Wakati
kumbukumbu za ripoti za uchunguzi wa usafirishaji wa mchanga wa madini
(makinikia) nje ya nchi zikiwa bado zinawatafuna watanzania walio wengi
kuhusu hatma ya nchi yetu katika sekta ya madini baada ya taarifa
kuonyesha tumeibiwa sana, kidonda hicho kimetonyeshwa upya jana baada
ya kamati mbili za bunge kuwasilisha ripoti kuhusu biashara ya madini ya
Almasi na Tanzanite.
Kamati
ya iliyochunguza biashara ya madini ya Almasi imeongozwa na Mbunge wa
Ilala, Mussa Azzan Zungu huku Kamati ya Tanzanite ikiongozwa na Mbunge
wa Bukombe, Doto Mashaka Biteko.
Wakati
wenyeviti wa kamati zote wakiwasilisha ripoti zao mbele wa Spika wa
Bunge na viongozi wengine waandamizi wa serikali na vyombo vya ulinzi,
wameonyesha namna serikali inavyopata hasara kutokana na kusainiwa kwa
mikataba mibovu, rushwa, biashara za kupendeleana, maamuzi ya kukurupuka
lakini pia na uzembe wa viongozi walioaminiwa kulinda rasilimali hiyo
adimu.
Moja
ya jambo lililowashtua watu wengi na pengine kuleta mfadhaiko, ni baada
ya Mwenyekiti wa Kamati ya Almasi, Mussa Azzan alipokuwa akieleza moja
ya sababu zilizosababisha serikali kupata hasara na kubambikiwa madeni
ni kiongozi aliyekuwa akihusika na uhakiki wa madeni hayo kutokuwa
makini.
Zungu
alisema, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi wa Madini Nchini,
Profesa Abdulkarim Hamis Mruma amelisababishia taifa hasara kwa kuruhusu
madini yapotee kwa uzembe.
Prof.
Mruma ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kwanza ya Makinikia
iliyoundwa na Rais Magufuli alipohojiwa sababu za kusababisha hasara
hiyo na serikali kubambikiwa madeni ambayo si halali alisema, nyaraka
hizo za madini alizisaini bila kusoma.
Kamati
ilipohoji kwanini kiongozi wa ngazi ya juu kama yeye anasaini nyaraka
bila kuzisoma alisema kuwa alikuwa ametingwa na kukosa muda wa kusoma
ripoti zilizoletwa kwake, lakini pia alikuwa anawaamini waliokuwa
wakizileta ndio sababu hakusita kuzisaini.
Prof.
Mruma alijizolea sifa nyingi alipowasilisha ripoti ya uchunguzi wa
makinikia ambapo yeye na wajumbe wengine wa kamati walikuwa wakichunguza
aina ya madini iliyokuwa katika mchanga huo. Katika ripoti yake
alionyesha namna taifa linavyopoteza matrilioni fedha kutokana na
usafirishwaji wa mchanga wa madini nje ya nchi.
Wengine
walionaswa na kamati hizo ni waliokuwa Mawaziri wa Wizara ya Nishati na
Madini, Prof. Muhongo na William Ngeleja ambao wao kwa nyakati tofauti
inadaiwa walitoa leseni za uchumbaji madini kwa kampuni mbalimbali mfano
Tanzanite One kinyume na sheria.
Aakieleza
zaidi Zungu alisema, kuna leseni moja ya madini ambayo serikali
ilishauriwa na kamati nyingi kutoitoa, lakini Prof. Muhongo siku chache
baada ya kuingia madarakani alitoa leseni hiyo.
Mwingine
anayetuhumiwa kuisababishia serikali hasara ni pamoja na Naibu Waziri
wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani wakati
akifanyakazi katika Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) ambapo kamati
imeeleza kuwa alishindwa kusimamia wajibu wake vizuri na kulisababishia
taifa hasara.
Aidha,
miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na kamati hizo, ni serikali
kuwachukulia hatua watumishi wote waliohusika kwa namna moja ama
nyingine katoka kulisababishia taifa hasara.
Lakini
pia kamati zimependekeza kupitiwa kwa mikataba ya kampuni za uchimbaji
madini kwani biashara hiyo imekumbwa na rushwa na uongo, hali
inayosababisha serikali kupata hasara.

0 comments:
Post a Comment