MKAZI wa Ubungo Kibangu Jijini Dar es Salaam Revocutus Mtiro (40) amefikishwa Mahakama ya Wilaya ya Ilala kwa tuhuma za kufanya Wizi kwenye Ofisi.
Akisomewa mashtaka hayo leo na Mwendesha mashtka wa Serikali Adolf Kisima mbele ya Hakimu E.R. Nassary alidai mshtakiwa huyo alitenda kosa kinyume na kifungu cha sheria cha 293 na 296(a) sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Ilidaiwa Mahakamani hapo mnamo Agosti 9 mwaka huu maeneo ya Samora Jijini Dar es Salaam mshtakiwa alivunja na kuingia ndani ya Ofisi ya Treasury Registral iliyopo kwenye jengo la CHC.
Kisima alidai baada ya kuingia ndani Mshtakiwa huyo alifanya tukio la wizi ambapo aliiba fedha taslimu shilingi milioni 51, 675, 900 mali ya Kampuni ya Treasury Registral.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo Mshakiwa huyo alipo ulizwa kuhusika na kosa hilo, alikana ambapo Mwendesha mashtaka alidai upelelezi bado haujakamilika.
Hakimu alitoa masharti ya dhamana ikiwa ni wadhamini wawili wa kuaminika mmoja awe na ajira kwenye sekta inayotambulika ambapo watasaini fedha taslimu shilingi milioni 25.
Hakimu alisema kesi hiyo itatajwa tena Septemba 4 mwaka huu ambapo mshtakiwa ameshindwa kukidhi masharti ya dhamana na amerudisha rumande.

0 comments:
Post a Comment