Saturday, February 28, 2015

DSC_0113Ofisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) nchini, Al Amin Yusuph, akiwasilisha mada ya mchanganuo wa ufumbi wa changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa mradi wa kijiji cha kidigitali.
Na Mwandishi wetu, Bagamoyo
WADAU mbalimbali wa elimu, afya, Tehama na masuala ya utamaduni na uchumi ambao wamo katika mradi wa kijiji cha dijiti cha Ololosokwan kilichopo wilayani Monduli Arusha wanakutana kwa warsha ya wiki moja ikiwa ni sehemu ya mandalizi ya uwapo wa kijiji hicho nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa Ofisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika la Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) nchini Al Amin Yusuph warsha hiyo imelenga kuangalia changamoto na namna ya kuzitatua ili mradi kuwa na tija kwa wananchi wake.
Yusuph alisema kwamba wadau hao wanapanga mkakati kuangalia vipaumbele na changamoto katika utekelezaji wa mradi huo wa miaka mitatu.
Alisisitiza kwamba kwa kuwa mradi huo utakuwa na mawasiliano ya kisasa, masomo kwa njia ya Tehama, tiba kwa kutumia mtandao wadau wamekusanyika mjini Bagamoyo kuangalia namna bora ya kuufanya mradi huo uwe endelevu hata kama UNESCO na mbia wake Samsung watajiondoa huko mbeleni.

Aliwataja baadhi ya wadau kuwa ni kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Afya na ustawi wa jamii, Samsung, Unesco, wanakijiji wa Ololosokwan, waganga wa jadi wakunga, Taasisi ya elimu na Chuo cha Ufundi cha DIT.
Alisema changamoto ambazo zinaonekana ni lazima ziangaliwe ni pamoja na matumizi ya lugha hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa wengi wa wananchi wa Kimasai hawazungumzi Kiswahili fasaha.
“tunategemea sana Tehama kufanikisha mradi huu, na lugha inayoweza kutumiwa ni Kiswahili, sasa hili ni changamoto ni lazima kuangalia mawasiliano” alisema Yusuph na kuongeza kuwa kuwapo kwa radio ya jamii kutachangia kwa kiasi kikubwa kutoa nafasi ya wananchi wengi kujifunza Kiswahili.
Aidha alisema kwamba mambo mengine ambayo yanaangaliwa katika warsha hiyo ni matumizi ya Tehama (intaneti) na kutoa mafunzo ya namna ya kuhudumia na kufanyia matengenezo mitambo mbalimbali iliyomo katika mradi huo.

0 comments:

Post a Comment