Friday, March 17, 2017

Mwendesha baiskeli Josh Edmondson amesema alikuwa akivunja sharia za mchezo huo kwa kujichoma kisirisiri sindano ambazo zilikuwa zikijumuisha muunganiko wa vitamin mbali mbali.
 
Josh, 24, alikuwa akiitumikia timu ya Sky mwaka 2013 na 2014, na sasa anakabiliwa na matatizo kutokana na matumizi makubwa ya dawa za kutuliza maumivu.

Katika mahojiano na Shirika la Utangazaji nchini Uingereza BBC, Josh amesema mashindano ya mwaka 2014 yalimfanya akiuke vifungu kadhaa vya UCI kwa mara mbili au tatu ndani ya kila mwezi mmoja.

Mara baada ya Josh kuifichua siri hiyo, timu ya Sky imesema dawa za kuongeza vitamin zilikutwa katika chumba cha Josh, lakini hawakuripoti tatizo hilo kwani walihofia kwamba lingekuzwa.

Wakati timu ya Sky ikijitetea kwa hilo, Josh amesema alikiri kutumia dawa hizo na kuueleza uongozi, lakini uongozi wa timu hiyo ulifanya kila linalowezekana ili kuyaficha maovu ambayo yalikuwa yakitendeka.

Dawa hizo zilionekana pia na wachezaji wengine toka katika timu ya Sky ambao walikuwa wakiishi nae nyumba moja na pia walipiga picha dawa hizo kama sehemu ya ushahidi.
Mara baada ya kubainika kwamba wachezaji wenzake wameziona dawa hizo, Josh aliwasiliana na daktari wa timu kwa njia ya Skype ili kuliripoti tatizo hilo.

Katika mahojiano hayo Josh alieleza mambo mengine kadha wa kadha ikiwemo:
  • Kwenda nchini Italy katika mazoezi ili apate nafasi ya kununua dawa mbalimbali kwaajili ya kuongeza vitamin, dawa ambazo zinaruhusiwa kwa matumizi ya binadamu lakini haziruhusiwi kutumika miongoni mwa wanamichezo.

  • Amejihatarishia maisha yake kwa kujisababishia mshtuko wa moyo kwa kujidunga dawa za kuongeza vitamin bila ushauri wa matabibu.

  • Alijipa mamlaka ya kununua dawa za kuongeza nguvu mwaka 2013 katika ziara ya Uingereza. Hata hivyo timu ya Sky imejitetea kwa kusema kwamba daktari wa timu ndie aliempatia dawa hizo bila uongozi kujua.

  • Hakuweza kutoka katika nyumba yake kwa miezi miwili kutokana na athari za dawa ambazo alikuwa akizitumia kwa wingi.

Katika hatua nyingine Josh amesema alikuwa chini ya msukumo mkubwa mwaka 2014 sio tu kutoka katika timu anayoitumikia, bali hata ndani ya nafsi yake.

Josh amesema alikuwa hataki kuiangusha timu yake wala mashabiki wake hivyo ilimlazimu kutumia dawa hizo ili aweze pia kuongezwa mkataba.

Sakata la Josh limezidi kuiweka pabaya timu ya Sky kwani mwaka uliopita mwendesha baiskeli Jonathan Tiernan-Locke alieleza BBC kwamba alikuwa akipewa dawa za kuongeza nguvu ambazo zimekatazwa michezoni mwaka 2012 katika mashindano ya kombe la dunia.

Baadae alifungiwa kutojihusisha na mchezo wa baiskeli kwa miaka miwili mara baada ya kubainika kwamba aalikuwa akitumia dawa zilizokatazwa michezoni hali iliyompelekea kuamua kujiuzulu.

0 comments:

Post a Comment