Friday, August 29, 2014

1Mganga Mfawidhi wa hosptali ya wilaya ya Iringa Dk. Mbaraka Mgangachuma akipanda mti uliotolewa na chama cha pool mkoa wa Iringa walipokwenda kutoa msaada wa kiti cha kubebea wagonjwa na kupanda miti katika hospitali hiyo.
…………………………………………………………………………..
Na Denis Mlowe,Iringa
 
MASHINDANO ya mchezo wa Pool mkoa wa Iringa yanayodhaminiwa na kampuni ya bia TBL kupitia kinywaji chake cha Safari Lager yamezinduliwa rasmi jana kwa chama cha pool mkoa wa Iringa kutoa msaada wa kiti cha kubeba wagonjwa na kupanda miti katika hospital ya wilaya ya Iringa Frelimo wenye thamani ya shilingi 350,000.
 
Akizungumza katika uzinduzi wa mashindano hayo yanayofanyika katika bar ya New Life mgeni Rasmi Afisa Utamaduni wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Carlos Mbinda alisema mashindano ya pool yamekuwa chachu ya ajira kwa vijana wengi katika mkoa wa Iringa na Tanzania kwa ujumla na kuwataka vijana kuuchukulia mchezo wa Pool kuwa mchezo rasmi kama michezo mingine ya mpira wa miguu.
 
Alisema vijana wengi wanapenda michezo lakini wanakosa ushirikiano kutoka katika serikali katika kuweza kufanikisha kuwepo kwa michezo hiyo hivyo kuwataka wadau mbalimbali kuwasaidia vijana katika kuundeleza mchezo wa pool ambao unazidi kuchukua kasi nchini na kuwa kimbilio la ajira kwa vijana wengi.
 
Aliishukuru kampuni ya bia ya TBL kupitia kinywaji cha Safari Lager kwa kudhamini mashindano hayo na kutoa wito kuendelea kudhamini mashindano hayo kuanzia ngazi za mita, kata, wilaya, mkoa na kisha kitaifa
 
“TBL wanafanya kazi kubwa sana kuisaidia serikali katika kuongeza ajira kwa njia ya michezo hususani kinywaji chake  cha safari lager hivyo ni jambo la kuwashukuru sana na natoa wito kwa uongozi wao kuwa waendelee kudhamini mashindano haya kwani ni muhimu sana katika kupambana na janga la maambukizi mapya ya ukimwi” alisema Mbinda
 
Aliwapongeza viongozi wa mchezo wa Pool mkoa wa Iringa kupitia mchezo huo kutoa msaada katika hospitali ya Wilaya ya Iringa ya Frelimo na kuwataka wanamichezo kuwa na moyo wa kujitolea wanapopata nafasi.
 
Kwa upande wake katibu wa mchezo wa Pool mkoa wa Iringa, Hadji Kiyeyeu aliishukuru TBL kwa kuwadhamini katika mashindano ya mkoa na kuwataka wanamichezo kuwatendea haki kampuni hiyo kwa kuwa wawakilishi wazuri katika maeneo yao wanayoishi.
 
Kiyeyeu alisema timu zinazoshiriki mashindano hayo mwaka huu ni timu nane ambazo ni Nginja Master, Garden, Embalasasa, Soko kuu, Kigoma Pub, Shooters Pub, Mountain City na Dabaga Road.

0 comments:

Post a Comment