NAVY
Kenzo ni mojawapo ya makundi yanayofanya vizuri hivi sasa katika sanaa
ya Muziki wa Kizazi Kipya, likiwa linaundwa na wasanii wapenzi, Aika
Mariale na Emannuel Mkono maarufu kama Nahreel, ambao wanatamba na kibao
chao cha Kamatia Chini.Kwa pamoja wanamiliki studio yao, The Industry na juzikati walizungumza na Risasi Vibes.
Risasi Vibes: Mashabiki wangependa kujua safari yenu ilianzia wapi?
Navy Kenzo: Tulikutana
India mwaka 2008, kila mmoja alikuwa shule kivyake, tulikutana katika ule mkutano wa wanafunzi Watanzania.
Risasi Vibes: Uhusiano ukaanzia hapo?
Navy Kenzo: Hapana,
ila pale tulijuana vizuri ni wapi mtu anaweza kumpata mwenzake na mara
nyingi tulikuwa tukitembeleana katika hosteli zetu tunazokaa.
Tunapokutana ilikuwa lazima ukute mmoja anasikiliza nyimbo kwenye simu
mwingine anaimba.
Kuna
siku tukaambizana mbona kama wote tunaweza muziki, kwa sababu Nahreel
alikuwa prodyuza toka shule na mimi Aika, naimba, tukapanga tukirejea
nyumbani tufanye kitu.
Risasi Vibes: Kwani huko shule mlienda kusomea muziki?
Navy Kenzo: Hapana, kila mmoja alikuwa anasomea kitu chake, Nahreel alisomea Computer Science na mimi Bachelor of Business Admnistration.
Tulivyorudi
mimi nikaenda kwetu Arusha, yeye akabaki Dar, nilienda kufanya kazi
katika kampuni ya baba yangu, nikamshauri aje Arusha sababu kule
wanamuziki wengi.
Risasi Vibes: Kwa hiyo ndiyo mkaanzia huko huko kutengeneza kundi lenu?
Navy Kenzo: Hapana kwa sababu baadaye mwenzangu alijiunga na Pah One, kwa hiyo hata mimi nilikuwa kama tu kukitokea kitu naimba nao.
Risasi: Ikawaje sasa mkaingia kwenye uhusiano rasmi na kukaa pamoja?
Navy Kenzo: Baadaye nilikuja Dar, nikaungana na Nahreel ambapo hapo sasa ndiyo tulipoanza msoto wetu.
Risasi Vibes: Kivipi?
Navy Kenzo: Nilipokuja
Dar, tukaanza kutafuta nyumba kila tukigusa ni bei kubwa sana na sisi
hela hiyo hatukuwa nayo, mwisho ikabidi tupate chumba maeneo ya
Mikocheni.
Risasi Vibes: Hapo ndipo mlipokuwa na studio?
Navy Kenzo: Ndiyo,
maana sebule ndiyo ilikuwa studio na huwezi amini, ndani tuna godoro,
tena dogo sana, wakati mwingine tunajikuta tumelala sakafuni.
Risasi Vibes: Sasa hela zenu mlikuwa mnazipataje?
Navy Kenzo: Yaani
we acha tu, kuna kipindi tulikosa hela kabisa hadi tukawa tunashinda na
njaa, nakumbuka kulikuwa na duka la Mangi karibia na kwetu, tukawa
tunakopa tukipata hela tunalipa.
Risasi Vibes: Kwa hiyo mlishawahi kushinda na njaa kabisa?
Navy Kenzo: Tena siyo mara moja, hapa mimi na yeye wote tunaumwa vidonda vya tumbo kwa sababu ya kushinda njaa.
Risasi Vibes: Lakini familia zenu zinajiweza, ilikuaje sasa?
Navy Kenzo:
Ni kweli wote tumetokea katika familia nzuri, lakini kuna kitu
tulijifunza kutoka kwa wazazi wetu kuwa lazima ujifunze kutafuta ili
uweze kuishi vizuri na ndicho tunachofanya kwa sababu tulilelewa maisha
mazuri na sisi tunataka watoto wetu pia waje kuishi vizuri.
Risasi Vibes: Kuna tetesi kuwa familia zenu hazikubariki uhusiano wenu ni kweli?
Navy Kenzo: Mara nyingi inatokeaga hivyo, lakini mwisho wa siku wanakubali wakiona msimamo wetu!
Risasi Vibes: Mlipataje studio kubwa mlipokuwa mkiishi?
Navy Kenzo: Yaani
ni Mungu tu na juhudi zetu kwa sababu tulivyoanza kutoa nyimbo na
kupendwa tuliweza kupata michongo mbalimbali ndiyo tukaweza sasa
kutengeneza studio ya kisasa.
Risasi Vibes: Kuna tetesi kuwa mmenunua kiwanja hapo mlipopanga, je zina ukweli?
Navy Kenzo: Unajua
kipindi tunapanga pale Mikocheni, pembeni yetu tukawa tunaona kiwanja
kiko wazi tukawa hatuelewi cha nani lakini huwezi amini mimi na mwezangu
tukasema ipo siku kitakuwa chetu na Mungu ni mwema siku tukakutana na
mwenye kiwanja tukazungumza naye na tukaanza kukilipia kidogokidogo.
Risasi: Kwa hiyo mpaka sasa ni sehemu yenu wenyewe?
Navy Kenzo: Ndiyo, tunamshukuru Mungu kwa hilo.
Risasi: Kwa kuwa mmetoka mbali, vipi kuhusu mpango wa kufunga ndoa?
Navy Kenzo: Hiyo ipo tu wala haikwepeki, tunaweka mambo vizuri.
0 comments:
Post a Comment