Thursday, March 2, 2017

Manispaa ya Kinondoni imetakiwa kuweka utaratibu mzuri kuhusu fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya mikopo kwa wajasiriamali wanawake, na vijana ili kujikomboa kiuchumi .
Taarifa hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Ally Hapi ambapo amesema kuwa Serikali inatenga bajeti ya asilimia 10 % kwa lengo la kutoa mikopo bila riba ambapo asilimia 5% ni kwa vijana na asilimia 5% kwa wanawake .Hapi amesema kuwa fedha zinazotengwa zinapitia katika benki ambapo wananchi huwekewa riba na masharti magumu jambo ambalo siyo kusudio la Serikali ya awamu ya tano.
“Serikali imedhamiria kusaidia wananchi wa hali ya chini hivyo naiagiza halmashauri iandae utaratibu mzuri utakao wawezesha vijana na wanawake kupata fedha ili kujikomboa kiuchumi bila yakulipia riba,” amesema Hapi

Amesisitiza kuwa manispaa iunde chombo maalum kwa ajili ya kukusanya fedha hizo zitakazokuwa zinakopeshwa kwa wajasiliamali hao.

“Utaratibu unaotumika hauko wazi na una urasimu ndani yake ambapo hata mkurugenzi wangu hakuwa wazi kunipatia taarifa hizo kutokana na benki kusuasua,” amesema

Sambamba na hayo, Hapi alitembelea shule ya Msingi Mbezi juu na Sekondari Mbezi Juu ambapo katika shule ya sekondari ametaka Ujenzi wa madarasa unaoendelea uzingatie ubora wa thamani ya fedha inayotolewa .

“Ni bora mtumie mafundi wa kawaida wenye uwezo ambapo mtapunguza gharama lakini wajenge kwa kuzingatia ubora unaotakiwa kuliko kutumia wakandarasi wakubwa ambapo fedha nyingi zinatumika,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni anaendelea na ziara ya kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi kuhusu kero mbalimbali wanazokabiliana nazo pamoja na kutoa maagizo ya Serikali, kwa watendaji na wananchi ili waongeze ufanisi katika kutatua kero za wananchi.

0 comments:

Post a Comment