Posted by Williammalecela.com on Monday, October 26, 2015
 |
| Julius Mtatiro |
 |
HATUWEZI KUSHINDA UBUNGE SEGEREA...
Ndugu zangu, kwa moyo
mkunjufu kabisa napenda kuwajulisha kuwa hatuwezi tena kushinda ubunge
wa jimbo hili kwenye uchaguzi uliofanyika jana.
Matokeo ya
majumuisho ya kila kata yanaonesha kuwa mgombea wa Chadema, Bi.
Anatropia Theonest ana wastani wa kura 2000 - 2500 kwa kila kata.
Mimi nina wastani wa kura 4000 - 5000 kwa kata na mgombea wa CCM ana wastani wa kura 5000 hadi 6000 kwa kata.
Hii ina maana kuwa kura za UKAWA kama zingelipigwa kwa mgombea halisi
wa UKAWA tungeishinda CCM kwa zaidi ya kura 20,000 lakini kwa sababu
zimepigwa kwenda vyama viwili tunaweza kushindwa kwa wastani wa kura
5000 hadi 10,000.
Haya yaliyotokea hapa Segerea ni funzo kubwa
kwa vyama vyetu na wanasiasa wetu kuheshimu na kusimamia makubaliano,
kuwa na roho ya kufikiria mustakabali wa taasisi na watu wetu kuliko
MASLAHI BINAFSI. Kwa hatua ya sasa sitaeleza hujuma za ndani kwa ndani
tulizofanyiana ndani ya UKAWA hadi kufika hapa.
Nachoweza kusema
ni Asante Mungu na asante wana Segerea, asante watu wote waliojitoa kufa
na kupona kutusaidia, lakini pia asante kwa wale wote waliotusaliti
kimya kimya ili kuchochea mgawanyiko wa kura hizi.
Naahidi
kushiriki katika hatua zote za kumsaidia mshindi wa uchaguzi wetu ili
atangazwe rasmi kuwa mbunge wa wana Segerea. Mimi nitaendelea na
majukumu mengine lukuki ya kulijenga taifa letu.
Kwa sababu
yaliyosababisha kukosa ushindi wetu ni mambo ya ndani ya vyama vyetu,
sitachukua hatua zozote wala kukata rufaa kwa sababu wananchi
hawakutunyima ushindi, tumeugawanya wenyewe.
Nawapongeza madiwani
wa UKAWA walioshinda kwenye kata zote 13 za jimbo letu, tulishirikiana
na kupambana pamoja hadi kuleta ushindi huu, nawataka wachape kazi kufa
na kupona na waisimamie manispaa ya Ilala bila woga, nawaomba wakatumie
mipango na ushauri tuliowahi kupanga pamoja ili kuwatendea wana Segerea
yale waliyoyatarajia.
Mwisho, nataka kuwaeleza watanzania wote
kuwa sina kinyongo na mtu yeyote kwa matokeo haya. Mimi ni kati ya watu
wanaoamini kuwa SIASA SI AJIRA...Nitaendelea kuwatumikia watanzania kwa
njia zote muhimu nje ya vyombo vya maamuzi.
Nataka kuwaambia
wananchi wa Segerea kwamba niko imara sana, sijayumba wala kutetereka,
nawapenda sana nyote na poleni na MSHTUKO wa matokeo haya na muda si
mrefu tutayaweka hapa.
Ni mimi, Mtatiro Julius, Segerea.
|
0 comments:
Post a Comment