Posted by Williammalecela.com on Monday, November 03, 2014
Janeth Mbene
DAR ES SALAAM
NAIBU
Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene, ameangushwa na Kimwei
Mhita (27) katika kinyang’anyiro cha kura za maoni za kumtafuta
Mwenyekiti wa Mtaa wa Masaki atakayewakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Waziri
huyo ambaye alikuwa anatetea kiti hicho ambacho ameshikilia kwa muda
mrefu, amejikuta akiangushwa mwishoni mwa wiki na mwanasiasa huyo kijana
ambaye hana umaarufu mkubwa katika medani ya siasa za chama hicho
akilinganishwa na waziri huyo.
Mhita alishinda nafasi hiyo ya uenyekiti wa mtaa kwa kupata kura 119 huku Waziri Mbene akiambulia kura 27.
MTANZANIA
ilipomtafuta Waziri Mbene kupata maoni yake kwa kuangushwa katika
uchaguzi huo, simu yake iliita muda mrefu bila kupokelewa.
Hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa simu, pia hakuweza kujibu.
Ujumbe
wa simu uliotumwa na MTANZANIA ulisomeka hivi: “Mheshimiwa habari za
asubuhi naitwa … ninaomba ufafanuzi wa ushiriki wako katika Uchaguzi wa
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Masaki.
“…kuna taarifa kuwa umeshiriki kuwania uenyekiti wa mtaa na kuangushwa na kijana, je ni kweli?”
Mbene
ni mbunge wa kuteuliwa na Rais Kikwete katika vipindi viwili tofauti.
Kwa mara ya kwanza aliteuliwa kuwa mbunge katika Bunge la tisa na
baadaye aliteuliwa tena na kuwa Naibu Waziri wa Fedha.
Baada
ya kipindi cha miezi kadhaa, katika mabadiliko aliyoyafanya Rais
Kikwete, alimhamisha wizara na kumpeleka kuwa Naibu Waziri Viwanda na
Biashara.
Agosti
24 mwaka huu, Kamati ya Siasa ya CCM mkoani Mbeya, iliagiza Mbene aitwe
kuhojiwa akidaiwa kuhusishwa na vurugu za siasa katika Wilaya ya
Ileje.
Mbene
ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, alikuwa
akilalamikiwa kutumia siasa za kukigawa chama kwa kujenga makundi ndani
ya chama hicho.
Uamuzi
wa kuitwa kwa Mbene uliwekwa wazi na Katibu Mwenezi wa CCM mkoani
Mbeya, Bashiru Madodi, aliyesema uamuzi huo ulifikiwa kwenye vikao vya
kamati za siasa vilivyojadili maadili na nidhamu katika mojawapo ya
wilaya mkoani humo, kati ya Agosti 22 na 23 mwaka huu.
Hivi
sasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kipo katika mchakato wa kura za maoni
kuwapata wagombea wake wataoshiriki katika Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa, Vijiji na Vitongoji unaotarajiwa kufanyika Desemba 14 mwaka huu.
CHANZO: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment