Posted by Williammalecela.com on Tuesday, December 30, 2014
 |
Kamanda wa Polisi Mkoa Mjini Magharibi Msaidizi Kamishna wa Polisi {
ACP } Mkadam Khamis Mkadam alisema Jeshi la Polisi Mkoa huo
linawashikilia watu wawili miongoni mwa majambazi wanaotuhumiwa kuhusika
na uvamizi wa Madaktari Bingwa wa Cuba katika maeneo kati ya Kikwajuni
Wireles na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar {SUZA } mapema jana usiku.
Alisema polisi ilianza uchunguzi mara moja baada ya kupata taarifa ya
kuvamiwa kwa Madaktari hao walionyang’anywa mikoba,vitu pamoja na Fedha zao ambapo mmoja kati yao Profesa Ulpiano alijeruhiwa kwa panga kichwani.
Kamishna Msaidizi wa Polisi { ACP } Mkadam Khamis Mkadam alieleza hayo
wakati Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika
nyumbani kwa Madaktari hao Vuga Mjini Zanzibar kuwafaribi baada ya
kupatwa na mkasa huo.
Kamanda Mkadam alisema Mkoa wa Mjini
umekuwa na matukio ya kuibuka kwa vitendo vinavyoashiria kuichezea amani
baadhi ya wakati jambo ambalo jamii inahusika kwa kiasi kikubwa katika
kushirikiana na Jeshi la Polisi kukabiliana na vitendo hivyo.
Alisema ulinzi ni jukumu la watu wote, hivyo miundo mbinu iliyopo hivi
sasa Duniani ya mitandao ya mawasiliani katika uwekaji wa Kamera za CCTV
inahitajika kutumika kwa lengo la kuwabaini watu wanaojihusisha na
matendo maovu.
Kamanda huo wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi
alizishauri Taasisi za Umma, Binafsi na hata watu wa kawaida
wakakijengea utamaduni wa kutumia mfumo huo mpya ili kuwa na maisha ya
salama.
Akiwapa pole Madaktari hao Bingwa wa Cuba wanaotoa huduma
katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja pamoja na kusomesha Chuo Kikuu cha
Taifa Zanzibar { SUZA } Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Iddi alisema hilo ni tukio la ajabu na la kusikitisha katika visiwa
vya Zanzibar.
Balozi Seif alisema vitendo hivyo viovu
vinavyofanywa na baadhi ya wahuni vimekuwa vikileta sura mbaya kutokana
na sifa ya Zanzibar yenye Utamaduni wa kistaarabu wa kupenda wageni
tokea karne nyingi zilizopita.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
aliwahakikishia Madaktari Bingwa hao wa Cuba kwamba Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kupitia vyombo vyake vya ulinzi inaendelea na
uchunguzi wa kina na wahusika wa vitendo hivyo watapopatikana mkondo wa
sheria utafanya kazi zake dhidi ya wahalifu hao.
Balozi Seif
aliwataka Madaktari hao kuendelea na majukumu yao kama kawaida na
Serikali itakuwa makini katika kuwahakikishia usalama wao pamoja na
wageni wengine wakati wao wote wawapo hapa Nchini.
Wakitoa
shukrani zao kwa faraja hiyo pamoja na juhudi zilizochukuliwa na vyombo
vya ulinzi katika kuwasaka wahalifu waliohusika na tukio hilo Madaktari
hao wa Cuba waliahidi kuendelea kutoa huduma kama kawaida licha ya mkasa
uliowakumba.
Madaktari hao walielezea matumaini yao kwamba
Serikali pamoja na vyombo vyake vya ulinzi vitafanya juhudi za ziada
katika kuona kwamba matukio kama hayo yanadhibitiwa kabisa.
Madaktari hao wanne wa Cuba ni Dr. Barbara, Dr. Daisy Batle, Dr.Katia
wakiwa na Kiongozi wao Profesa Ulpiano walivamiwa ghafla na vijana
walioshuka na mapanga kwenye Gari aina ya Noah wakati wakitokea
Kikwajuni kuelekea nyumbani kwao Vuga.
Othman Khamis Ame Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
|



0 comments:
Post a Comment