Monday, August 21, 2017

Image result for mbarawa images

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema ujenzi wa barabara ya juu Tazara Flyover katika makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela eneo la Tazara
unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba mwakani ili kuanza kutumika na wananchi ikiwa ni azma ya Serikali ya kupunguza foleni jijini Dar es Salaam.

Waziri Mbarawa ameyasema hayo wakati Rais wa Shirika la kimataifa la Maendeleo la Japani (JICA), Dkt. Shinichi Kitaoka alipokagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo ya juu ambao unatekelezwa baina ya Tanzania na Serikali ya Japani.

"Ujenzi unaendelea vizuri na sasa umefikia asilimia 53, tutahakikisha kasi ya ujenzi huu inaendelea ili barabara hii ikamilike kwa wakati na kuanza kutumika, wananchi wamekuwa wakipoteza muda mwingi takribani masaa mawili hadi matatu kwa ajili ya kuvuka sehemu hii,” amesema Profesa Mbarawa.




Aidha, Waziri Mbarawa ameishukuru Serikali ya Japani kwa kuweza kufadhili mradi huo ambao utasaidia kupunguza msongamano wa magari katika makutano hayo na hivyo kurahisisha usafiri kwa wakazi wanayoitumia barabara hiyo.

"Kwa niaba ya Mheshimiwa Raisi wetu Dkt. Johm Pombe Magufuli, tunaishukuru Serikali ya Japan kwa kuweza kushirikiana na serikali yetu katika kukamilisha miradi mbalimbali hapa nchini pamoja na mradi huu," amesisitiza Profesa Mbarawa.


Profesa Mbarawa amewataka wananchi wanaotumia miundombinu ya barabara kuendelea kutunza miundombinu hiyo ambayo Serikali inatumia gharama kubwa kuijenga ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuchochea kukuza uchumi wa nchi.

Kwa upande wake Raisi wa Rais wa JICA Dkt. Shinichi Kitaoka amesema kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutaboresha mfumo wa miundombinu ya usafiri na JICA itahakikisha kazi ya Ujenzi huu inafanyika na kukamilika kwa wakati.

Mradi wa Tazara Flyover umefadhiliwa na Serikali ya Japani kupitia JICA na hadi kukamilika kwake utaghalimu shilingi Bilioni 99.

Chanzo: ITV

0 comments:

Post a Comment