Monday, August 7, 2017


Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) imejitokeza mbele ya vyombo vya habari na kutoa taarifa ya kupinga tafiti zilizotolewa na kampuni ya GeoPoll
na kueleza kuwa tafiti hizo sio takwimu rasmi (Official Statistics) kwa kuwa hukusanywa kwa mfumo ambao hautambuliwi na Ofisi hiyo ya Taifa ya Takwimu.
Akizungumza juu ya tukio hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt. Albina Chuwa amebainisha kuwa, Ofisi yake inapenda kujulisha umma kuwa takwimu hizo za Geo Poll sio rasmi na hazikufuata mfumo unaotambuliwa na Ofisi yake hapa nchini huku ikikiuka kifungu cha 20 cha Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015.
“Takwimu hizi sio sahihi na sio rasmi. Tunapenda kujulisha umma juu ya hilo. Hivyo takwimu za GeoPoll sio sahihi na waache mara moja na wafuate taratibu na vigezo vilivyowekwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu. Suala la takwimu sio kama mtu anaenda kukata majani shambani, zinautaratibu wake wa kuzikusanya tunataka wafuate utaratibu zilizowekwa.” Ameeleza Dk. Albina Chuwa.
Dk. Albina Chuwa ameeleza kuwa, hivi karibuni kumekuwa na takwimu zinazotolewa na kampuni ya GeoPoll yenye ofisi ya Kanda ya Afrika, mjini Nairobi nchini Kenya. Ambapo amebainisha kuwa Takwimu hizo ambazo hutolewa kwa njia ya mitandao ya kijamii, zinahusu ukusanyaji wa taarifa za televisheni na Redio nchini kwa idadi ya watazamaji na zinazotolewa kila baada ya miezi mitatu.
Hata hivyo, Dk. Albina Chuwa ameweka wazi kuwa, Takwimu zinataratibu zake kwa nchi yoyote ile hivyo hawapo tayari kuona watu wanaingia nchini na kufanya shughuli za takwimu bila kufuata misingi na miongozo iliyopo kwani ni kukiuka kanuni na misingi ya sheria iliyopo.
“Kifungu cha 20 cha Sheria ya takwimu ni takwimu ambazo zimetolewa kwa kufuata misingi ya utoaji takwimu rasmi (Fundamental Principles of Official Statistics) na utolewaji wake umeratibiwa na Ofisi yetu ya Taifa ya Takwimu, Hivyo basi, takwimu zinazotolewa na taasisi au mtu yeyote zitatambuliwa kuwa Takwimu rasmi iwapo tu zitakidhi vigezo vinavyotolewa na kusimamiwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Kwa mantiki hiyo, takwimu zinazotolewa na mtu ama taasisi yeyote bila kufuata au kukidhi vigezo vinavyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa mujibu wa sheria ya Takwimu, hazitambuliwi kuwa ni takwimu rasmi na kwa maana hiyo haziwezi kutumika katika kupanga mipango ya maendeleo ya nchi.” Alifafanua Dk. Albina Chuwa.
Kwa hatua hiyo, Dk. Albina Chuwa amesema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaitaka kampuni hiyo ya GeoPoll kufuata taratibu zote zilizoainishwa katika sheria ya Takwimu, kwani takwimu zao hazikukidhi vigezo na zimekuwa zikileta mkanganyiko kwa wadau pamoja na kuathiri mahusiano ya kiutendaji baina ya vyombo vya habari hapa nchini.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ni taasisi ya Umma iliyoanzishwa kwa sheria ya Takwimu ya mwaka 2015. Kwa mujibu wa sheria hiyo, Ofisi hiyo imepewa mamlaka ya kutoa, kusimamia na kuratibu upatikanaji wa takwimu rasmi kwa ajili ya matumizi ya Serikali na wadau wa takwimu.

0 comments:

Post a Comment