MAJINA MATANO NGOMA NZITO: Mizengwe yatawala hadi usiku wa manane Kamati Kuu kufyeka waliodaiwa kuanza kampeni mapema.
Taarifa kutoka chanzo kimoja cha uhakika ndani ya CCM kilieleza
kwamba kulikuwa na mizengwe ya kuwapo kwa barua kutoka kwa vigogo wenye
ushawishi mkubwa ndani ya chama hicho kushinikiza kuondolewa kwa baadhi
ya wagombea kwa madai kuwa walianza kampeni mapema na hivyo kuhatarisha
hatma ya ushiriki wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika
Oktoba 25, mwaka huu.
Hali hiyo inaelezwa kwamba ndiyo kigezo ambacho wajumbe wa Kamati
Kuu waliokutana kwenye ofisi moja nyeti mjini Dodoma waliendelea
kuishikilia kwa lengo la kuwaondoa wagombea wenye dosari hizo.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, baadhi ya wajumbe walikuwa kwenye
mjadala mkali kutokana na hofu kuwa wakiteuliwa watia nia walioanza
kampeni mapema watakiweka chama chao katika hatari ya kuwa na mgombea
aliyepoteza sifa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi mkuu zinazosimamiwa na
Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Hadi kufikia mishale ya saa 7:31 usiku hakukuwa na taarifa zozote
za matokeo ya majina matano yaliyopitishwa na Kamati Kuu kati ya 38 ya
waliorejesha fomu ili yapelekwe kwenye kikao cha Nec kwa mchujo zaidi
ili wabaki wanafainali watatu.
USIRI MKUBWA WATAWALA
Kama ilivyotarajiwa, kikao hicho cha Kamati Kuu, kilifanyika kwa
usiri mkubwa kiasi cha kuwafanya waandishi wa habari kuwa na wakati
mgumu kupata taarifa zilizokuwa zikiendelea ndani yake.
Awali kabla ya Kamati Kuu ya chama hicho kukutana kwa kazi hiyo,
siri nzito ilitenda juu ya maamuzi yaliyofanywa na kikao cha Kamati ya
Usalama na Maadili ya CCM kilichoketi juzi usiku chini ya Mwenyekiti wa
CCM Taifa, Rais Kikwete. Kikao hicho cha Kamati ya Usalama na Maadili ya
CCM, kilikaa kupitia mafaili ya wagombea 38, waliorejesha fomu za
kuomba kuteuliwa na chama hicho kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Kabla ya kikao cha Kamati Kuu, Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi
na Uenezi, Nape Nnauye, alipotafutwa na NIPASHE jana kwa njia ya simu
kutoa ufafanuzi iwapo kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili kilifanyika
kama ilivyokuwa imepangwa awali, alisema: “Nianze na hili la Kamati Kuu
(CC), mimi pia sijui kinafanyika wapi na saa ngapi. Halafu hata hicho
kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili unachoniuliza hapa;
hakikufanyika.”
Kabla ya Rais Kikwete kuongoza Kikao cha Kamati Kuu kwa ajili ya
kufyeka majina 33 ya wagombea wanaoomba kuteuliwa kuwania kiti cha urais
na kubaki matano; alifanya kazi kubwa mbili katika siku ya jana,
ikiwamo kuzindua jengo jipya na la kisasa la CCM, maarufu kama Dodoma
Convention Centre na baadaye jioni kwenda kulivunja Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Jumla ya makada 42 wa CCM walichukua fomu kwa ajili kuomba ridhaa kwa chama hicho kiwateue kuwania urais.
Hata hivyo, kati hao 42, makada 38 ndiyo waliorejesha fomu huku wanne `wakiingia mitini’ na fomu hizo.
NIPASHE


0 comments:
Post a Comment