Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Samia Suluhu Hassan ameuagiza uongozi wa mkoa wa Dodoma uhakikishe unaondoa vitendo vya ukiritimba kwa baadhi ya watendaji wa serikali ambavyo vinaweza kusababisha ucheleweshaji au kukwamisha ujenzi wa miji mipya mikubwa mitano ya kisasa katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Dodoma.
Mhe
Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo 14-Mar-2017 wakati
akifanya mazungumzo na viongozi wa mkoa wa Dodoma baada ya kupokea taarifa ya
Kikosi Kazi kilichoundwa na serikali kwa ajili ya kuratibu shughuli mbalimbali
za Serikali kuhamia Dodoma.
Amesema ni muda muafaka sasa hivi kwa uongozi wa mkoa wa
Dodoma kujiimarisha na kujipanga ipasavyo katika kupokea wawekezaji wenye nia
njema ya kuwekeza kwenye sekta mbalimbali mkoani humo hasa wakati huu ambao
serikali inahamia Dodoma.
Ameonya kuwa
wawekezaji matapeli kamwe wasipewe nafasi ya kuwekeza Dodoma na ametaka uongozi
wa mkoa wa Dodoma kuwa makini makundi hayo ili wasije kuvuruga mipango ya
serikali ya kujenga Makao makuu ya kisasa katika Manispaa ya Dodoma.
Makamu wa Rais pia
ameuagiza uongozi wa mkoa wa Dodoma kulinda na kuendeleza maeneo yote yenye
uoto wa asili ili yasije yakaharibiwa kutokana na uwekezaji utakaofanyika mkoani
humo.
Amesema
amefurahishwa na kasi ya uongozi wa mkoa wa Dodoma jinsi unavyojipanga katika
kuhakikisha azma ya serikali ya kuhamia Dodoma inafanikiwa kwa haraka ikiwemo
utengaji wa maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda na huduma za kijamii.
Kuhusu maeneo ya
wafanyabiashara wadogo, Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu
Hassan amewataka viongozi wa mkoa wa Dodoma wahakikishe wanatenga haraka maeneo
maaluma kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo ili nao waweza kunufaika na mpango
wa Serikali kuhamia mkoani Dodoma.
“Ni muhimu maeneo
yote yatakayotengwa kwa ajili wafanyabiashara wadogo yawe huduma zote za
msingi ili kusaidia wafanyabiashara hao waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi“Amesisitiza Makamu wa Rais.
Makamu wa Rais Mhe
Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa ni muhimu kwa uongozi wa mkoa wa Dodoma
kuwashirikisha viongozi wa wafanyabishara wadogo kuhusu maeneo yatakayotengwa
ili kuondoa malalamiko kutoka kwa wafanyabishara hao kupewa maeneo yasiyofaa wa
ajili ya shughuli zao.
Awali kabla ya
kumkaribisha Makamu wa Rais kuzungumza na viongozi wa mkoa wa Dodoma, Mkuu wa
Dodoma Jordan Rugimbana alimweleza Makamu wa Rais mipango na mikakati ya mkoa
huo kuhusu azma ya serikali ya kuhamia Dodoma ikiwemo uimarisha wa huduma za
msingi ikiwemo afya, miundombinu, maji na elimu.
Mkuu huyo wa mkoa
wa Dodoma Jordan Rugimbana amesema mpaka sasa kazi ya kuainisha maeneo
mbalimbali kwa ajili ya uwekezaji, makazi na mahali ambapo ofisi za serikali na
za mabalozi zitajengwa umeshakamilika.
Amesema uongozi wa
mkoa wa Dodoma utaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za serikali,
mashirika ya kimataifa na mabalozi ili kuhakikisha maeneo yaliyotengwa
yanaendelezwa haraka.
Ameeleza kuwa
ujenzi wa miji Mitano mikubwa mkoani Dodoma na ujio wa wawekezaji mbalimbali
utaufanya mkoa huo kuwa na uhitaji nishati ya umeme ya uhakika hivyo amehimiza
ujenzi wa bomba la gesi asili kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma ukafanyika
haraka.




0 comments:
Post a Comment