Tuesday, March 3, 2015

Serikali ya Tanzania imetia saini mkataba wa mashirikiano na Serikali ya Denmark wenye thamani ya dola za Marekani milioni 100 kwa ajili ya kusaidia mpango wa awamu ya nne wa sekta ya afya(HSPS IV) kwa kipindi cha miaka mitano ili kuwezesha kila Mtanzania kupata huduma za afya kwa wakati wote.


Mkataba huo, ambao ni msaada kutokaDenmark ulitiwa saini jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,Dk. Donald Mbando, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI)dawati la Afya, Dk. Deo Mtasiwa na Balozi wa nchini,Johnny Flento.
  Akizungumzia kuhusu mkataba huo, Dk. Mbando alisema utawezesha kuongeza uwezo wa upatikanaji wa huduma za afya na kushirikisha sekta binafsi.
  Dk. Mbando alisema alizitaja asasi za kiraia ambazo nazo zilitia saini mkataba huo kuwa ni Sikika, CCBRT, Mariastopers na Muungano wa hospitali binafsi. 
  “Msaada huu umekuja kwa wakati muafaka kwa kuwa tuko katika hatua ya kukamilisha mpango wa awamu wa sekta ya afya wa awamu ya tatu, hivyo utasaidia kutekeleza mpango wa awamu ya nne na Matokeo Makubwa Sasa(BRN) kwenye sekta ya afya,ambapo utaongeza upatikanaji wa rasilimali watu, dawa na vifaa tiba,” alisema Dk. Mbando.
  Aliongeza kuwa utasaidia pia kuongeza jitihada za kupunguza vifo wa watoto na wakina mamawajawazito ambavyo bado ni changamoto. 
  Kwa upande wake Balozi wa Denmark,Flento alisema ushirikiano wa sekta binafsi na Serikali ni muhimu ili kuwezesha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa kila mtu. Pia utasaidia kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika sekta ya afya,zikiwemo za usimamizi wa fedha za umma na upungufu wa rasilimali watu.
  Naye Mkurugenzi wa Sikika Irenei Kiria alisema ushirikishaji wa sekta binafsi katika mkataba huo, utaongeza uwajibikaji, utoaji wa huduma za afya kwa kiwango kinachotakiwa na kuhakikisha rasilimali zinatumika ipasavyo.


0 comments:

Post a Comment