Serikali, imesema watumishi wa umma walioorodheshwa kwenye orodha
ya watumishi wa umma wenye vyeti feki, wakati hawakutakiwa kuwekwa,
wakate rufaa.
Kauli hiyo, ilitolewa jana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Laurean Ndumbaro,
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
“Kama mtakumbuka, uhakiki wa vyeti feki kwa watumishi wa umma,
ulihusisha vyeti vya kidato cha nne, kidato cha sita, ualimu na taaluma
zingine.
“Baada ya uhakiki huo, iliagizwa watumishi 9,932 waliokuwa na
vyeti feki, waondolewe katika ajira, watumishi 1,538 wenye vyeti vyenye
utata kwa maana kwamba vinatumiwa na watu zaidi ya mmoja, wathibitishe
vyeti vyao kabla ya Mei 15 mwaka huu na mishahara yao isimamishwe hadi
uhakiki utakapokamilika.
“Wale watumishi 11,596 waliogundulika kuwa na vyeti pungufu,
wanatakiwa kuwasilisha vyeti vyao vikaguliwe kabla ya Mei 15, mwaka huu,
vinginevyo watachukuliwa hatua.
“Lakini, wale wanaodai kwamba wamewekwa kwenye orodha ya wenye
vyeti feki wakati hawakutakiwa kuwa huko, tunawaomba waandike barua za
kukata rufaa kwa Katibu Mkuu Utumishi kupitia kwa waajiri wao.
“Waajiri hao, watatakiwa kuwasilisha vyeti hivyo Baraza la
Mitihani la Taifa kwa ajili ya uhakiki zaidi kabla ya Mei 15, mwaka huu.
“Pamoja na hayo, ieleweke kwamba, baadhi ya watumishi wakati
wanaajiriwa, waliwasilisha vyeti vya matokeo mengine ya sekondari na
wakati wa uhakiki, walionyesha vyeti vingine.
“Lakini, naomba ieleweke kwamba, hakuna mtumishi wa umma mwenye cheti halali atakayeondolewa katika utumishi wa umma.
“Kuhusu suala la mafao ya watumishi hao, hilo tunaliangalia namna ya kulifanya kwa sababu kuna sheria zinazolisimamia,” alisema Dk. Ndumbaro.
Ajira za dharura
Pamoja na hali hiyo, Dk. Ndumbaro aliwataka wakuu wa idara ambazo
huduma zake zimeathiriwa na zoezi la vyeti feki baada ya watumishi
kuacha kazi kwa kuwataka kuandika barua kwake ili zitangazwe nafasi za
ajira za dharura kwa lengo la kuziba mapengo hayo.
Akizungumzia wizara ambazo taarifa za uhakiki wake hazikutolewa
hivi karibuni, alisema zitatolewa Mei 10 mwaka huu baada ya uhakiki wake
kukamilika.
Katika hatua nyingine, Dk. Ndumbaro alisema Serikali itaajiri
watumishi 1,500 kuanzia sasa hadi mwisho wa Bunge la Bajeti
linaloendelea mjini hapa. Kwa mujibu wa Dk. Ndumbaro, ajira hizo zimetolewa ili kukabiliana
na uhaba wa watumishi wa umma ulioko katika sekta mbalimbali serikalini.
“Katika hili, waajiri watatakiwa kuhakiki vyeti vya waombaji
wote kabla hawajaajiriwa ili kuepuka uwepo wa watumishi wengine wenye
vyeti feki,” aliagiza.

0 comments:
Post a Comment