Posted by Williammalecela.com on Tuesday, August 01, 2017
 |
MIAKA
34 iliyopita, siku kama ya leo (Agosti 1, 2016), zaidi ya wanajeshi 100
na raia 200 waliuawa kwenye jaribio la mapinduzi nchini lililotibuka.
Wanawake walibakwa na baadhi yao walijiua kwa kutendewa unyama. Uchumi
wa Kenya ulipata hasara ya Sh500 milioni kwa kuvurugika kwa saa 12.
Mnamo siku hiyo maafisa wa vyeo vya chini wa kijeshi walijaribu
kupindua serikali ya Rais Daniel arap Moi, shughuli iliyochukua saa 12.
Mmoja wa wanajeshi waliopanga mapinduzi hayo alikuwa Senior Private
Hezekiah Ochuka Rabala, aliyejitangaza rais kwa saa sita pekee kabla ya
wanajeshi watiifu kwa serikali kutibua njama zake na wenzake.
Wanajeshi hao wa jeshi la angani, walitwaa kituo cha utangazaji cha
shirika la utangazaji la Kenya wakati huo kikifahamika kama Sauti ya
Kenya (VOK) na kutangaza sababu zao za kupindua serikali.
Kulingana nao, walichochewa kupindua serikali kwa sababu ya hali mbaya
ya uchumi na utawala mbaya. “Kwa hivyo, hali ya kutotoka nje imetangazwa
na watu wanashauriwa kukaa ndani ya nyumba zao.Mipaka yote imefungwa,
wabunge wote wakae ndani ya nyumba zao kwa usalama wao,” alitangaza Bw
Ochuka.
Polisi wote waliagizwa kuvua mavazi yao rasmi na kuwa raia wa kawaida, ishara kwamba wanajeshi walikuwa wametwaa mamlaka.
Baadaye ilibainika kuwa jaribio hilo la mapinduzi lingezimwa mapema.
Shirika la ujasusi la Kenya, wakati huo likifahamika kama Special
Branch, lilikuwa limepenya katika jeshi na lilifahamu kwamba baadhi ya
wanajeshi walipanga kupindua serikali.
Maafisa wa Special Branch
walikuwa na majina ya wanajeshi waliopanga mapinduzi hayo lakini
walipoomba ruhusa ya kuwakamata siku mbili kabla ya Agosti 1 1982 Rais
Moi alikataa.
Miongoni mwa wanajeshi ambao aliyekuwa mkuu wa
ujasusi wakati huo James Kanyotu aliomba Rais Moi kumruhusu kuwakamata
walikuwa Sajini Joseph, Koplo Charles Oriwa, Koplo Walter Ojode, Koplo
Bramwel Injene Njereman na Senior private Protas Oteyo Okumu na Hezekiah
Ochuka. Walivyotwaa serikali
Rais Moi hakudhani kwamba ingekuwa
vyema kwa polisi kuingilia masuala ya kijeshi na alimweleza Bw Kanyotu
kwamba suala hilo lingetatuliwa Jumatatu ya Agosti 2 1982. Hata hivyo,
saa sita usiku wa Agosti 1, wanajeshi waliopanga mapinduzi hayo walitwaa
Sauti ya Kenya, Benki Kuu ya Kenya kwa kile walichotaja kama kulinda
pesa za umma.
Aidha, walipanga kulipua Ikulu ya Nairobi na makao
makuu ya jeshi (DOD) jambo ambalo halikufaulu. Waliwateka baadhi ya
marubani wa ndege za kivita na kuwalazimisha kushiriki katika ulipuaji
huo.
Kapteni Jorim Nyamor, mmoja wa marubani hao alisimulia jinsi
alivyotekwa kutoka nyumbani kwake Nairobi na kupelekwa Nanyuki ambako
operesheni ya mapinduzi ilipangiwa.
Hii ilikuwa muda mfupi tu
baada ya Hezekiah Ochuka kutangaza kuwa jeshi lilikuwa limepindua
serikali. Ochuka alikuwa na kiongozi wa wanafunzi wa chuo kikuu cha
Nairobi Titus Adungosi.
Kapteni Nyamor alisema alikamatwa pamoja na wanajeshi wengine baada ya kuagizwa na watekaji wake kulipua DOD.
“Niliwauliza wanipe muda wa saa moja au mawili kwa sababu nilikuwa na
jambo la dharura la kushughulikia na walikubali,” Kapteni Nyamor ambaye
baadaye aliajiriwa na Shirika la Ndege la Kenya alisema alipohojiwa na
Taifa Leo 2012.
“Tulipelekwa jela ya Kamiti na baadaye
tulipelekwa Naivasha ambapo tuliteswa” alisema. Alisema waliwekwa kwenye
maji baridi kwa miezi minane lakini baadaye hawakupatikana na hatia na
walistaafishwa kwa lazima baada ya kulipwa Sh60 pekee. Kunyongwa
Wanajeshi waliopatikana na hatia, akiwemo kiongozi wa mapinduzi hayo, Ochuka walinyongwa katika jela la Kamiti. Walikuwa wafungwa wa mwisho kuuawa baada ya kuhukumiwa kunyongwa nchini Kenya, kulingana na rekodi za magereza.
Japo jaribio hilo lilikuwa la kijeshi baadhi ya wanasiasa walitajwa
kuhusika akiwemo kiongozi wa Cord Raila Odinga ambaye wakati huo alikuwa
naibu mkurugenzi wa Shirika la Ukadiriaji bidhaa la Kenya.
Alikamatwa na kushtakiwa kwa uhaini lakini baadaye mashtaka dhidi yake
yaliondolewa. Mwingine alikuwa ni Rateng Oginga Ogego aliyekuwa
mwanafunzi wa somo la sayansi ya kisiasa katika chuo kikuu cha Nairobi
wakati huo.,Baadaye aliteuliwa balozi wa Kenya Amerika. Ogego
alishtakiwa na kufungwa jela miaka sita. Aliambia mahakama ya rufaa
kwamba alijuta kwa sababu jaribio hilo lilifeli na hukumu yake
ikaongezwa hadi miaka 10 jela. Isaac Ruto ndani
Bw Isaac Ruto,
ambaye kwa sasa ni Gavana wa Bomet aliyekuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili
katika chuo kikuu cha Nairobi wakati wa jaribio hilo na naibu
mwenyekiti wa chama cha wanafunzi. Alikamatwa na kuachiliwa baada ya
mwezi mmoja.
Mfanyabiashara Shem Ochuodho, ambaye wakati mmoja
alikuwa mbunge wa Rangwe. Alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu chuoni na
mwanachama wa baraza la chama cha wanafunzi. Alikamatwa kwa kushiriki
maandamano haramu na kusukumwa jela miezi sita.
Wengine ambao
walinusurika walikuwa ni Philip Murgor ambaye alisukumwa jela miezi sita
kwa kuhusishwa na mapinduzi hayo. Baba yake Charles Murgor alikuwa
naibu waziri.
Kiongozi wa Amani National Congress Musalia
Mudavadi ambaye alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo kikuu
cha Nairobi alitoweka baada ya jaribio hilo la mapinduzi lakini baada ya
siku tatu alijitokeza nyumbani kwao Vihiga. Alikamatwa na kuachiliwa baada ya siku tatu.
|
0 comments:
Post a Comment