Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amemuagiza Mwakilishi wa Mchumi wa Manispaa ya Kinondoni, Febronia Luyageza kuiandikia barua Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ya kuomba kibali cha kubadilisha matumizi ya fedha za mradi wa ujenzi wa soko la Mkunguni zaidi ya milioni 130 kutokana na soko hilo kuwa na mgogoro kwa muda mrefu kati ya Halmashauri, chama cha ushirika na baadhi ya wananchi wenye viwanja. Ili fedha hizo zitumike katika ujenzi wa soko la Maandazi ambalo halina mgogoro.
Hapi ametoa maagizo hayo leo katika ziara yake kwenye Kata ya Hananasifu baada ya Afisa Mtendaji wa kata hiyo, Salum Mzaganya kuomba kibali cha fedha hizo kutumika baada ya kutotumika zaidi ya miaka mitatu kutokana na mgogoro uliopo.
“Naagiza manispa muombe kibali TAMISEMI cha kubadilisha matumizi ya fedha hizo, ili mzihamishe na kuzipeleka katika soko la maandazi lisilo na mgogoro,” amesema.
Kuhusu mgogoro wa soko la Mkunguni, Hapi amemuagiza Afisa Masoko wa Manispaa ya Kinondoni kuunda kamati itakayokutanisha chama cha ushirika, manispaa na wananchi wanaomiliki viwanja katika soko hilo ili kutafuta muafaka wa mgogoro huo.
“Undeni kamati kati ya watu wa manispaa, ushirika na wenye viwanja ili mpate muafaka, lakini nashauri ushirika mkubali kugawana asilimia na serikali. Hapo mtaweza kupata fedha za serikali kwa ajili ya ukarabati wa soko,” amesema.
Aidha, amewataka watendaji wa manispaa kupanga miradi katika maeneo yasiyo na mgogoro, na kuwataka kubadilisha matumizi ya fedha za miradi itakayobainika kuwa na migogoro ili fedha hizo ziende katika miradi mingine ya maendeleo isiyo na migogoro.
“Lakini tabia hii ya kuandika barua ya kuomba fedha za miradi katika maeneo yenye migogoro,” amesema.
0 comments:
Post a Comment