Waziri Mkuu Majaliwa ametoa miezi mitatu kwa wananchi wote waliojenga ndani ya eneo la mpaka wa Tanzania na Zambia kubomoa nyumba zao huku akiiagiza (TRA) kuanza kuweka alama za X katika nyumba 252 zilizojengwa ndani ya mpaka huo ili wahusika wabomoe
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo wakati alipotembelea eneo la ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha (OSBP) katika mpaka wa Tanzania na Zambia, ambacho kinajengwa na serikali ya Tanzania na kitakachogharimu sh. bilioni 12.
"Kuna watu wamejenga ndani ya mpaka wa Tanzania na Zambia na kuendesha biashara zao, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na linazikosesha serikali mapato. Natoa muda wa miezi mitatu kwa watu wote waliojenga kuanzia umbali wa mita 50 kutoka Tanzania na mita 50 kutoka Zambia kuzibomoa nyumba hizo kwa hiari wao wenyewe". Ametoa agizo hilo Waziri Mkuu
"Hatuna msamaha kwa watu waliojenga katika eneo hili kwa sababu wamesababisha tupoteze kodi nyingi, hivyo baada ya kumalizika muda huo mamlaka husika zibomoe nyumba zote zitakazosalia", amesema Majaliwa.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Nakonde nchini Zambia, Bw. Field Simwinga amesema wameshakubaliana na Waziri Mkuu Majaliwa katika maongezi yao na utekelezaji wa agizo hilo utaanza mara moja kwa kuwa jambo hilo linaathiri shughuli za mipakani kwa pande zote mbili.
0 comments:
Post a Comment