Posted by Williammalecela.com on Wednesday, April 05, 2017
 |
KISA cha binti mwenye umri wa miaka 16 (jina linahifadhiwa kutokana na
miaka yake) kujitupa baharini akiwa katika boti ya Kilimanjaro V akitoka
Dar es Salaam kwenda Zanzibar juzi, kinaanzia kwenye mawasiliano yake
na mvulana mmoja, kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook, imefahamika.
Msichana huyo alikuwa akiwasiliana na mvulana huyo ambaye walifahamiana kupitia Facebook, kwa kutumia simu ya mkononi.
Nipashe ilifika Kikwajuni, nyumbani kwa msichana huyo ambaye ni
mwanafunzi wa kidato cha tatu (shule inahifadhiwa) na kuikuta familia
yake ikiwa na majonzi, huku wakiwa hawaamini kilichotokea na binti huyo
akiwa bado hai.
Akizungumza kwa huzuni, mama mdogo wa msichana huyo, Asha Saleh
Mandhi, alisema palitokea mzozo baina yake na binti huyo baada ya
kumkuta na simu ya mkononi wakati wazazi wake hawajamnunulia.
Alisema Jumatano iliyopita majira ya jioni akiwa nyumbani hapo na
baada ya kupata taarifa kuwa mtoto wake wa kumlea anamiliki simu,
alimwita na kumtaka aeleze amepewa na nani la sivyo atampeleka polisi
akajieleze.
Alisema siku ya pili yake asubuhi, msichana huyo alitoroka nyumbani
na ndipo alipotoa taarifa kituo cha polisi Madema kuwa amepotelewa na
mtoto.
“Mimi ndiye ninayemlea huyu mtoto. Kwa kweli sijui amefikwa na
mtihani gani kwa sababu hatujampa simu, lakini nashangaa tumemkuta na
simu na hakutaka kumtaja aliyempa,” Asha alisema.
“Kitendo cha kumuuliza ndicho kilichomfanya kukimbia na kwenda kusikojulikana.”
Mama mdogo huyo alisema baada ya kuwa ametoroka, aliichukua simu hiyo
na kuangalia mawasiliano yake na ndipo alipofanikiwa kupata jina la
kijana mmoja wa kiume ambaye alikuwa anawasiliana naye mara kwa mara.
Hakumtaja.
Alisema baada ya kumpata kijana huyo kwa njia ya simu, aliulizwa
anamfahamu vipi binti yao na kujibu kuwa wamejuana kupitia Fecbook,
lakini hawajawahi kuonana kwa sababu yeye anaishi Dar es Salaam na binti
anaishi Zanzibar.
Alisema alimpa taarifa kijana huyo kuwa binti yao ametoroka na
haijulikani alikokwenda, hivyo kumwomba kusaidiana kuhakikisha wanampata
akiwa salama.
“Kwa kweli huyo kijana alikubali kutoa ushirikiano na akawa
anawasiliana na binti yetu na kumueleza kuwa yuko Dar es Salaam na
amehifadhiwa na dereva teksi baada ya kukosa msaada wa eneo analotaka
kwenda ambako ni kwa bibi yake anayeishi Mburahati, Dar es Salaam,”
alisema.
Alisema aliwasiliana na dereva huyo ambaye alimueleza kuwa
amesharipoti katika serikali ya mtaa katika eneo analoishi kuwa
amemwokota binti huyo bandarini, Dar es Salaam baada ya kukaa kwa muda
mrefu bila kupata msaada.
Mama mdogo huyo alisema mama mzazi wa binti huyo anaishi Muscat, Oman na kwamba amemlea tangu akiwa mdogo.
Alisema walipata mshtuko baada ya kupata taarifa kuwa binti yao
amejitupa baharini wakati akitokea Dar es Salaam baada ya kusakwa kwa
siku kadhaa na hatimaye kupatikana.
MFANYAKAZI WA NDANI
Mmoja wa mashuhuda na mfanyakazi wa ndani katika nyumba anayoishi
manusura huyo alisema wakati akiwa katika boti wakitokea Dar es Salaam
juzi, walipata taarifa kuwa kuna mtu amejitupa baada ya kufika Chumbe,
lakini hakujua kuwa aliyejitupa anamfamu.
“Baada ya kupata taarifa kuwa kuna mtu kajitupa baharini, tukaanza
kupiga kelele na nilimwona akielea baharini, lakini nilijua ni mtoto wa
kizungu bila kufahamu kuwa nilikuwa namfahamu,” alisema Hiyari Miraji
Othman.
Alisema alikuja kufahamu kuwa anamfahamu manusura baada ya saa nne na kwamba hakutegemea angeweza kufanya kitendo hicho.
Alimwelezea msichana huyo kuwa ni mpole na mwenye nidhamu kwa kuwa
amekuwa akimuona hivyo nyumbani kwao Kikwajuni kwa muda mrefu.
“Hapa kwao nakuja kila siku kwa sababu ndipo penye kibarua changu,” alisema.
“Hapa huwa tunapika vyakula kwa ajili ya biashara na huwa namwona tabia zake ni mtoto mzuri anayejielewa.”
Credit – Nipashe |
0 comments:
Post a Comment