Posted by Williammalecela.com on Thursday, June 11, 2015
Mpendazoe: Mwalimu aliwauliza Wajumbe wa NEC maswali, kwamba wao ni wahuni au ni Viongozi wa CCM?
Lowassa, nionyeshe marafiki zako na mimi nitakuambia wewe ni nani
SIKU Edward Lowassa alipotangaza rasmi kugombea urais wa Tanzania
nilibahatika kumsikiliza na nilishuhudia umati mkubwa wa watu
waliofurika kumsikiliza. Ni kweli yalikuwa ni mafuriko ya watu.
Sijui kama walikwenda kwa hiari yao au walilipwa ili waende kwenye
mkutano huo. Hilo sijui wala si ajenda yangu kwenye makala hii. Jambo
ambalo ninataka wasomaji wa makala hii walizingatie ni aina ya watu
waliokuwepo kwenye mafuriko hayo, kwani ndege wenye manyoa yanayofanana
ndiyo wanaoruka pamoja.
Tumeona utawala wa Rais Jakaya Kikwete. Rais aliyeingia kwa hamasa kubwa
akibeba matumaini na matamanio ya mamilioni ya Watanzania . Utawala wa
Kikwete ulikuja na kila ahadi za kurudisha utukufu wa Taifa. Lakini
Kikwete atakapoondoka mwezi wa kumi mwaka huu, Je atakuwa amefanikiwa
kurudisha heshima ya taifa letu? Na wakati wa mchakato wa kugombea
urais, Watanzania wengi walimuunga mkono Kikwete hadi baadhi ya viongozi
wa dini walifikia kusema alikuwa chaguo la Mungu. Walisema sauti ya
wengi ni sauti ya Mungu!
Leo ukisema kwamba Kikwete alikuwa chaguo la Mungu, sijui kama
Watanzania wengi watakubaliana na wewe. Sijui. Rais Kikwete alitengeneza
mtandao uliomsaidia kuingia Ikulu.Lowassa ametengeneza mtandao
unaomsaidia aingie Ikulu.
Isipokuwa katika maelezo yake Lowassa, amejitahidi kujitofautisha na
Kikwete na hasa aliposema suala la urafiki wao lisihusishwe katika azma
yake ya kuomba nafasi ya kuwa rais. Anawataka Watanzania wampime kama
yeye binafsi na wasilihusishe suala la urafiki wao.
Sijui kwa nini kwa sasa Lowassa anajitenga na Kikwete. Lakini
Watanzania wanakumbuka Lowassa aliwahi kusema urafiki wao si wa kukutana
barabarani.
Kwa kuwa Lowassa anaomba nafasi ya nyeti ya urais ni muhimu Watanzania
wajiridhishe bila shaka yoyote Lowassa ni nani. Na je anaweza
kukabiliana na changamoto zinazolikabili Taifa letu hasa ufisadi, rushwa
na kuporomoka kwa maadili.
Mwalimu Nyerere katika kitabu chake, Nyufa, cha mwaka 1995, alisema:
“Sasa Tanzania inanuka rushwa… tunataka kiongozi anayejua hivyo, ambaye
atasema rushwa kwangu mwiko, mwaminifu kabisa kabisa, hawezi kugusa
rushwa na… watoa rushwa watamjua hivyo. Lakini hatutaki aishie hapo tu,
maana haitoshi wewe mwenyewe uwe mwaminifu…Unaweza ukawa wewe mwaminifu
kabisa kabisa, lakini una shinikizo la ndugu zako, jamaa zako na
marafiki zako.“Kwa hiyo si inatosha wewe kuwa mwaminifu tu, lakini uwe
na uwezo wa kuwaambia jamaa zako kwa kauli ambayo wataiheshimu na
hawatarudia tena.
Unawaambia jamaa na rafiki zako kwa dhati kabisa… Ikulu ni mahali
patakatifu, mimi sikuchaguliwa na wananchi wa Tanzania kuja kupageuza
pango la walanguzi na hakuna serikali yoyote duniani inayoongozwa bila
miiko”.
Zipo taarifa zinazoeleza kwamba fedha nyingi zimetumika katika kufanya
maandalizi ya mkutano wa Arusha uliosababisha mafuriko ya watu. Aidha,
ndugu Lowassa mara kadhaa amekiri kwamba marafiki zake ndio
wanaomchangia kufanikisha safari yake ya matumaini.
Hivyo fedha nyingi anazochangia kwenye harambee kwenye misikiti na
makanisani nyingine anatoa yeye na nyingine anachangiwa na hawa marafiki
zake ambao wengi wao ni wafanya biashara matajiri na wengi wao ni wale
waliotajwa kwenye kashfa za ufisadi na tuhuma mbalimbali.
Hawa marafiki zake Lowassa wamesaidia sana kumjua Lowassa ni nani, kwani
wahenga walisema, “Nionyeshe marafiki zako na mimi nitakuambia wewe ni
nani au wewe una tabia gani”.
Hawa marafiki zake na Lowassa wanaweza kuwasababisha Watanzania wamtilie
shaka Lowassa kama anaweza kuwa safi na kustahili kupewa dhamana ya
kuongoza nchi. Naomba niwakumbushe kauli ya Mwalimu Nyerere kuhusu mmoja
wa wagombea urais kwenye NEC Dodoma mwaka 1995, “Hapa hatuchagui mtu
maarufu, tunachagua mtu safi na huyu si safi”. “Kama unapenda sura yake
basi nenda kanywe nae chai. Wengine mnasema aaah ni tuhuma tu.
Hapa mnasema ni tuhuma tuhuma tu! Lakini mtakumbuka mke wa Kaisari
alipotuhumiwa kwa ugoni, Kaisari akaagiza uchunguzi ufanyike”.
“Uchunguzi ukafanyika na ikabainika kwamba si kweli. Lakini Kaisari bado
akamwacha, akasema mke wa Kaisari hapaswi hata kutuhumiwa. Na sisi hapa
mgombea wetu hapaswi hata kutuhumiwa wakati wapo wengine wasafi ambao
hawana tuhuma.“Kama mtamteua huyu mimi sitapiga kampeni. Siko tayari
kumsafisha mtu matope halafu nimwombee kura.
Hapana kabisa . Huyu najua si msafi na nchi nzima inajua si msafi. Hafai kuwa mgombea wetu”.
Aidha, mtakumbuka pia kuwa mwaka 1995, kundi la Vijana lilimtaka Lowassa
ateuliwe kugombea urais wa Tanzania. Hata hivyo, ilitolewa kauli kuwa
Lowassa alikuwa na tuhuma za rushwa, kujilimbikizia mali na kupungukiwa
na maadili, kinyume na katiba ya CCM na kanuni za chama hicho.
Kamati Kuu ilipopeleka mapendekezo ya kutompendekeza kugombea urais,
Lowassa alitetewa kwa makelele, kihuni, bila kufuata taratibu za kikao
cha NEC Dodoma. Kundi moja lilikuwa limejiandaa kumpitisha kwa hoja ya
nguvu na si kwa nguvu ya hoja.
Waliyatetea maelezo ya Kamati Kuu, lakini waliyakataa yale ya nyongeza
aliyoyatoa Mwenyekiti Ali Hassan Mwinyi (Rais wa wakati huo) ambaye
alielezea tuhuma hizo zilizokuwa zinamkabili Lowassa. Hivyo, naomba
kusisitiza kwamba Lowassa hakuwa chaguo la CCM katika uchaguzi wa mwaka
1995. Katika kikao hicho cha Kamati Kuu, Mwalimu Nyerere aliamua
kusaidia kikao kwa kutoa maelezo ya nyongeza.
Aliwauliza wajumbe wa NEC maswali, kwamba wao ni wahuni au ni viongozi
wa CCM? Ikiwa wao ni viongozi wa CCM, je, hivyo ndivyo wanavyopaswa
kumtafuta mgombea wa urais, kwa makelele?
Kama Watanzania wangewaona walivyokuwa wanafanya katika kikao hicho, je,
wangeamini kuwa wao ni viongozi kweli? (Wajumbe walibaki kimya). Kisha
Mwalimu aliendelea kusisitiza maelezo aliyoyatoa Mwenyekiti Ali Hassan
Mwinyi akisema: “Mwinyi amemstahi sana Lowassa”.
Hakuwaambia wajumbe wa NEC baadhi ya tuhuma mbaya kabisa kuhusu Lowassa.
Ikiwa NEC inachoombwa ni kuchagua kati ya wenye tuhuma za rushwa
kuchaguliwa kwa nafasi ya urais, na wale wasioitaka, basi huu ni wakati
muafaka kwao kuipeleka hoja hiyo mbele ya Watanzania waiamue kwa kuwa
ndani ya NEC hakuna mwenye uwezo wa kumfukuza mwenzie, wote ni wajumbe
sawa kwa mujibu wa katiba ya CCM”.
Hatimaye kikao cha NEC kiliondoa jina la Lowassa, kikawateua Benjamin
William Mkapa, Cleopa David Msuya na Jakaya Mrisho Kikwete kuwa
wagombea. Majina yaoyaliwasilishwa kwenye Mkutano Mkuu ambao ndio
uliopaswa kumchagua miongoni mwao kuwa mgombea
Mwandishi Fred Mpendazoe
Toleo la 409: Jun 10 2015
0 comments:
Post a Comment