Kwa nini Lowassa anataka urais kwa nguvu, gharama yoyote? | The Times of Tanzania Makala
Kwa nini Lowassa anataka urais kwa nguvu, gharama yoyote? Na Omar
Mohamed ZIPO sababu nyingi zinazomsukuma Edward Lowassa autake urais…
Saturday 3rd October 2015
Kwa nini Lowassa anataka urais kwa nguvu, gharama yoyote?
Na Omar MohamedZIPO sababu nyingi zinazomsukuma Edward Lowassa autake urais wa Tanzania mwaka huu wa 2015 kwa nguvu na kwa gharama yoyote. Lakini kubwa mbili kati ya sababu nyingi hizo, ni hizi hapa: Tuhuma dhidi ya Richmond na makachero wa Scotland Yard wa Uingereza!
Tuanze na hili la pili ambalo ni geni kwa Watanzania walio wengi. Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Wilbrod Slaa, katika moja ya makombora aliyomrushia Lowassa, ambaye kwa sasa anagombea urais wa Tanzania kupitia chama hicho pamoja na Ukawa, ni tuhuma za kusakwa na makachero wa Uingereza kutoka kitengo maarufu cha Scotland Yard.
Katika mkutano huo na waandishi wa habari katika hoteli ya Serena, Dar es Salaam, Dk Slaa hakutaka kutoa maelezo kwa kina, zaidi ya kusema tu kwamba makachero hao wa Scotland Yard wa Uingereza wanamchunguza Lowassa, kwa tuhuma za kuhamisha kiasi cha fedha cha karibu pauni milioni 400 za Uingereza kutoka moja ya benki za Tanzania kwenda moja ya benki za nchi hiyo.
Hata hivyo, gazeti moja linalochapishwa kila wiki nchini, lilipata kuripoti taarifa hizo za uhamishaji huo wa fedha nyingi kiasi hicho Novemba 2010, uliodaiwa kufanywa na wana familia ya Lowassa.
Taarifa hizo ziliwaletea kasheshe kubwa sana wamiliki na waandishi wa gazeti hilo hata kabla taarifa zenyewe hazijachapishwa na kusambazwa kwa wasomaji nchini. Kwa kutumia nguvu yake ya fedha, Lowassa alidhamiria kwa nguvu zake zote na kwa gharama yoyote, kuhakikisha kwamba taarifa hizo hazichapishwi na kusambazwa nchini. Lakini kutokana na umahiri wa kimaadili wa wamiliki wake, taarifa zilichapwa na zikasambazwa!
Kwa vyovyote iwavyo, inawezekana kabisa taarifa hizo mpya zilizoibuliwa juzi na Dk Slaa kuhusu kashfa hiyo ya Lowassa kusakwa na makachero wa Scotland Yard kutokana na uhamishaji huo wa mabilioni hayo ya fedha, zinaweza zikawa na uhusiano na fedha hizo zilizoripotiwa na gazeti hilo. Wakati huo, taarifa hizo zilihusu kuchunguzwa kwa mmoja wa watoto wa kiume wa Lowassa, anayejulikana kwa jina la Fred kuhamisha sh bilioni moja kutoka moja ya benki za nchini kwenda Uingereza, kupitia kampuni ya uwakala ya nchi hiyo ya Mishcon, zikiwa na maelezo ya kutaka kununulia nyumba London, Uingereza.
Kwamba mazingira hayo ya fedha kiasi hicho kuhamishwa kutoka benki moja nchini na kuingizwa kwenye akaunti ya kampuni hiyo ya uwakala, ndiyo yaliyoishawishi taasisi ya SCD 6 Economics and Specialist Crime Proceeds of Curruption Unit ya Uingereza, kutilia shaka uhalali wa fedha hizo, hivyo kuamua kuanzisha uchunguzi wake.
Katika uchunguzi huo wa kutaka kutambua uhalali wa fedha hizo, taasisi hiyo iliwasiliana na Kitengo cha Ufuatiliaji wa Fedha Haramu cha nchini, ikitaka kupata maelezo ya awali kutoka kitengo hicho.
Ilielezwa na gazeti hilo, kwamba maelezo ya awali ambayo taasisi hiyo ya Uingereza iliyahitaji kutoka katika kitengo hicho cha Tanzania kinachohusika na fedha haramu, ilikuwa kufahamu kama Fred alikuwa kweli na ubia wa kibiashara katika kampuni za Alphatel Partinership (T) Ltd, Barare Ltd na Intergrated (T) Ltd, zote zikifahamika kumilikiwa na Lowassa.
Itakumbukwa pia, kwamba Dk Slaa katika mkutano wake huo wa hivi karibuni na waandishi wa habari, alimtuhumu Lowassa kumiliki kampuni nyingi nchini, ambazo yeye mwenyewe haonekani humo, kwa maana ya majina yake.
Lakini taasisi hiyo ya Uingereza, ilijiridhisha kwamba kampuni tatu hizo hapo juu, zote zinahusishwa na Lowassa, lakini zikitambulishwa kwa majina ya wakurugenzi ambao ni familia ya mwanasiasa huyo, huku Fred akiwa ndiye msimamizi mkuu.
Mpaka sasa, haifahamiki kama Kitengo hicho cha Tanzania chenye jukumu la Kufuatilia Fedha Haramu kilitoa ushirikiano kwa kiwango gani kwa Taasisi hiyo ya Uingereza, hasa ikikumbukwa ushirikiano uliowahi kutolewa na Takukuru kwa Kamati Teule ya Dk Mwakyembe wakati wa sakata la kashfa ya Richmond mwaka 2007/2008.
Hakuna Mtanzania atakayeshangaa kusikia kwamba tangu mwaka huo wa 2010 hadi sasa, kitengo hicho cha Tanzania hakijatoa maelezo ya kina na ya kuridhisha kwa taasisi hiyo ya Uingereza, kama ambavyo vitengo vyetu muhimu vilishindwa kutoa ushirikiano hata kwenye kashfa ya Richmond na ile ya Rada, iliyosababisha taasisi za Uingereza kujitolea kusaidia masikini wa Taifa hili kurejeshewa kile kilichokuja kubatizwa jina la ‘chenji ya rada.’
Kwa upande wa Richmond, umma wa Watanzania umesikia kutoka kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, Dk Harrison Mwakyembe, Dk Slaa na wanataaluma wengine wa sheria wakiweka wazi, kwamba kisheria, makosa yoyote ya jinai, hayana muda wa ukomo wa kufikishwa kwenye mikondo ya sheria.
Kwa hiyo, mpaka hapa, Lowassa anafahamu vema kwamba nyuma yake, kuna kesi mbili kubwa za kujibu, kama itatokea akaingia Ikulu, Mtanzania mwenye dhamira ya kweli ya kupambana na vitendo vya ufisadi nchini. Ana kesi ya Richmond, ana kesi ya kujibu ya kuhamisha pauni milioni 400, sawa na karibu sh bilioni 1,200!
Katika hali ya kawaida, na kwa sababu wahenga wanasema lisemwalo lipo, kama halipo leo litakuja kesho, hakuna namna yoyote ya Lowassa kukwepa kesi hizo, zaidi ya yeye kuhakikisha kwa nguvu zote na kwa gharama yoyote iwayo, anakuwa rais wa nchi hii.
Na kwa vyovyote vile iwavyo, dalili hazimpi matumaini ya kubaki salama endapo mgombea urais huyu wa sasa wa CCM, Dk John Magufuli atafanikiwa kuingia Ikulu, kwa sababu katika kampeni zake zote amewahakikishia wananchi umuhimu wa Serikali yake kuunda mahakama maalumu itakayoshughulika na kesi za wezi wa mali za umma, wahujumu uchumi na mafisadi! Mpaka tarehe hii, si haba. Lowassa ameweza kuonesha Watanzania nguvu zake za kiakili, kimwili na kiroho anazotumia kuusaka urais wa Tanzania mwaka huu, ameweza kuwaonesha nguvu ya fedha aliyokuwa amejiandaa nayo kwa ajili ya kuusaka urais ili kukwepa dhahama hiyo inayomsubiri.
Kwa nini akiwa Rais wa Tanzania, anaweza kuruka kihunzi cha kesi zote hizo? Kwa Katiba ya Tanzania hii ya mwaka 1977, ipo kazi kweli kumfikisha rais wa nchi hii kizimbani kwa tuhuma za aina yoyote. Kwa Katiba yetu hii, kazi hiyo ngumu haipo kwa rais aliyeko madarakani pekee, bali hata kwa rais mstaafu!
Kwa hiyo, pona ya Lowassa kuepuka mkono wa sheria, sasa na maisha yake mingine yote aliyobaki nayo duniani, ni kuukwaa urais basi! Kama Mwenyezi Mungu atamjalia kukaa madarakani miaka 10 ya urais, basi yeye na familia yake, akina Fred watakuwa salama, hawataguswa na chombo chochote kile cha ndani au cha nje.
Kwa kuwakumbusha tu wasomaji wangu, njia hiyo ya kujiokoa anayoitafuta Lowassa kwa nguvu zake zote, ndiyo aliyoitumia Rais wa sasa wa Kenya, Uhuru Kenyatta. Itakumbukwa kwamba jumla ya Wakenya sita, wakiwamo wanasiasa watatu, watendaji wa Serikali wawili na mwandishi wa habari, walifikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), iliyoko mjini The Hague, Uholanzi, wakikabiliwa na tuhuma za kuchochea mauaji na vurugu katika nchi hiyo jirani mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007.
Mwaka 2012, Wakenya wanne kati ya hao sita, walikutwa na kesi ya kujibu katika mahakama hiyo. Hao ni Uhuru, William Ruto, Francis Muthaura na Joshua arap Sang. Wawili waliachwa huru na mahakama hiyo, baada ya kutoguswa na tuhuma zilizokuwa zikiwakabili. Hao ni Henry Kosgey aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Kenya na Hussein Ali, aliyekuwa waziri katika Serikali ya Rais Mwai Kibaki.
Mwaka 2014, wananchi wa Kenya walifanya Uchaguzi Mkuu kama ambavyo Watanzania wanafanya uchaguzi huo mwaka huu. Watuhumiwa wakuu wa mauaji na vurugu za Kenya mwaka 2007/8 katika Mahakama ya ICC, Kenyatta na Ruto, walitumia uchaguzi mkuu huo wa ndani ya nchi yao, wakacheza karata zao vizuri!
Uhuru aligombea urais, huku Ruto akiwa mgombea mwenza. Baada ya matokeo kutangazwa wawili hao wakaibuka kidedea, wakaapishwa na kuingia Ikulu ya Kenya. Kesi ya The Hague dhidi ya Uhuru imetupwa!
Uhuru alifanikiwa mwaka jana kuruka kihunzi cha kesi iliyokuwa ikimkabili The Hague, je Lowassa naye atafanikiwa kukwepa mikono ya sheria juu ya tuhuma kuu mbili zinazomzunguka, za Richmond na uhamishaji wa fedha nyingi katika mazingira ambayo kisheria hayakubaliki? Tusubiri.
0 comments:
Post a Comment