WAKATI Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
Freeman Mbowe, akituhumiwa kuhongwa ili kumpitisha Edward Lowassa kuwa
mgombea urais wa chama hicho, imefahamika kwamba amefanya uhamisho wa
mabilioni ya fedha kwenye akaunti yake hivi karibuni.
Mbowe,
ambaye uamuzi wake wa kumpitisha Lowassa kuwania urais pasipo
kushindanishwa na mtu ndani ya chama chake na ndani ya muda mfupi
unadaiwa kukigawa chama hicho, amefanya uhamisho huo wa fedha kwa
kumtumia mtu anayeitwa Junaid Ali, ambaye ni Meneja wa Mahusiano ya
Wateja wa Benki ya Noor iliyopo Falme za Kiarabu.
Mwanasiasa huyo
ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai anayemaliza muda wake, ana
makampuni mengi hapa nchini lakini amefanya uhamisho huo wa fedha kwa
kutumia kampuni isiyofahamika sana ijulikanayo kwa jina la Aretra World
Wide Limited.
Kwa kumtumia Ali, Mbowe aliagiza fedha hizo zipelekwe katika akaunti tatu tofauti ambazo zote ziko nje ya Tanzania.
Kampuni hizo na kiasi cha fedha kilichopelekwa ni Puku Hong Kong
Limited iliyotumiwa dola 230,555 (shilingi milioni 461), TanChin Trading
Co. Limited iliyotumiwa dola 302,614 (shilingi milioni 605) na Hong
Kong Da Web International Tradings Limited iliyotumiwa dola 489,860
(shilingi milioni 980). Jumla ya fedha zote zilizohamishwa ni zaidi ya
shilingi bilioni mbili.
Makampuni yote yaliyotumiwa fedha yana ofisi zake nchini Hong Kong na yote yamefunguliwa akaunti katika benki maarufu ya HSBC.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kwamba Junaid Ali ambaye
amepewa maelekezo ya kufanya malipo hayo ni mtaalamu wa masuala ya
kufungua makampuni yanayojulikana kama offshore ambayo mara nyingi
hutumiwa na wafanyabiashara kufanya malipo pasipo kujulikana na watu.
Makampuni ya namna hii hufunguliwa katika nchi zenye usiri mkubwa kwa
watu wanaohifadhi fedha na ndiyo maana wakati wa sakata la ununuzi wa
rada, Andrew Chenge na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Dk. Idris
Rashid, walitumiana fedha kupitia akaunti zao zilizo katika nchi
zinazoongoza kwa kuwa na makampuni mengi ya namna hii.
Akimwandikia Junaid, Mbowe alisema; “ Tafadhali, nakuomba na kwa haraka,
ufanye uhamishaji wa fedha kutoka katika benki yako na kwenda kwenye
akaunti zifuatazo; Puku, TanChin na Hong Kong Da Web,” aliandika Mbowe.
Katika barua hiyo ambayo gazeti hili imefanikiwa kuona nakala yake,
Mbowe ameitambulisha kampuni yake kwa anuani ya S.LP 293816, iliyopo
katika jengo la World Trade Centre, Mtaa wa Sheikh Zayed, Dubai.
Uhamisho huo mkubwa wa fedha umefanyika katika kipindi ambacho wagombea
ubunge wa chama hicho wamelalamika kwamba wamekosa msaada wa chama chao
kifedha; huku kukiwa na tuhuma kwamba huenda viongozi wa juu wa Chadema;
hasa Mbowe, walihongwa fedha ili kumruhusu Mbowe awanie urais.
Tayari, mmoja wa washauri wa siasa wa Chadema kutoka Marekani, Joe
Costello, amewaandikia waraka viongozi wa juu wa Chadema, akisema kwamba
asilimia 30 ya wana Chadema wamechukizwa na uamuzi wa Lowassa
kuchaguliwa kuwa mgombea katika mazingira yanayozua maswali na
hawamtaki.
Kwa kuwa kampuni hiyo ya Mbowe ni offshore, gazeti
hili limeshindwa kufahamu ni kiasi gani cha fedha Mbowe amehifadhi au
ameweka kwenye akaunti hiyo na chanzo cha mapato hayo ni kipi kwa vile
biashara zake nyingi anafanya hapa nchini, ingawa ameanza kujitanua
kimataifa.
Hata hivyo, uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba
Mbowe alitakiwa kupokea kiasi cha dola 330,000 (shilingi milioni 660)
–takribani sawa na fedha aliyoihamishia TanChin Hong Hong, kutoka kwa
wafadhili wa chama hicho waliopo nchini Japan.
Kwa mujibu wa
mawasiliano baina ya viongozi wa juu wa Chadema na wafadhili hao wa
kijapani kupitia kwa mtu anayefahamika kwa jina la Naomi pamoja na
Mchungaji Mariko Morikubo, Chadema ilikuwa ichangiwe fedha za kijapani
(Yen), milioni 40 ambazo ni sawa na dola 330,000 kabla ya mwisho wa
Julai mwaka huu.
Mawasiliano ya awali baina ya wafadhili hao
ambao ni makanisa ya Kikristo yaliyoko nchini Japan, yalianzishwa na
aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbrod Slaa, ambaye aliomba
msaada wa magari pamoja na fedha kwa ajili ya kusaidia Chadema kwenye
uchaguzi huo.
Ndani ya Chadema, ni viongozi wakuu watatu ndiyo
wanaonekana kushiriki katika mazungumzo hayo; Mbowe, Slaa na Reginald
Munisi ambaye ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho.
Barua
pepe za awali kutoka kwa Slaa kwenda kwa akina Naomi wa Japan
zinaonekana kuanza kuandikwa mwanzoni mwa mwaka huu, lakini Mbowe
aliingilia kati ulipofika wakati wa kupokea malipo.
Akiandika
kupitia barua pepe ya Jumatatu, Aprili 20, 2015, Mariko aliwataka
viongozi wa Chadema kumpa taarifa muhimu kuhusu namna atakavyofanya
malipo, namba ya akaunti ya Chadema pamoja na mambo mengine.
“
Salamu kutoka Japan. Takaboshi (wafadhili hao wa Chadema) wanakutana
kesho jijini Tokyo, Japan. Wanajadiliana kuhusu suala la kuwatumia
fedha. Tafadhali naomba namba ya akaunti yenu ya benki ya chama ili
wafahamu namna ya kuwatumia,” ilisema barua pepe (email hiyo).
Barua pepe hiyo iliandikwa saa 3:32 asubuhi na ilipofika saa 9:29,
Munisi aliijibu lakini badala ya kuwapa akaunti ya Chadema kama
wafadhili hao walivyotaka, yeye aliwapa nambari ya akaunti binafsi ya
Mbowe.
“ Mpendwa Mariko, nakushukuru sana kwa ufuatiliaji wako.
Namba ya akaunti ni 02J1039056202. Jina la mwenye akaunti ni Freeman
Mbowe. Au mnaweza kufanya hivyo kwa kutumia akaunti dada ya benki ya
Citibank ya Marekani iliyopo jijini New York. Namba ya akaunti hiyo ya
fedha za kigeni (dola ya Marekani) ni 36072436,” ilisema sehemu ya barua
pepe hiyo ya Munisi ambaye wiki iliyopita alifanya mkutano na waandishi
wa habari kulalamika kuhusu masuala ya Daftari la Kudumu la Wapiga
Kura.
Baada ya kuona Wajapani wanachelewa kutuma fedha, Mbowe
alifunga safari yeye mwenyewe kwenda nchini humo kuonana na wafadhili
hao kama ambavyo barua pepe aliyowaandikia inavyosema.
“Nimewasili salama hapa Guangzhou, China. Nawashukuru kwa mawasiliano
yenu na Dk. Slaa na utayari wenu wa kuniona Tokyo. Sitakuja peke yangu
bali nitafuatana na mtu ambaye, kwa bahati mbaya, hatashiriki kwenye
mazungumzo yetu. Mungu awabariki sana,” aliandika Mbowe.
Gazeti hili linaendelea na uchunguzi wake kuhusu ni nani hasa alifuatana na Mbowe kwenye safari yake hiyo.
Juhudi za kumpata Mbowe kutoa maelezo kuhusu suala hili ziligonga
mwamba kwa vile simu yake ilikuwa ikiita bila majibu na wasaidizi wake
waliopokea walisema alikuwa kwenye mikutano ya kampeni za Lowassa.
Mwisho
|
0 comments:
Post a Comment