Posted by Williammalecela.com on Tuesday, October 28, 2014
aliyekuwa
Katibu Myeka wa Mwalimu, Samwel Kassori, ilibainisha namna Mwalimu
alivyohuzunishwa na suala la kuuzwa kwa NBC kwa mojawapo ya makampuni
kutoka nchini Afrika Kusini.
“Lakini moja
kubwa ninalokumbuka ni kuhusu mchakato wa uuzwaji wa benki ya NBC mwaka
1997 mwezi Aprili wakati wa utawala Mkapa ambapo Mwalimu aliwahi
kulengwalengwa na machozi akipinga benki hiyo kuuzwa kwa ABSA Group
kutoka Afrika ya Kusini.
“Wakati huo
nakumbuka serikali ilipanga kumwandalia Mwalimu sherehe ya kitaifa ya
siku yake ya kuzaliwa (birthday) ya kutimiza miaka 75 ambazo
zingefanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee wa Jijini Dar es Salaam,
na jambo hilo lilimshtua kidogo akaniagiza nichunguze fedha hizo
zingetoka wapi na kwanini afanyiwe sherehe kubwa kiasi hicho na pia
tetesi zilikuwa zimezagaa kuwa NBC inauzwa.
“Wakati huo
Waziri wa Fedha alikuwa Daniel Yona, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo alikuwa
Peter Ngumbulu na Gavana wa Benki Kuu (BoT) alikuwa Dk. Idris Rashid.
“Baada ya
kupata taarifa za kwamba benki hiyo iko mbioni kupigwa bei, Mwalimu
aliomba maelezo kutoka kwa wahusika ambao ni Waziri wa Fedha, Katibu
Mkuu na Gavana wa BoT.
“Majibu ya
serikali yalikuwa kwamba NBC inauzwa kwa sababu taasisi za fedha za
Kimataifa za Fedha (IMF) na Benki ya Dunia (WB) ziliagiza Benki hiyo
kuuzwa.
“Baada ya
kupata maelezo hayo Mwalimu alikasirika kweli kweli, akaniita na tukiwa
nyumbani kwake Msasani aliniagiza kumpigia simu Rais wa (WB) wakati ili
azungume naye.
“Baada ya
kumpata Rais huyo wa (WB) ambaye bado alikuwa akimwita Mwalimu Mr.
President (Mheshimiwa Rais), alikana IFM pamoja na Benki ya Dunia
kushinikiza au kutoa masharti kuuzwa kwa NBC.
“Namnukuu Rais
huyo wa WB aliniambia:”Mr Kasori do me a favour could you request
President Nyerere to come to our headquarters in Washington and read
the documents from Tanzania government, they are too voluminous but will
try to make executive summary of the same”
“Maana yake ni
kwamba walitaka Mwalimu akajioonee mwenyewe nyaraka zilizotumwa katika
taasisi hizo za kimataifa kuhusu uuzaji wa NBC na walisema wangelipa
gharama zote muhimu za safari hiyo.
“Baada ya
mazungumzo ya simu siku mbili baadaye tulifunga safari na Mwalimu hadi
Washington nchini Marekani ambapo tulikutana na Rais wa WB kwa kikao cha
siku nzima na kupitia nyaraka muhimu zilizowasilishwa kwao na serikali
ya Tanzania.
“Tulirudi
nyumbani baada ya wiki moja na Mwalimu aliniagiza kwanza niwatafute
Yona, Ngumbulu na Dk. Rashid ili azungumze nao kabla ya kukutana na Rais
Mkapa.
“Basi baada ya
mimi kufanya mawasiliano nao wote hakuna aliyeitikia wito wa Mwalimu
“walimpuuza” na badala yake walimtuma Donald Kamori ambaye alikuwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC.
“Nakumbuka
vizuri kikao na Kamori kilifanyika Msasani nyumbani kwa Mwalimu Nyerere,
Aprili 13 mwaka huo 1997, na Kamori alikuwa mtaalamu aliyebobea katika
masuala ya fedha na ndiye kati ya wataalamu wazawa walioanzisha BoT.
“Kamori akiwa
na nyaraka na takwimu za kitaalamu. Alimweleza Mwalimu bila ya kuficha
kuwa kuiuza NBC serikali ilikuwa inafanya makosa makubwa katika sekta ya
fedha kwa kuwa Benki hiyo ilikuwa inaendeshwa kwa faida kubwa. Uuzwaji
wake ungeleta athari ya moja kwa serikali pamoja na taasisi zake nyeti.
“Mwalimu
alitikisa kichwa kwa masikitiko makubwa, akasema ‘ooooh kweli
nimesomesha Watanzania’ alikuwa amevutiwa sana na maelezo ya kitaalamu
ya Donald Kamori.
“Baada ya
kupata maelezo ya kutosha kutoka kwa Kamori, Mwalimu aliomba kukutana na
Rais Mkapa na kikao kilifanyika Ikulu ambapo alitetea NBC isiuzwe kwani
ndiyo ilikuwa nguzo ya serikali hasa wakati inapoishiwa fedha katika
mambo “nyeti yanayohusiana na usalama wa nchi” ilikuwa inakopa fedha
NBC.
“Majadiliano na
Mkapa yalichukua muda mrefu sana kuhusu suala hilo na itoshe kusema
kwamba baada ya majadiliano hayo marefu likazaliwa wazo la kugawanywa
kwa hiyo na kuanzishwa kwa Benki ya NMB ambayo serikali ina hisa hadi
leo.
“Kilichomsikitisha
zaidi Mwalimu ni kwamba baada ya juhudi zote hizo Kamori alifukuzwa
kazi kama Mkurugenzi Mtendaji wa NBC na kurudishwa BoT bila kupangiwa
kazi yoyote.Hakuwa na ofisi pale akifika anasoma magazeti aliyojinunulia
na kurudi zake nyumbani.
“Alitishwa sana
na kuhojiwa ni kwanini alikwenda kumweleza Mwalimu na kumwonyesha
nyaraka za uuzwaji wa NBC kwa Benki ya ABSA ya Afrika ya Kusini?
“Kamori
alinipigia simu akanieleza masahibu yaliyomkuta na mimi nikaufikisha
ujumbe wake kwa Mwalimu, baada ujumbe huo Mwalimu alisikitika sana,
akahoji ni kwanini wanafanya mambo hayo “kumfedhehesha” akiwa hai?
“Huyo Kamori
alikuwa mzalendo kweli kweli ni kati ya Watanzania walioipenda nchi yao.
Siku hiyo hiyo aliacha kazi akasema hawezi kupokea mshahara asioufanyia
kazi na akaenda kufanya kazi zake sijui kwa sasa atakuwa wapi.
“Sakata la
kuuzwa kwa NBC kwa kweli ni kati ya mambo yaliyowahi kumchanganya akili
Mwalimu na kwa upande wangu uuzwaji wa benki ile ulifungua milango ya
ufisadi mwingine uliokuja kufanyika miaka ya baadaye,” alisema.
0 comments:
Post a Comment