Wednesday, January 4, 2017

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuhakikisha eneo la Kisarawe II linakuwa na umeme wa uhakika ili kuwezesha viwanda na wananchi wa eneo hilo kupata nishati hiyo.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo wakati alipotembelea kiwanda cha Milkcom kinachozalisha bidhaa za maziwa na kiwanda cha Watercom kinachozalisha maji vilivyoko katika kata ya Kisarawe II wilayani Kigamboni akiwa katika ziara yake ya kikazi.
“Waziri wa Nishati ahakikishe eneo hili linapata umeme wa uhakika ili kuviwezesha viwanda hivi kufanyakazi vizuri jambo litakaloongeza uzalishaji. Pia wananchi wanaoishi katika maeneo haya nao watanufaika na upatikanaji wa nishati hiyo,” alisema.
Awali, Msemaji wa Viwanda hivyo, Aboubakar Faraj akisoma taarifa ya viwanda hivyo kwa Waziri Mkuu alisema moja ya changamoto zinazowakabili ni pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika jambo linasababisha kupanda kwa gharama za uzalishaji.
Aliongeza kuwa kwa sasa viwanda hivyo vimeajiri watu zaidi ya 1,800, ambapo alisema endapo Serikali itawahakikishia upatikanaji wa umeme na barabara wataongeza ajira kwa asilimia 25 ifikapo mwaka 2018.
Mapema Waziri Mkuu alizindua wodi ya wazazi katika Zahanati ya Kisarawe II iliyojengwa kwa ufadhili wa kampuni ya mafuta ya Oilcom. Wodi hiyo yenye vyumba vitatu itawapunguzia akinamama kusafiri umbali mrefu kutuata huduma hiyo.

0 comments:

Post a Comment