Wednesday, March 29, 2017

Image may contain: 4 people, people smiling, guitar
*LEO MACHI 29 NI KUMBUKUMBU YA KIFO CHA TX MOSHI WILLIAM*
Marehemu TX Moshi William alifariki tarehe 29 Machi mwaka 2006 siku ya JUMATANO majira ya saa 3 asubuhi na kuzikwa siku hiyo hiyo katika makaburi ya Keko machungwa.

Tarehe na siku ya kifo chake vimejirudia mwaka huu na siku hiyo huwa kuna burudani ya Msondo katika ukumbi wa Sugar Ray kwa Sokota. Marehemu TX Moshi William alijiunga na Msondo mwaka 1982 akitokea Polisi Jazz. Miongoni mwa nyimbo alizotunga mara baada ya kujiunga ni pamoja na Ajuza, Asha Mwanaseif, (aliomtungia mkewe), na Ashibaye.
Alitunga nyimbo nyingi lakini nyimbo zilizotia fora sana ni pamoja na Kilio cha Mtu Mzima, Ndoa Ndoano, Piga Ua Talaka Utatoa, Ndoa ya Isihaka Kibene, Kaza Moyo na Ajali.
Wimbo wa Ajali aliutunga baada ya kupata ajali ya kuparamia mti wa mvinje pale Mivinjeni Desemba 16, 2005 iliyompelekea kuvunjika mguu.
Moshi William alikua chakaramu na mbunifu wa kutunga vionjo ikiwemo mtindo ujulikanao kama Mambo Hadharani na katika nyimbo alipenda kuchombeza vionjo vyenye kutoa raha na kunogesha wimbo mfano utasikia "we nani", " kidogo tu..kidogo tu", "kwanini lakini", " watoto wanachezea umeme", "dispilin", " fair play" nk
Wakati wa uhai wake TX Moshi William alipitia katika bendi mbalimbali za muziki wa dansi ambazo ni pamoja na Safari Trippers, Juwata Jazz. UDA Jazz, na Polisi Jazz bendi ambayo alitokea wakati anajiunga msondo.
Tx Moshi William alijaliwa kupata tuzo mbalimbali mfululizo za muziki kama Kilimanjaro Music Award.
Marehemu Moshi alibatizwa jina la TX, na mtangazaji mashuhuri na wa siku nyingi aliyekuwa mtangazaji wa Radio Tanzania, marehemu Julius Nyaisanga Uncle J. Nyaisanga alimbatiza jina hilo kutokana na tunzi zake za uhakika. Nyaisanga alikua mtangazaji wa RTD na kisha vituo vya utangazaji vya ITV Radio one. Jina halisi la TX ni Shaaban Mhoja Kishiwa ingawa alikuwa akijulikana zaidi kwa jina la Moshi William TX.
Alizaliwa mwaka 1958 Korogwe mkoani Tanga.
Kwa kweli Tx Moshi William ameacha pengo na kumbukumbu isiyosahaulika kwa wapenzi wa Msondo na ulimwengu wa muziki wa Dansi Tanzania. Tarehe 29 wana Msondo ngoma na wapenda muziki wa dansi tumkumbuke TX Moshi William.

0 comments:

Post a Comment