Msanii wa Bongo Fleva, Nandy amesema kwa sasa hayupo tayari kuishi pekee yake kwani bado anatamani kuendelea kuishi na wazazi wake.
Muimbaji huyo amesema anafurahia kuishi na wazazi wake kwani wanamchango kwenye kile anachokifanya ingawa kazi zinazompelekea kutoka usiku zimekuwa zikimpa changamoto kwani haipendezi hasa kwa mtoto wa kike.
“Hapana hata kidogo kwa sababu bado kuna vitu nahitaji kutoka kwa wazazi wangu na nikiwa nao karibu nafanya vitu vingi sana vya maana kuliko nikiwa nao mbali,” Nandy amekiambia kipindi cha Leo Tena cha Clouds FM.
Nandy ameongeza kuwa wakati anaanza muziki wazazi wake walikuwa wanampinga kwa sababu alikuwa bado ni mdogo na walihitaji asome kwanza, lakini alipokuja kwenda nchini Nigeria kwa ajili ya muziki wakaona yupo makini upande huo ndipo wakaanza kukubali anachofanya.
Katika hatua nyingine muimbaji huyo amesema kwa sasa yupo katika mahusiano na kuweka wazi sifa za mpenzi wake, huku akikanusha taarifa za kuwahi kutoka kimapenzi na MC Pilipili.
“Kwa sasa hivi… yes!, mimi ni mwanamke na ni binti nina mahusiano, lakini more detail mpaka itakapofikiwa wakati watu wataelewa zaidi lakini sasa hivi wajue… ni mcha Mungu, mcheshi, ana hekima, mchapa kazi ,” amesema Nandy.
0 comments:
Post a Comment