Meli ya kivita ya Marekani USS Theodore Roosevelt.
Jeshi la majini la Marekani limepeleka meli yake ya kivita ya USS
Theodore Roosevelt ikisindikizwa na meli yenye kubeba makombora ya USS
Normandy kuhakikisha kile ilichosema njia muhimu za bahari katika eneo
hilo zinabakia kuwa wazi na salama na kufanya idadi ya meli za kivita za
Marekani katika eneo hili kufikia tisa.
Kwa mujibu wa afisa mwandamizi wa ulinzi wa Marekani ambaye amezungumza
na shirika la habari la Ufaransa AFP msafara wa meli za Iran unajumuisha
meli tisa zikiwemo mashua mbili za doria lakini mahala hasa unakoelekea
msafara huo hakujulikani.
Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani Kanali Steven Warren amekanusha
repoti kwamba meli za Marekani zimeagizwa kuzuwiya meli za Iran zenye
kuwapelekea silaha Wahouthi.
Meli za Iran yumkini zikazuiliwa
Marekani imesema haishiriki moja kwa moja katika mashambulizi
ya anga ya ushirika unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya waasi wa Kishia
wa jamii ya Wahouthi nchini Yemen lakini inasaidia kwa kutowa taarifa
za kijasusi na msaada wa vifaa.
Maafisa kadhaa wa serikali ya Marekani wamedokeza kwamba yumkini Saudi
Arabia,Misri na washirika wao wengine ndio zitazozizuwiya meli hizo za
Iran itakapolazimika.
Inasemekana kwamba msafara huo wa meli za Iran tayari umevuka mlango
bahari wa Hormuz kuondoka Ghuba na hivi sasa unaelekea upande wa
magharibi ambapo inaaminika kuwa Yemen.
Upatanishi wa Iran wagonga ukuta
Rais Hassan Rouhani wa Iran leo ametowa wito wa kusitishwa mara
moja kwa mapigano nchini Yemen na kukomeshwa kwa mashambulizi ya anga
ya ushirika unaongozwa na Saudi Arabia ili kuwezesha kufanyika kwa
mazungumzo kati ya pande zinazohasimiana nchini humo.
Rais Rouhani amesema"Tunataraji kwamba kila mtu atazinduka na tunatumai
pendekezo la Iran litatekelezwa.Ni kusitishwa kwa mapigano mara
moja,kushughulikia hali ya majeruhi na kufanya mkutano baina ya Wayemen
kutafuta suluhisho na hatimae kuunda serikali yenye kushirikisha makundi
na makabila yote.Tunaamini kwamba huu ni ufumbuzi ambao unaweza
kutatuwa masahibu ya Yemen."
Rais Rouhani ametowa kauli hiyo muda fupi kabla ya kuondoka katika
uwanja wa ndege wa Mehrabad mjini Tehran kuelekea Indonesia kuhudhuria
mkutano wa Kilele wa Asia na Afrika.
Dhima ya Iran
Unyeti wa dhima ya Iran katika mzozo huo umezidi kujitokeza leo
hii wakati serikali ya Yemen ilipokataa pendekezo la Iran la
kusuluhisha mzozo huo.Waziri wa mambo ya je wa Yemen Riyadh Yassin
amesema juhudi zozote zile za upatanishi kutoka Iran hazikubaliki kwa
sababu Iran inahusika katika mzozo huo wa Yemen.
Amesema Wahouthi na vikosi vya Rais wa zamani Ali Abdullah Saleh lazima
waondoke katika miji na vijiji vyote vya Yemen ikiwemo Sanaa na Aden na
kurudi katika ngome yao kuu ya kaskazini ya mji wa Saada wakiwa kama
raia na kusalimisha silaha zao.
Nchini Yemen kwenyewe mzozo huo hauonyeshi dalili ya kupowa wakati idadi
ya vifo vya raia waliouwawa katika mashambulizi ya anga yanayongozwa na
Saudi Arabia dhidi ya ghala la makombora mjini Sanaa hapo jana
ikiongezeka na kufikia 38 huku watu 532 wakiwa wamejeruhiwa.

0 comments:
Post a Comment