Posted by Williammalecela.com on Thursday, June 15, 2017
Muonekano wa nje wa ndege ya Boss wa Barrick Gold Corporation
Sehemu ya ndani ya Gulfsytream IV
Herry Oppenheimer akishuka katika uwanja wa ndege Mwadui 1952 kama vile alivyoshuka Thornton Lawson wa Barrick 2017
Siku kadhaa za "Makinikia" (japo TUKI wamesema tuite maboso na si makinikia) zimekuwa ni za kubandika na kubandua.
Toka katika kuta za masoko makubwa ya hisa ya London Stock Exchange,New
York Stock Exchange nk,hadi viunga vya Tandale na Sitimbi,kila mwenye
utashi wa kisiasa anaongelea juu ya Barrick,Magufuli na Makinikia,na
usipomtaja Tundu Lissu,basi mjadala unakosa nakshi.
Lolote linalohusu Barrick,JPM au Tundu Lissu na maboso,limekuwa ni
habari inayoweza kuuza ukurasa wa kwanza wa magazeti makubwa na madogo.
Hata ndege aliyokuja nayo "boss" wa Barrick toka Canada mpaka Dsm
imekuwa ni "habari",ndiyo maana msemaji wa Ikulu ndugu G.Msigwa ameweka
ujio wa ndege binafsi ya boss wa makinikia kama sehemu ya "Content" ya
taarifa ya Ikulu kwa umma wa Watanzania.Ndege hiyo nayo imekuwa ni
"habari",katika taarifa ya Ikulu,Mr Msigwa anaweka msisitizo wa "ujio Mr
Thornton akiwa na ndege binafsi"
Thornton J.Lawson ametua Tanzania na ndege binafsi aina ya Gulfstream IV
(GIV),yenye usajili wa Canada unaosomeka kama C-FHPM.Hii ni moja kati
ya ndege za anasa zinazotumiwa na matajiri na viongozi wenye ukwasi
duniani.Ni bahati mbaya au nzuri,kuna baadhi ya viongozi wa nchi za
Kiafrika,licha ya ufukara na umaskini wa wananchi wao,ndege jamii hii ni
moja ya ndege zinazomilikiwa kwa usafiri binafsi wa marais hao.
Gulfstream ni ndege inayoweza kukaa hewani masaa zaidi ya 14 bila kugusa
ardhi,uwezo wa kubeba tani 40 za mafuta na speed ya 980km kwa
saa.Imetengenezwa kubeba abiria kati ya 09 hadi 11.
Hiyo ya boss wa Barrick imekuwa "configured" kubeba watu sita tu,chumba
cha kulala,ukumbi wa mikutano,sehemu ya kupumzikia,choo na bafu.Kwa
umuhimu wa ujio wa kibiashara katika ardhi ya makinikia,boss wa Barrick
amesafiri toka Canada mpaka Dsm akiwa peke yake ndani ya chombo hicho
kama abiria.
Kwenye "Flight Tracking History" ya ndege hiyo,inaonekana ilitoka Canada
kuvuka bahari ya Atlantic,ikatua Nice Côte d' Azur International
Airport katika jiji la Nice Ufaransa kwa ajili ya kujaza mafuta,na
baadae kunyanyuka moja kwa moja kwa masaa saba na nusu hewani hadi
katika ardhi ya Dar es Salaam.Majira ya 1945(UTC) ambayo ni sawa na saa
2245 za huko Afrika Mashariki Gulfstream IV iligusa ardhi ya Tanzania.
Hii inatokea baada ya Barrick kupoteza mvuto katika masoko makubwa ya
hisa ya Ulaya na Amerika.Ujio wa Thornton,mazungumzo na baadae
maafikiano juu ya "mgogoro" huu wa kiuchumi,unarudisha taswira chanya
katika ulimwengu wa biashara ya madini iliyobebwa na familia za
kiyahudi.
Masaa matatu baada ya mkutano wenye tabasamu mbele ya waandishi wa
habari kati ya Rais wa nchi na Chief Executive wa Barrick Gold
Corporation,hisa za Barrick zinapanda kwa kasi katika masoko makubwa ya
hisa,na safari ya Thornton J Lawson,bingwa wa "fitna" za biashara ya
madini inaonekana kuwa yenye mafanikio makubwa kwa wadau na wanahisa wa
Barrick Gold Corporation.The deal is Done!!!
Hii inarudisha nyuma miaka zaidi ya 60,baada ya Dr John Williamson
mmiliki wa mgodi wa Mwadui kuwawekea ngumu kampuni ya De Beers kuwa
mshirika na mwanahisa wa almasi ya Mwadui.Hali hii ilifanya thamani na
soko la almasi ya Afrika Kusini kuporomoka katika soko kuu huko London
na De Beers kutikisika kiuchumi.
Machi 1952,kampuni ya De Beers ilimpandisha ndege mwanafamilia,mtoto wa
kwanza wa mmiliki wa kampuni,Mr Herry Oppenheimer kwenda Mwadui na
kuweka mambo sawa,ili kuimarisha soko la almasi ya Afrika Kusini kule
London,na kujihakikishia umiliki wa asilimia kadhaa katika mgodi wa
Mwadui.
Wakati Herry akipanda ndege kurudi Afrika Kusini,taarifa zilishafika
London kuwa sasa almasi ya Mwadui na ile ya Afrika Kusini zitachanganywa
katika soko kuu la London.Heshima ya Be Beers katika ulimwengu wa
madini ikapanda maradufu na kwa faida kubwa.Historia ile ya mabeberu wa
madini inajirudia,na wajukuu wetu wataikuta na kuisoma katika vitabu vya
kumbukumbu.
Wakati mwaka 1992,Nicolas Oppenheimer mtoto pekee wa Herry Oppenheimer
aliyegonga mwamba kwa Nyerere alipanda ndege kuja kuchukua 75% za mgodi
wa Mwadui na kuiacha 25% isiyoeleweka mikononi mwa serikali,leo Thornton
Lawson anapanda ndege toka Canada kuja Tanzania,kuweka mambo sawa ili
kile wanachokibeba kwa "utapeli wa kisheria" kiangaliwe upya na
kujadiliwa.
Tunaweza kuwa na tofauti za vyama na mtazamo wa kiitikadi,lakini
hatuwezi kuwa vipofu wa kutotambua "kiburi cha rasilimali" ambacho Rais
amejaribu kuwaonyesha mabepari wa madini,wakawasha ndege saa moja baada
ya hotuba ya Rais na kuanza kuitafuta anga ya Tanzania kuja kuweka mambo
sawa.
Zamani walitutumia tiketi za ndege tukawafuata katika hotel zao na
kujadiliana juu ya mali zetu,sasa wanawasha ndege zao za kifahari na
kutia mafuta kutufuata katika ardhi yetu.Hata kama watatushinda,lakini
kiburi cha rasimali zetu tumewaonyesha.
Barafu wa JF
0 comments:
Post a Comment