandishwa vyeo mbalimbali ikiwemo Konstable wa Polisi (1989), Sagenti wa
Polisi (1991), Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (1997), Mkaguzi wa Polisi (2003),
Mrakibu Msaidizi wa Polisi (2006), Mrakibu wa Polisi (2008), Mrakibu Mwandamizi
wa Polisi (2011), Kamishna Msaidizi wa Polisi (2015) na Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Polisi (2016).
Baadhi ya
nafasi alizowahi kushika ni pamoja na kuwa Mwendesha Mashtaka wa
Polisi katika mkoa wa Iringa, Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mufindi, Afisa
mnadhimu wa Polisi katika Mikoa ya Iringa na Geita, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Iringa na mpaka anafariki alikuwa Kamanda wa Polisi katika mkoa wa Singida.
Kufuatia
kifo hicho Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Ernest Mangu anatoa pole kwa
Maofisa, Wakaguzi,Askari, ndugu, jamaa na marafiki kwa Msiba huo.
0 comments:
Post a Comment