Posted by Williammalecela.com on Thursday, August 27, 2015
Lowassa, anguko la upinzani nchini na hadithi ya bora shetani nimjuaye kuliko malaika nisiyemjua!
Edward Lowassa, Anguko la Upinzani Nchini Na Hadithi ya Bora Shetani Nimjuaye Kuliko Malaika Nisiyemjua!
Na Dkt. Hamisi Kigwangalla
Raia Mwema Agosti 26, 2015.
Nimekuwa na siku nyingi kidogo sijaandika. Leo nikiwa Arusha nikitokea
msibani Usangi kumzika Mzee wetu na muasisi wa TANU na CCM, Mzee Peter
Kisumo, nilikutana na marafiki zangu wa UKAWA na tukataniana kidogo; na
hapo nikasikia matumaini waliyokuwa nayo, si ya kushinda uchaguzi bali
ya kukidhoofisha chama changu, Chama Cha Mapinduzi, mmojawapo alisema:
‘baada ya Oktoba CCM na uwanja wa siasa hautabaki sawa na leo…CCM
haitokuwa imara na salama tena.’
Mazungumzo yale yalinifikirisha. Nikafanya tafakuri tunduizi. Nikaamua kuweka mawazo yangu kwenye rekodi.
Kwa hakika ushindi kwa CCM mwaka 2015 kwenye uchaguzi mkuu kwa nafasi za
Urais, wabunge na madiwani uko wazi kabisa. CCM itapata ushindi wa
kishindo. Kwa nini? Nitafafanua kwa ufupi tu hapa.
Sababu kubwa za kwa nini CCM itashinda mwaka huu ni zifuatazo; kwanza,
CCM ni chama ambacho kimejengwa kwenye misingi na itikadi, na kina
wanachama wengi zaidi wanaoamini kwenye itikadi na misingi hiyo kuliko
wale wachache wanaokiuka, mfano mzuri ni wale wanaofanana na Ndg. Edward
Lowassa ambaye aliondolewa kwenye kinyang’anyiro cha Urais bila maelezo
ya kina, japokuwa wengi wa wachambuzi wa mambo ya kisiasa walibaki
wakisema kwa kiasi kikubwa inawezekana ni historia yake ya kuhusika
kwenye moja ya skendo kubwa kabisa za ufisadi kuwahi kutokea nchini,
maarufu kama ‘kashfa ya Richmond’. Kashfa hii ilipelekea kujiuzulu kwake
nafasi ya uongozi wa Waziri Mkuu.
Pili, CCM ndicho chama pekee chenye muundo thabiti wa kitaasisi –
kutokea kwenye nyaraka mbalimbali zinazoeleweka, muundo wa utumishi,
watumishi na ofisi, muundo wa vikao na ratiba zake, sera, itikadi, vifaa
na majengo, na vitega uchumi vinavyoendeshwa kwa mfumo unaoeleweka,
ukilinganisha na vyama vya upinzani vinavyoendeshwa kwa matukio – ni
tukio moja baada ya jingine, hakuna mfumo wa muundo wa kitaasisi
uliosimama na unaoeleweka. Vyama vingi vya upinzani vinajaribu kuanza
harakati za kuunda mfumo na muundo wa kitaasisi lakini havijafika
popote.
Tatu, CCM ni chama chenye wanachama wengi kuliko vyote; kwa mtaji wa
wanachama zaidi ya milioni saba, ukiongeza na wapenzi, washabiki na watu
wanaoamini tu kwenye uwepo wa dola imara inayotokana na CCM, kwa hakika
ushindi kwa CCM ni dhahiri. Namba zina sifa moja kubwa, kuwa huwa
hazisemi uongo.
Nne, CCM itashinda mwaka huu sababu imefanya kazi nyingi na zinaonekana. Sintozitaja kwenye makala hii.
Tano, CCM inafanya mabadiliko ya uongozi, sera, mikakati yake ya
kuendesha shughuli zake na ina falsafa ya ‘kujikosoa na kukosoana’ na
inakubali kujirekebisha ama kurekebishwa. Tofauti na vyama vingi vya
upinzani, ambavyo toka vianzishwe, baadhi yavyo, mpaka leo hii
havijawahi kufanya mabadiliko kwenye sera, muundo na hata sura za
viongozi wake, na badala yake vinaongozwa na familia ama watu wa kanda
ama kabila fulani. Ukitaka kubadilisha sura za viongozi utakumbana na
hasira za waasisi hao wenye vyama hivyo.
Sita, ngome za CCM hazijatikiswa hata kidogo na haziwezi kuyumba ndani
ya miezi hii miwili ya kampeni. Ushindi kwenye serikali za mitaa wa
takribani asilimia 80 ni kipimo tosha kuwa bado CCM ni chama
kilichojikita mpaka kwenye nyumba kumi za kila mtaa/kitongoji, na kwamba
bado kinapendwa na kuaminiwa na watanzania walio wengi.
Saba, kitendo cha UKAWA kuwa tayari kumpokea na kumteua Ndg. Lowassa
kuwa mgombea wao ni pigo kubwa kwao; kwanza ni kiongozi mbabe na
asiyeshaurika, hawezi kukubali kuendeshwa na taratibu za vyama hivyo –
anajiamini yeye ni ‘taasisi’, maarufu na ana timu ya kumfanyia kazi,
tayari tunavyoongea amekwisha wakatisha tamaa wenzake aliowakuta huko,
baada ya kuvijenga vyama vyao kwa jasho na damu kwa miaka zaidi ya 20,
ameingia yeye tu na kateuliwa kuwa mgombea wao, na tayari ameanza
kuzitenga timu za kampeni alizozikuta huko na mifumo ya uongozi
aliyoikuta huko na kuanza kutumia makundi yake ya Urais aliyotoka nayo
anakokujua.
Nane, kuna hiki kitu wataalamu wa mambo ya siasa wanaita ‘incumbency
advantage’, yaani ‘faida ya kuwepo madarakani’. Hii peke yake,
kisaikolojia, inaiweka CCM juu ya vyama vingine hata kabla hatujaanza
kampeni.
Tisa, kwenda kwa Ndg. Lowassa na hatimaye kuteuliwa kupeperusha bendera
ya UKAWA kunafanya kambi ya upinzani, iliyoungana, kwa mara ya kwanza
kuwa kwenye upande wa kujitetea (defensive side) muda wote, nafasi
ambayo hawajazoea kucheza kwenye mechi hizi, badala ya ile ya
kushambulia (offensive), ambayo wameizoea. Pia kwenda kwake UKAWA na wao
kumkubali kunajenga mazingira ya kuwafanya wapinzani waonekane ni wenye
tamaa ya kushika dola kwa nguvu zote hata kama ni kwa kuchukua makapi;
kwamba, wanataka kwenda kwenye pepo ya mwenyezi Mungu hata kama ni kwa
kupitia kwa shetani!
Maana kumchukua mtu kama Ndg. Edward Lowassa kuwa mgombea wao, ambaye
walitumia muda mwingi na nguvu zao zote kumchafua, na ambaye wanapaswa
wamshukuru kwa kuwapa umaarufu na heshima nchini – kipindi wakimchafua,
kunaondoa imani ya wananchi juu ya nguvu ya kimaadili (moral authority)
ya wao kukemea ufisadi, na kunazua maswali ya uhalali wao kisiasa
(political legitimacy) na maswali ya thamani yao kiitikadi na kimaadili
(ideological values and integrity): kwamba, kama wiki tatu zilizopita
alipokuwa akigombea kupitia CCM alikuwa shetani, na leo anagombea
kupitia UKAWA amekuwa malaika, kwamba alikuwa shetani kwa miaka 8, na
leo amegeuka malaika kwa kuingia UKAWA.
Kumi, Chama Cha Mapinduzi, kimeteua mgombea mzuri wa Urais. Ndg. John
Pombe Magufuli anamuacha mbali Ndg. Edward Lowassa kwa sifa za
kimaadili, mwonekano wa kiutendaji, imani ya wapiga kura kwenye uwezo wa
kutekeleza ahadi atakazotoa, uwezo wa kuhutubia, uwezo wa kiutendaji,
na rekodi ya mafanikio katika utendaji, uadilifu, elimu na hata uwezo wa
kufanya kampeni na kujieleza.
Kumi na Moja, kwenda kwa Ndg. Edward Lowassa UKAWA kumefanya watu
wanaoamini kwenye mabadiliko ya kweli kutokea nje waone kama
wamesalitiwa maana Ndg. Lowassa si mwanamabadiliko, ni mtu wa mfumo wa
kizamani (status-quo), lakini pia kumefanya wanasiasa walioupa upinzani
nguvu na umaarufu kidogo walionao leo, ni kama hawajui la kusema wala la
kufanya.
Ndg. Wilibrod Slaa – hatujui kama amejiuzulu wadhifa wake wa Katibu Mkuu
wa CHADEMA na kama atarejea kwenye majukwaa kumsafisha Ndg. Lowassa ama
ameamua kukaa kimya kabisa – yote ni machungu kwake, amsafishe ili
avunje alichokijenga toka mwaka 2007 na astaafu kwa aibu? Na watanzania
wamuone ni mtu asiyeamini kwenye chochote kile, ama anyamaze kimya,
athibitishe kuwa aliyoyasema kwa kipindi chote hicho ni ya kweli, na
kwamba wenzake ni walafi wa madaraka tu.
Profesa Ibrahim Lipumba, aliyeamua kujiuzuru wadhifa wake wa Mwenyekiti
wa CUF kufuatia ujio wa Ndg. Lowassa amesema hakubaliani na uamuzi huu
wa UKAWA.
Kwa hakika kuna makundi makubwa yaliyodumu kwenye ufuasi wa wanamageuzi
hawa wakongwe kwa muda mrefu watakubaliana nao na hawatounga mkono
UKAWA.
Kumi na Mbili, watanzania watachagua CCM kwa sababu, kwa wale
wanamabadiliko walioamini kwenye mabadiliko kutokea nje ya mfumo
hawatoona jipya linalokuja na UKAWA, wataona hakuna tofauti kati ya CCM
na UKAWA na kwamba wataona bora hata ya CCM imekataa kwa vitendo, pamoja
na vitisho vya ‘mafuriko ya kuigiza ya Ndg. Lowassa’, kwa kumkata jina
na hatimaye kumuondoa kwenye mbio za Urais, kwa tuhuma za ufisadi
uliokubuhu. CCM wamefanya hivyo bila kupepesa macho. Wametoa uongozi kwa
nchi, wameonesha kuwa kuna mambo wanayoamini na wanayasimamia. Upinzani
wamempokea na kumpa bendera yao apeperushe. Wapiga kura wataona hawa
wanasiasa wote ni mashetani tu (kama kipimo cha wanasiasa ni ushetani),
na watachagua bora shetani waliyemzoea kuliko malaika wasiyemjua na
ambaye ameanza safari kuelekea kwenye dola kwa kusajili shetani mkubwa
kuliko wote na kumwita ‘malaika’. UKAWA wamemomonyoka kimaadili (moral
decay) zaidi ya CCM kwa kumpa bendera yao Ndg. Lowassa.
Kumi na Tatu, lugha ya CCM kwenye kampeni itakuwa rahisi sana kutokana
na kuwa na mgombea wa upinzani wanayemjua vizuri, na lugha ya
kuwasambaratisha wasemaji wote wa UKAWA itakuwa rahisi sana, maana CCM
itakuwa na kauli zao wakimchafua Ndg. Lowassa alipokuwa CCM na
watawakumbusha tu wananchi.
Kumi na Nne, uwezo wa kifedha wa Ndg. Lowassa utaathirika kwa sasa akiwa
mgombea wa UKAWA kwa maana atahofia kutumia pesa zake nyingi kwenye
kutafuta Urais kupitia upinzani hali ya kuwa anajua hana nafasi ya
kushinda, pia marafiki zake waliokuwa wakimchangia kipindi akiwania
Urais ndani ya CCM wamebaki CCM ama wanahofia kutengwa na CCM mara
atakaposhindwa na hawana imani kuwa atashinda Urais kutokea nje ya CCM,
na UKAWA hawana ruzuku ama vitega uchumi vya kulingana ama kuishinda
CCM, hivyo vifaa vya kampeni (branding materials) ya CCM na uwezo wa
kujitangaza utampoteza mgombea huyu mtata wa UKAWA mara moja kampeni
zitakapoanza.
Kumi na Tano, UKAWA hawana sera ambayo itamuunganisha mgombea wao na
kumuuza kwa wananchi sababu UKAWA siyo chama cha siasa, na hivyo mbali
na kumsafisha mgombea wao, hawatokuwa na jipya la kutoa kwa umma
ukilinganisha na CCM ambao watakuwa na ilani ya kueleweka na ambayo
wataiuza kwa wananchi bila shaka.
Je, wataweza kumsafisha Ndg. Lowassa ndani ya siku 64 za kampeni na
watanzania wakawaelewa? Ni maswali watakayopaswa kuyatafakari na
kuyajibu, pengine wakati wanayapatia majibu, muda wa kampeni utakuwa
umeishakwisha na watakuwa wameishashindwa uchaguzi.
Kwa vyovyote vile malengo ya Ndg. Lowassa, kudhoofisha CCM, hayatotimia
na huu utakuwa ni mwisho wake kisiasa, na hatoanguka peke yake,
ataanguka na vyama vyote vya upinzani vinavyounda UKAWA. Baada ya
kushindwa kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, siyo CCM itakayokuwa
inarudi kwenye meza kujipanga upya, bali ni vyama vitakavyosambaratika
kutoka UKAWA vitakavyorudi kujiuliza vilipoangukia na kuanza upya safari
ya kujijenga, na hii ni kama hata kutakuwa na mabaki ya vyama hivyo.
Mwandishi wa makala hii ni Mwanasiasa, Msomi aliyebobea kwenye afya ya
jamii, uchumi na uongozi, na ni Mbunge wa Jimbo la Nzega anayemaliza
muda wake. Anapatikana kwa email hkigwangalla@gmail.com , Twitter: HKigwangalla, Facebook: www.facebook.com/TeamHamisiKigwangalla
0 comments:
Post a Comment