Na Judith Mhina – MAELEZO
Uwekaji jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi lenye urefu wa kilomita 1445 kutoka Wilaya ya Hoima nchini Uganda hadi Kijiji cha Chongoleani Mkoani Tanga, kumefungua fursa za biashara na uwekezaji na kuifanya Tanzania kujitangaza duniani kote.
Mafuta ni nishati muhimu sana katika maendeleo ya nchi yeyote ile, pia uwepo wake huharakisha maendeleo kwa kuwa soko lake ni kubwa na yanahitajika duniani kote. Mfano nchi za kiarabu ni tajiri na zimeharakisha maendeleo ya wananchi wake kwa kuwa kipato kitokanacho na mafuta ni kikubwa.
Hivyo basi, kuwekwa kwa jiwe la msingi la bomba la mafuta Tanga, ni fursa ambayo inautangaza mkoa huo, ni vema basi na sisi kama watanzania kuieleza dunia nzima kuna nini Tanga na pia apendaye kuwekeza katika sehemu hiyo aweze kujua ni fursa gani zinapatikana.
Jiwe la msingi limewekwa hivi karibuni na marais wa Tanzania na Uganda, Waheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na Yoweri Kaguta Museveni na kuandika historia mpya ya uwekezaji.
Fursa zinazopatikana Mkoa wa Tanga ni nyingi, kwa kuwa mkoa umebahatika kuwa na mazingira tofauti ya kijiographia katika sehemu za milima, miinuko na zile za tambarare.
Wilaya ya Tanga imebahatika kuwa na maeneo ambayo mfanyabiashara au mwekezaji anaweza kuwekeza katika kujenga viwanda vya samaki, mafuta ya nazi na biashara au utalii wa fukwe, mahoteli na ule wa kupiga kambi.
Aidha, eneo la Kigombe ambalo lipo mpakani mwa wilaya ya Tanga, Mheza na Pangani ni eneo pekee lililotambuliwa duniani kuwa na samaki adimu wa Silikant ambaye alitoweka miaka 6000 iliyopita. Eneo hilo, likatangazwa kuwa ni Hifadhi ya Bahari na Maeneo Tengefu pia, kuwa eneo la utalii wa baharini.
Wilaya ya Korogwe, ni eneo ambalo ndio hasa chimbuko la uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara. Mazao ya chakula ni kama mahindi, maharagwe, ndizi, viazi mviringo, vitamu na jamii za magimbi, matunda ya aina mbalimbali yaliyoletwa na wakoloni enzi hizo kama; peazi, machungwa, maembe, pichezi, matunda damu, zaituni, maparachichi, na nyanya. Mazao ya biashara ni korosho, katani, chai, mbao, mpunga na ufugaji wa ngombe wa maziwa na nyama, mbuzi, na kondoo.
Pia, mbuga ya Korogwe ina matunda kama vile maembe, machungwa, machenza, ndimu, limao, maparachichi, mapeazi, na mafenesi . Vilevile, kuna matunda ya asili yanayoota mbugani na ni maarufu sana hadi leo kama k’hole, kungwina, mavilu, ng’obe, ngoweda, zambarau, mkwaju na kunghuju.
Aidha, wilaya ina aina mbalimbali za mboga za majani ambazo zililetwa na wakoloni, kama spinachi, kabichi, Chinese, bamia, biringanyi, hoho, karoti, dengu, kunde, njegere na kweme. Halikadhalika, kuna mboga za asili zinazoota bila kupandwa, kwenye mashamba au mbugani kama mchunga, kibwando, bwache, mk’hota, tunguja, mwavu, mk’hobo, buluza, kisomanguo mgagani na tikini.
Mboga hizi za asili zinahistoria na makabila makuu matatu ya Tanga yaani wasambaa, wazigua na wabondei, ambao baadhi ya majina yao ndio hizo mboga kama; Mamsunga, makibwando, wanabwache, wanamkhota, satunghuja, samwavu, mk’hobo, wanabuluza, sesomanguo na mengine mengi.
Maeneo ya uwekezaji ni katika ranchi za ufugaji, katika maeneo yaliyotengwa, pia anaweza kupata maziwa ya kutosha kutengeneza bidhaa, zitokanazo na maziwa kama jibini, siagi, mtindi na zao la ngozi kuweka kiwanda cha viatu, mabegi, kuzalisha nyama na mazao yake.
Wilaya imetenga ekari kadhaa kwa ajili ya uwekezaji katika eneo la kiwanda cha sementi Mkomazi ambapo kuna madini aina ya gypsum kwa wingi. Vilevile kuna Hifadhi ya wanyamapori ya Mkomazi ambayo ni sehemu nzuri ya kutembelea na kuona uzuri wa nchi ya Tanzania.
Wilaya za Mheza na Mkinga zina utajiri mkubwa wa maeneo ya uwekezaji wa viwanda vya juisi ya matunda, ambapo wanazalisha kwa wingi machungwa ambayo ni matamu kuliko machungwa yeyote yalimwayo Tanzania, na huzalisha kwa misimu miwili kwa mwaka. Mazao ya biashara ni viungo kama tangawizi, iliki, pilipili manga, mdalasini, chai, kokoa, katani muhogo, mahindi, maharagwe mbogamboga na matunda.
Aidha, hifadhi ya Mazingira ya Taifa ya Amani ambayo ipo mpakani mwa wilaya ya Korogwe na Muheza kwenye zao la kokoa, chai, vipepeo, vyura na vinyonga wa rangi mbalimbali, wenye soko kubwa nchi za nje.
Eneo hili la utalii unaweza kuona tumbili wa rangi ya bluu, weupe na weusi na ni zuri kwa ajili ya utalii wa ndani na wa nje, hali ya hewa ya baridi na mvua zinapatikana mara kwa mara. Aidha, msitu mzuri wenye kuhifadhi maporomoko ya maji ya Amani yenye uoto wa asili unaopendeza na kuvutia.
Wilaya hizi mbili zina utajiri mkubwa wa samaki na uzalishaji wa lulu ya Chaza wa baharini kwa ajili ya kutengeneza urembo wa aina mbalimbali, wa kina mama na samaki aina mbalimbali, hivyo eneo linaloweza kuwekezwa kwenye upande wa kiwanda cha samaki.
Wilaya ya Handeni na Kilindi ni wilaya zenye utajiri mkubwa wa uzalishaji wa mahindi na maharagwe. Aidha, kuna madini ya aina mbalimbali kama green tourmaline, ruby na mengine mengi.
Pia eneo la Kilindi kuna milima ya Tao la Mashariki yenye maporomoko ya maji na wanyamapori ambapo ni eneo muhimu kwa uwindaji, vilevile kuna ranchi kubwa za ufugaji wa ng’ombe ambapo mwekezaji anaweza kuwekeza kwenye eneo hili la mifugo, halikadhalika kiwanda cha nyama au maziwa.
Wilaya hizi zimetenga maeneo ya uwekezaji katika kuanzisha ranchi za ufugaji wa ng’ombe wa nyama na unenepeshaji na ujenzi wa machinjio ya kisasa eneo la Mkata, kwa ajili ya usafirishaji nyama nje ya nchi na uuzaji katika maeneo ya migodi hapa Tanzania.
Wilaya ya Lushoto, ni kati ya wilaya zenye watu wengi katika Mkoa wa Tanga na wazalishaji wakubwa wa matunda na mbogamboga. Ambapo katika upande wa utalii, Lushoto ni kitovu cha utalii katika milima ya Usambara yenye misitu minene ya Maghamba na maporomoko ya maji na uoto wa asili na wanyama wadogo wadogo.
Aidha, wilaya inazalisha matunda ya asili ya maeneo ya baridi kama peazi, peachezi, matunda damu, parachichi, fyoksi, mapera na strawberry.
Katika Wilaya ya Pangani kuna utajiri mkubwa wa samaki wa aina mbalimbali na mazingira ya bahari ambayo yametunzwa vema kiasi cha kuwa na urithi mkubwa wa Kasa, ambao hutaga mayai kando kando mwa bahari ya hindi. Kasa hawa huvutia watalii wengi na watafiti wa kasa kutoka pande mbalimbali za dunia.
Aidha, pwani hii imerembeshwa na hifadhi ya Taifa ya wanyamapori ya Saadani. Hifadhi hii ni maarufu kwa vyakula vya mazao ya baharini, yanayopikwa kwa ufundi na wapishi mashuhuri ya eneo la Tanga.
Bomba la mafuta linakuja na fursa zake za ajira, ambapo waajiriwa hao watakuwa ni Waganda, Watanzania na wageni kutoka nje ya mataifa hayo, hao wote wanahitaji kuzitambua fursa zilizopo Tanga ili washiriki katika kushangaa maajabu ya Mkoa huo, au kutafuta wabia katika kuwekeza hapa nchini.
Hima bila kupoteza fursa husika linalowezekana leo lisingoje kesho. Tanzania ya viwanda hiyo ipo mlangoni ni vema ukaikaribisha ili tujenge Taifa letu. Hakika naungana na usemi wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kuwa nchi yetu ni tajiri sana na inapaswa kuwa nchi mhisani (donar country) ikisaidia nchi nyingine. Fursa zipatikanazo nchini hazinabudi kutumiwa ipasavyo kwa ajili ya maendeleo ya watanzania kwa ujumla.
0 comments:
Post a Comment