Wednesday, March 4, 2015

.


Mheshimiwa Zitto

Mheshimiwa Ngeleja
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi Mlalamikiwa naomba kutoa maelezo ya utetezi wangu kama ifuatavyo:


Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakanusha tuhuma nilizotuhumiwa na Mlalamikaji kwamba mimi Mlalamikiwa niliomba fadhila za kiuchumi kutoka kwa James Rugemalira kinyume na fungu la 6(f) la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambalo linamzuia kiongozi wa Umma kuomba au kupokea- fadhila za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi Mlalamikiwa napenda kulieleza Baraza lako kwamba sijawahi kuomba wala kupokea fadhila za kiuchumi kutoka kwa James Rugemalira kinyume na fungu la 6 (f) la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

ISIPOKUWA- kwamba mimi Mlalamikiwa, nikiwa Mbunge wa Jimbo la Sengerema, kwa nyakati mbalimbali kama wafanyavyo wabunge wenzangu wengine, nimekuwa nikiomba misaada mbalimbali kutoka kwa wafadhili na marafiki mbalimbali (watu binafsi na taasisi za Umma au kampuni binafsi) ili kuniwezesha kutekeleza mambo mbalimbali yanayonikabiri kama Mbunge jimboni kwangu- na nje ya jimbo langu.

Baadhi ya matumizi ya misaada tunayoipata wabunge kutoka kwa wafadhili mbalimbali ni pamoja na michango au matoleo kwenye shughuli mbalimbali za kijamii mfano harambee za makanisa na misikiti (jimboni na nje ya jimbo),- misaada kwenye ofisi zetu za vyama vya siasa majimboni, kuchangia vikundi mbalimbali vya wajasiriamali jimboni na nje ya jimbo, uwezeshaji wa vikundi mbalimbali na michango kwenye miradi ya maendeleo kwa wananchi ambayo haikutengewa fedha kutoka kwenye bajeti za Serikali Kuu, Halmashauri au Mfuko wa Jimbo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, msaada nilioupata kutoka kwa James Rugemalira hautofautiani na misaada wanayopewa wabunge wenzangu kutoka kwa marafiki zao na wafadhili mbalimbali. Jambo hili la wabunge kupewa misaada siyo geni, na ndiyo maana hata Bunge kama taasisi limekuwa likibariki misaada hiyo wakati hoja za kuhoji misaada wapatayo wabunge zinapojitokeza. Baadhi ya wafadhili ambao wamekuwa wakitoa misaada kwa wabunge mbalimbali ni pamoja na Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni za IPP, Bakhressa, Manji,Subhash Patel, NSSF,PSPF,PPF,LAPF,NHIF, CRDB, NMB,NBC,NHC, James Rugemalira, VIP Engineering and Marketing Ltd, IPTL, n.k.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nina mifano michache na vielelezo vya ushahidi kuhusu namna ambavyo wabunge tumekuwa tukipewa misaada na Bunge kubariki misaada hiyo ilipohojiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano na kielelezo cha kwanza ni wakati Taarifa / Hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa mwaka wa fedha 2014/2015 ilipohoji uhalali wa Mhe Zitto Zuberi Kabwe (Mb) na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha za Serikali (PAC) na washirika wake, kupata msaada wa jumla ya shilingi 119,930,000/= kutoka katika taasisi za Umma, yaani TANAPA (Shs. 12,200,000/=) na NSSF (Shs.79,027,000/=), katika kipindi cha miezi mitatu- tu kati ya tarehe 10 Desemba, 2012 na 4 Machi, 2013.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hoja ya tuhuma hizi kuwasilishwa rasmi Bungeni, Bunge halikumwajibisha Mhe. Zitto Kabwe kwa tuhuma hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naliomba Baraza lako likubali kupokea nakala ya sehemu ya Hotuba/Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa mwaka wa fedha 2014/2015 yenye kubeba tuhuma hizo kwa Mhe. Zitto Kabwe, ikiwa ni sehemu ya maelezo ya utetezi wangu. Hotuba hiyo inasomeka kama Kiambatisho “A”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano na kielelezo cha pili ni tuhuma ambazo Mhe. Livingstone Lusinde, Mbunge wa Jimbo la Mtera, alipomtuhumu Mhe Zitto Kabwe (Mb) kupokea msaada wa jumla ya zaidi ya shilingi milioni 30 kutoka kwa kampuni ya Pan Africa Power Solutions (T) Limited maarufu kama “PAP” kwenye kipindi cha kati ya tarehe 28/3/2014 na tarehe 08/04/2014, kwa matumizi yake binafsi wakati akijua kwamba kampuni ya PAP inahusishwa na kadhia ya ESCROW hapa nchini. Tuhuma hizi zilitolewa dhidi ya- Mhe Zitto katikati ya mjadala wa hoja ya ESCROW Bungeni, Dodoma kwenye mkutano wa 16 na 17 uliofanyika mwezi Novemba, 2014.

Mhe. Zitto Kabwe alipokea fedha kutok PAP kama ifuatavyo: tarehe 28/03/2014 (Tshs 6,000,000/=), tarehe 03/04/2014 (USD 5,000/=), tarehe 08/04/2014 (Tshs 10,000,000/=) na tarehe 08/04/2014 (Tshs 10,000,000/=).

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na tuhuma na vielelezo hivi ambavyo Mhe Lusinde (Mb) aliviwasilisha mezani kwa Mhe Spika, kwa hatua zaidi, Bunge halikumchukulia hatua yoyote Mhe. Zitto Kabwe kuhusu tuhuma hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana hata pale Mhe Zitto mwenyewe alipoliomba Bunge limpeleke kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge inayoongozwa na Mhe. Brig. Jenerali Ngwilizi (Mb) ili kuchunguza tuhuma zilizotolewa na Mhe. Lusinde dhidi yake kwa kusema kwamba:

Nanukuu “Mheshimiwa Mwandosya aliomba nisiseme baadhi ya mambo, nakubali sana kwani ni mzee wangu, lakini naomba tu kitu kimoja. Wakati mwingine tuhuma hizi zikiachiwa bila kufanyiwa uchunguzi watu wanaziamini, watu wanaziamini! Mheshimiwa Spika, ni vizuri kwa sababu baadhi ya tuhuma zimesemwa ndani ya Bunge na Bunge lina vyombo vyake, tuna kamati ya Mheshimiwa Ngwilizi, mimi I want to subject myself kwenye kamati ya Maadili ya Bunge ili ifanye uchunguzi kwa tuhuma ambazo Mheshimiwa Lusinde alizizungumza, Mheshimiwa Hawa Ghasia akazirudia leo kwa juu juu, sijui alikuwa ananionea aibu mdogo wake na Mheshimiwa Nchambi amezizungumza. Naomba ziende kwenye Kamati ya Maadili ” bado Bunge halikuchukua hatua yoyote kumwajibisha Mhe Zitto Kabwe kwa tuhumu za kupokea msaada huo wa zaidi ya shilingi milioni 30 kutoka kampuni ya PAP inayohusishwa na kadhia ya ESCROW.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Baraza lako lipokee nakala ya sehemu ya kumbukumbu rasmi za Bunge (Hansard) kuhusu maelezo ya Mhe Zitto Kabwe (Mb) wakati anajibu tuhuma zilizoelekezwa kwake na baadhi ya waheshimiwa wabunge pamoja na nakala za vielelezo kuhusu namna Mhe Zitto Kabwe alivyopokea fedha kutoka kwa kampuni ya PAP. Naomba nyaraka na vielelezo hivi vipokelewe kama sehemu ya maelezo ya utetezi wangu. Nyaraka na vielelezo hivi kwa pamoja vinasomeka kama Viambatisho “B”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na maelezo yangu hapo juu naendelea kusisitiza kwamba msaada nilioupata kutoka kwa ndugu James Rugemalira haukuwa fadhila za kiuchumi bali ulikuwa ni msaada wa kawaida kama wapatavyo wabunge wengine kutoka kwa marafiki na wafadhili mbalimbali ikiwa ni ukarimu au fadhila ya kawaida kutoka kwa wafadhili hao, ili kuwasaidia wabunge kutekeleza majukumu yao ya kibunge ndani na nje ya majimbo yao. Misaada hiyo husaidia juhudi za serikali na wananchi kwa ujumla kutatua kero za wananchi na kuchangia shughuli za kijamii hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mnamo tarehe 31/12/2014 iliniandikia barua ya kunitaka kulipa kodi ya mapato (30%) kutoka kwenye msaada wa shilingi 40,425,000/= nilioupokea tarehe 12/02/2014 kutoka kwa James Rugemalira kupitia Akaunti yake ya VIP TZS TRUST.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TRA waliutafsiri msaada niliopata kutoka kwa James Rugemalira kama mapato ya kawaida yanayostahili kutozwa kodi ya asilimia 30, hivyo wakaniagiza nilipe kiasi cha shilingi 13,138,125/= kama kodi ya mapato kutoka kwenye msaada huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 15/01/2015 mimi Mlalamikiwa nililipa kodi ya mapato (30%) kama nilivyoagizwa na TRA. Nilitii maelezo ya TRA pamoja na kwamba sikuwa na uhakika kama aliyenipa msaada huo ndugu James Rugemalira hakuwa amelipia kodi stahiki ya fungu hilo la fedha alizozipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 15/01/2015 mimi Mlalamikiwa nililipa kodi ya mapato (30%) kama nilivyoagizwa na TRA. Nilitii maelezo ya TRA pamoja na kwamba sikuwa na uhakika kama aliyenipa msaada huo ndugu James Rugemalira hakuwa amelipia kodi stahiki fungu hilo la fedha alizonipatia msaada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaliomba Baraza lako lizingatie kwamba baada ya msaada nilioupata kuulipia kodi ya shilingi 13,138,125/= kiasi kilichobaki ambacho ndiyo kiini cha suala hili ni shilingi 27,286,875/=.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaliomba Baraza lako lipokee nakala ya barua--- niliyoandikiwa na TRA na nakala ya malipo niliyofanya kuhusu kadirio la kodi ya 30% kwenye msaada nilioupata, ikiwa ni sehemu ya maelezo na utetezi wangu. Nyaraka na vielelezo hivi kwa pamoja nimeviambatisha kama Viambatisho “D”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwa mara nyingine tena kulithibitishia Baraza lako tukufu kwamba mimi Mlalamikiwa mnamo tarehe 24/12/2014 niliwasilisha “TAMKO LA VIONGOZI WA UMMA KUHUSU RASILIMALI NA MADENI” kwa Kamishna wa Maadili kwa mwaka ulioishia tarehe 31 Desemba, 2014 linaloonesha pamoja na mambo mengine, msaada wa shilingi 40,425,000/= nilioupokea kutoka kwa James Rugemalira, kupitia Akaunti yake ya VIP TZS TRUST, iliyoko Benki ya Mkombozi, Tawi la St. Joseph, ikiwa ni utekelezaji wa vifungu vya 6 (e) na 12 (2) vya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

0 comments:

Post a Comment