Tuesday, October 14, 2014





MWANASIASA mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru amewataka Watanzania kutokimbilia kugombea urais na badala yake waangalie namna ya kujikomboa kiuchumi ili nchi iweze kujitegemea.


Miongoni mwa watu waliojitokeza kutaka kuwania nafasi hiyo wazi wazi ni Mbunge wa Jimbo la Bumbuli, January Makamba na Mbunge wa Jimbo la Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla.

Wengine wanaotajwa kutaka nafasi hiyo ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye na Mbunge wa Jimbo la Sengerema, William Ngeleja, wote kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kingunge alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza kwenye hafla ya kumwapisha Kamanda wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mkoa wa Dodoma, Haidery Gulamali na kuwataka kufikiria zaidi nchi inavyoweza kuwainua watu wake ili waweze kutengeneza vitu mbalimbali, kama magari, ndege na kujenga reli.

Kingunge ambaye pia ni Kamanda Mkuu wa UVCCM Taifa, alisema pamoja na kwamba Tanzania imejikomboa mikononi mwa Mwingereza na kupata uhuru tangu mwaka 1961, lakini nchi inamtegemea katika suala zima la uchumi.

"Sasa sisi tumetosheka na madaraka tu, kila mtu anataka kuwa Rais, anataka kuwa mbunge, lakini nchi inabaki vile vile, kazi tunawafanyia mataifa mengine, tunaponunua magari kutoka Japan ni matumizi ya kile kidogo kinachopatikana, anayefaidika ni yule anayetengeneza na sisi tutaendelea kuwa maskini.

"Tumefanya suala la madaraka kuwa ndiyo jambo kubwa, hatujiulizi masuala makubwa na ya kimsingi, hivi kwa nini sisi kila kitu kikubwa tunachokihitaji kimetengenezwa na watu wengine, hayo ndiyo masuala ya kujiuliza na si kila mtu kutaka madaraka tu.
"Kwa sababu hatujiulizi maswali hayo na kuyafanyia kazi, wao wanaendelea kututawala kwa sababu tumepigania kujitawala, lakini bado hatujajitegemea, Mwalimu Julius Nyerere alisema 'kujitawala ni kujitegemea, kama hamjajitegemea hamjajitawala hasa sisi Waafrika bado hatujajitawala, maana hatujajitegemea kiuchumi bado," alisema Kingunge.

Kutokana na hali hiyo, alisema wana-UVCCM na wananchi kwa ujumla wanapaswa kutambua kuwa, siri ya maendeleo ya dunia ni maarifa ya kisasa ambayo yalimwezesha mzungu kutawala dunia hadi sasa, pamoja na nchi nyingi za Kiafrika kupata uhuru.
"Kutotumia sayansi na teknolojia za kisasa ndiko kunakotufanya tubaki kuwa tegemezi, vijana wakielewa siri ya maendeleo ya dunia na kuanza kutafuta, wawezeshwe sayansi na teknolojia, na wakianza kudai hivyo, wataanza kuleta mabadiliko nchini.

"Kwa hiyo tunasema kizazi cha sasa cha Waafrika kina changamoto mpya na kubwa zaidi, kizazi chetu sisi changamoto ilikuwa kubwa kweli, kumwondoa Mwingereza haikuwa kazi ndogo, kwa sababu alikuwa ametanda dunia nzima.

"Lakini nasema changamoto ya sasa ndiyo ya kukamilisha ukombozi wetu na kutokomeza unyonge  wa Mwafrika, ni changamoto ya kujiuliza maswali makubwa na kusema sasa tutafanya na kufika mahali vijana wetu ndiyo watengeneze reli, ndege, magari na teknolojia nyingi badala ya kula makombo yanayotengenezwa na nchi nyingine," alisema.
Kuhusu Katiba

Kuhusu Katiba iliyopendekezwa, aliwataka vijana kuisoma na kuilewa ibara kwa ibara. Alisema katiba hiyo imezingatia maslahi ya makundi yote yaliyopo nchini, lakini pia imezingatia maslahi ya sasa na vizazi vijavyo.

"Kwa vigezo hivyo, hiyo ni katiba bora, lakini msitosheke kuambiwa ni vizuri na ninyi  msome, mhamasishe wananchi wengine waisome na wakati ukifika wajitokeze kuipigia kura ya ndiyo," alisema.

0 comments:

Post a Comment