HII NDIYO ORODHA YA WALIOMNYIMA LOWASSA URAIS
NA LUQMAN MALOTO
MWANASAIKOLOJIA Tim Urban katika andiko lake Nini Kinakufanya Uwe Wewe (What Makes You You), anafafanua dhana mbalimbali kuwa ukishashakuwa wewe hata ubadilishwe utabaki wewe tu!
Ipo dhana ya mwili (The Body Theory), kwamba hata ukatwe kidole au ubadilishe figo na ini, utabaki wewe tu. Dhana ya ubongo (The Brain Theory), kuwa hata ukichezewa utabaki wewe tu.
Kuna kitu ni lazima kiwe kwenye mstari wake, ukishapewa uhusika na ukivuma, ni vigumu kubadilika kwa ngonjera. Hoja nzito huwa hazilainishwi kwa maneno mepesi.
Aliyekuwa Mgombea Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Ngoyai Lowassa, ameshindwa na Dk John Pombe Magufuli ambaye sasa ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wiki iliyopita, niliandika makala yenye kichwa “Shombo za Kubenea zimeharibu ndoto ya Lowassa”. Niliahidi pia nitaandika makala kuchambua orodha ya watu ambao kwa namna moja au nyingine wamesababisha ndoto ya Lowassa iwe ngumu kutimia.
Uungwana ni kutimiza ahadi na katika makala haya nachambua uhusika wa mmoja baada ya mwingine. Hapa simtaji Kubenea kwa sababu nilishamalizana naye katika makala yaliyopita.
Msingi mkuu ni jinsi ambavyo Lowassa alivyopewa uhusika mbaya kwenye jamii ya Watanzania. Na kama alivyosema Tim Urban, Lowassa baada ya kupewa uhusika huo, amekuwa hivyo!
TUNDU LISSU
Mwaka mzima unautangazia umma kuwa Kaundime ni mwanamke kahaba, hafai na ameshindikana kwa kubadili wanaume. Kila ukimuona barabarani anapita, unapaza sauti: “Mtazameni yule mwanamke, ni wa kuogopwa, ni kahaba kuliko machanguduo wanaojiuza barabarani.”
Kutokana na kelele zako, wazazi na familia yako yote imeweza kupokea na kuamini kuwa Kaundime ni mwanamke aliyeshindikana. Jamii nzima inamtazama Kaundime kwa jicho la mshangao, kwa kumuona ni mwanamke aliyekosa aibu.
Wanawake wenzake wakimuona wanabetua midomo juu, wanamuonea kinyaa. Mwenyewe ameshajisikia vibaya mpaka amezoea. Ikafikia kipindi mpaka akikatiza barabarani, akisikia tu neno ‘malaya’, anageuka, anajua atakuwa anasemwa yeye. Anaishi kwa kujishtukia Kaundime wa watu!
Baada ya kupita miezi 12, unamchukua Kaundime mpaka nyumbani kwenu, unakwenda kumtambulisha kwa wazazi wako, unawaambia ndiye unampenda na unataka kumuoa. Wazazi wako wanakuuliza: “Kaundime huyuhuyu?”
Unawajibu kwa kujiamini kabisa: “Ndiyo, Kaundime huyu, mwanamke bora kabisa kuwahi kumuona.”
Kwa kuhisi labda akili zako zitakuwa zimegawanyika kushoto na kulia, wazazi wako wanakuchukua pembeni, wanakuuliza: “Upo sawa kweli?” Nawe unawajibu: “Taslimu kabisa!”
Baadaye wanakuuliza: “Mbona ni wewe mwenyewe ulikuwa unaimba hapa mji mzima kuwa Kaundime ni mwanamke kahaba na hajatulia, unataka huyo ndiye awe mkwe wetu? Awe mama wa wajukuu zetu? Hapana kabisa!”
Wewe unawaambia wazazi wako: “Kaundime hajawahi kuwa kahaba, watu wanamsingizia, na walianza kumsingizia ili achafuke kusudi nisimuoe.”
Hapo wazazi wako kama vile hawaamini: “Hivi kweli upo sawa? Nani alikuwa anamsingizia? Mbona ni wewe mwenyewe uliyekuwa unatangaza kuwa Kaundime ni kahaba?”
Familia nzima inaungana kumkataa Kaundime, wewe unashikilia msimamo kuwa watu wana chuki zao binafsi lakini ukweli ni kuwa Kaundime ndiye mwanamke bora sana kuoa.
Septemba 15, 2007, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibroad Slaa alitaja majina 11 katika orodha ya aibu (list of shame) ambayo ni maarufu zaidi kama orodha ya mafisadi.
Ndani ya orodha hiyo yupo Lowassa. Kwa taarifa tu ni kuwa Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu ndiye aliyeandika waraka wa list of shame kisha kusomwa na Slaa.
Lissu ni Mbunge wa Singida Mashariki, na baada ya kusomwa kwa orodha hiyo, alifanya mahojiano mbalimbali pamoja na mikutano ya hadhara akielezea ufisadi wa Lowassa.
Lissu alilikoroga zaidi mwaka huu, pale alipohojiwa kuhusu chama chake kumteua Lowassa kuwa mgombea urais, akasema walifanya hivyo kutokana na uhusika wake katika kashfa ya Richmond.
Ukweli ni kuwa list of shame ilisomwa kutokana na ufisadi uliofanyika Benki Kuu katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA). Hapa Lissu alijichanganya, na hiyo ilisababisha CCM kutumia sauti yake kutengeneza tangazo la kumponda Lowassa na lilirushwa mno na Star TV.
DK WILLIBROAD SLAA
Huyu ndiye mwiba hasa wa Lowassa. Ndiye aliyesoma list of shame, Viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke, Dar es Salaam na aliendelea kuchambua ufisadi wa Lowassa katika mikutano mbalimbali.
Maneno ya Slaa yalituama kwenye vichwa vya watu. Alibainisha kuhusu Lowassa kupora mradi wa maji Arumeru na kupeleka Monduli. Akaeleza kwamba Monduli Lowassa amejenga ofisi ya kifisadi kama mbunge.
Alimtaja Lowassa kuhusu EPA na alimng’ang’ania katika Richmond. Hivyo, huwezi kutaja eneo ambalo Lowassa alianza kuharibikiwa na safari yake ya Ikulu pasipo kumtaja Slaa.
Baada ya Lowassa kujiunga na Chadema, Slaa alijiengua na chama hicho, kisha baadaye aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza sababu mbalimbali za kujitoa.
Kikubwa ambacho Slaa alikisema ni kuwa Lowassa alijiunga Chadema kama mzigo, vilevile alijiunga na chama hicho bila kujisafisha na skendo zake ambazo amekuwa akituhumiwa nazo kwa miaka nenda rudi.
Slaa ni mwanasiasa mkubwa nchini. Kabla ya Lowassa kujiunga na Chadema, Slaa ndiye alikuwa moyo wa chama hicho. Wapo watu wengi walikishabikia kwa sababu yake.
Wenye kasoro za kujitambua hudiriki kusema Slaa hakuwa na athari yoyote alipojiengua Chadema. Huo ni utani! Msimamo wa Slaa ulikuwa msumari wa moto kwa safari ya Lowassa kwenda Ikulu.
Ni imani yangu kuwa hata CCM wenyewe walianza kujihakikishia ushindi baada ya Slaa kutoka kwenye vyombo vya habari na kuweka wazi msimamo wake kuwa hakubaliani na uamuzi wa Chadema kumpokea Lowassa na kwamba ni mtu fisadi asiyesafishika.
Kumbuka kuwa Slaa alikuwa mgombea urais wa Chadema mwaka 2010 na alitoka wa pili. Na katika kinyang’anyiro hicho, alipata asilimia 26 ya kura zote. Huyu ni mtu mwenye watu wengi ambao kwa miaka nenda rudi wamejenga imani kubwa kwake.
DK HARRISON MWAKYEMBE
Aliongoza Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza mkataba wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond na serikali. Alipokamilisha na timu yake, alisoma bungeni na ndiyo ikawa sababu ya Lowassa kujizulu uwaziri mkuu mwaka 2008.
Ripoti ya Richmond ndiyo maarufu zaidi katika historia ya Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lililoongozwa na Spika Samuel Sitta. Na ripoti hiyo ndiyo nyundo nzito kwa Lowassa.
Wanasiasa wanapotaka kufanya marejeo ya ufisadi wa Lowassa, haraka sana huzungumzia Ripoti ya Richmond. Hivyo, huwezi kueleza kushindwa kwa Lowassa pasipo kumtaja Mwakyembe kama sehemu ya vyanzo vilivyokatisha ndoto za Mzee wa Matumaini.
Hata Dk Kikwete kwa kutambua umuhimu wa Mwakyembe, alimteua kuwa mmoja wa wajumbe wa timu ya kampeni za urais kumnadi na kumtetea Dk Magufuli. Hii ni kwa sababu anajua kuwa alikuwa na nondo nyingi.
Na Mwakyembe hakufanya ajizi, alitumia fursa hiyo vizuri, alifanya mikutano na mahojiano akielezea hata yale ambayo hayakusemwa kwenye Ripoti ya Richmond, akibainisha uhusika wa Lowassa katika kashfa ya Richmond.
ASKOFU JOSEPHAT GWAJIMA
Halikuwa jambo baya kwa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kusimama binafsi na kumtetea Lowassa kuwa ndiye anayefaa kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Shida ilijionesha pale Gwajima alipoonekana mstari wa mbele, huku akijitambulisha kuwa rafiki wa Lowassa, wakati huohuo, video za askofu huyo zikivuja kumuonesha jinsi mchungaji huyo akishambulia dini ya Kiislam.
Kitendo cha Lowassa kumuweka karibu Gwajima ambaye sauti na video zake zilisambazwa, akikashifu Uislam ilikuwa sawa na kukataa kura za Waislam. Maana CCM walizitumia kufikisha ujumbe kwa Waislam.
Upande mwingine, Gwajima aliwahi kumtusi Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kadinali Polycarp Pengo, hivyo kuweka utengano na Wakatoliki.
Kingine ni jinsi Gwajima alivyotokeza kumjibu Slaa ambaye alimtaja askofu huyo kuwa mshenga wa ndoa ya Lowassa na Ukawa.
Askofu Gwajima alifanya mashambulizi katika maisha binafsi ya Slaa. Waungwana wakajiuliza: "Huyu ni rafiki wa Lowassa, wakishinda na kushika dola itakuwaje?"
PETER MSIGWA
Wanasema ni vizuri kuweka akiba ya maneno. Msigwa aliwahi kukaririwa akisema kuwa yeyote atakayemuunga mkono Lowassa inabidi apimwe akili.
Kauli ya Msigwa ilimpa wakati mgumu alipokuwa anagombea jimboni kwake Iringa Mjini. Upande wa pili, kauli hiyo ya Msigwa ilitumika mno na viongozi wa CCM kama marejeo ya jinsi ambavyo Lowassa asivyofaa.
DK JOHN MAGUFULI
Kipindi CCM wakipelekwa puta na Lowassa, viongozi wa chama waliumiza kichwa aina ya mtu ambaye hana makando-kando mengi na anauzika.
Wengi ndani ya chama hawakuwa wakiuzika, Magufuli akachukuliwa kama risasi kali kwa sababu anakubalika kwa wananchi, vilevile hana kashfa nyingi kama Lowassa.
Naamini kuwa kama Magufuli asingekuwepo, CCM wangemsimamisha Lowassa kuwa mgombea urais. Wangekosa namna.
Na kama CCM ingemkata kwa jeuri tu, basi Lowassa angeweza kushinda urais kupitia Ukawa kwa sababu CCM ingesimamisha mgombea dhaifu.
Shida ni kuwa Lowassa alishindana na Magufuli ambaye aliuzika kirahisi kwa wapigakura, ingawa siyo uongo kwamba msuli wa Lowassa ulikuwa tishio.
PROFESA IBRAHIM LIPUMBA
Utafanya makosa ya aina ya pekee kama utasema kujitenga kwa Profesa Lipumba ndani ya umoja wa Ukawa, hakukuwa na athari yoyote katika safari ya Lowassa.
Lipumba ni mwanasiasa mkubwa na moja ya nembo za upinzani nchini. Ni kweli kuwa alipotangaza anajitenga na kujivua uenyekiti wa Cuf, kuna waliomzodoa kwamba hana athari yoyote.
Kama Lipumba angesimama na kumfanyia kampeni Lowassa, angeweza kuongeza kura nyingi ambazo ama alizikosa au hata kwenda kwa Magufuli.
FREEMAN MBOWE
Kauli za Mbowe ziligeuka mtaji wa CCM katika kumshambulia Lowassa. Kwanza alishamtaja Lowassa kama fisadi, baadaye akasema ni dhaifu, kisha akashangaa wezi wa kuku wanauawa huku Lowassa akiachwa akitembea barabarani.
Maneno yanaumba , kwa hiyo matamshi ya Mbowe yalishamchafua Lowassa na kumuacha nyang’anyang’a. Watanzania wengi walimuona Mbowe kama mtu asiye na aibu alipokuwa anageuza maneno, mara leo Lowassa fisadi, kesho ndiye anafaa kuwa Rais wa Tanzania.
KINGUNGE NGOMBALE MWIRU
Kwa ukubwa wa umri wake na uzoefu wa kisiasa alionao, ilidhaniwa angekuwa mshauri mzuri kwa Lowassa na pengine safari ya Matumaini ingetimia ndani ya CCM.
Kingunge akiona kabisa Lowassa anakosa nidhamu kwa chama, akifanya matumizi ya kufuru na kuonesha vitendo kama chama amekiweka mfukoni, mzee huyo hakumkosoa.
Badala yake Kingunge naye akageuka mpambe, akimtetea Lowassa kwa jambo. Naye akasema hakuna mwenye ubavu wa kumkata Lowassa CCM.
Huyu mzee hakutumia uzee wake vizuri, kumwelekeza Lowassa njia sahihi za kupita ili kukwepa mkasi wa CCM.
Kingunge alipomfuata Lowassa Ukawa, watu wakasema "Na Kingunge naye!"
Neno mabadiliko lililonadiwa na Kingunge, lilikosa afya. Maana Kingunge mitaani ni alama ya wafaidi nchi kwa kiwango cha juu.
Na kwa sababu Lowassa alikuwa anazungumzwa kama mtu mwenye malengo machafu katika kuchukua nchi, Kingunge aliyafanya maneno hayo kuwa na nguvu zaidi.
Ilionekana kuna kitu kinatafutwa, maana Kingunge siyo wa kudai mabadiliko mwaka 2015, wakati yupo daraja bora (elite class ) katika wafaidi keki ya taifa tangu uhuru wa Tanganyika na kabla Tanzania haijazaliwa.
GODBLESS LEMA
Kwa kutazama mbegu iliyopandwa kwa muda mrefu, Lema yumo kwenye orodha ya waliosababisha Lowassa ashindwe kupata urais. Alifanya mikutano mingi kumshambulia kama mtu asiyefaa kwenye jamii.
Moja ya nukuu maarufu ambayo Lema aliwahi kuitoa kumshambulia Lowassa ni ile aliyosema: “Ni jambo la heshima kubwa kwa Mungu kumzomea Lowassa kwa sababu ni fisadi.”
DK KIKWETE
Kifo cha Lowassa kisiasa kilianzia pale Dk Kikwete akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipoikubali barua ya Lowassa ya kuomba kujiuzulu uwaziri mkuu, maana ilithibitisha kwamba alikuwa na doa serikalini.
Dk Kikwete katika kampeni za Magufuli, alitokeza waziwazi na kueleza jinsi ambavyo Lowassa alivyocheza ‘faulo’ katika mkataba wa Richmond.
Aliwahi kusema: “Mwenye Richmond ni yule anayetembea na Tundu Lissu kwenye mikutano, amtaje mwenyewe, asipomtaja, nitamtaja mwenyewe.”
Na kweli, katika mkutano wa kufunga kampeni za CCM, Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Dk Kikwete alimtaja Lowassa moja kwa moja kuwa ndiye janga kuu la Richmond.
Dk Kikwete akiwa mwenyekiti wa chama ndiye aliyesimamia mkasi wa kumkata Lowassa. Kama angetaka Lowassa awe, hakika angekuwa.
FREDRICK SUMAYE
Alipofanya uamuzi wa kuhamia Ukawa, wafuatiliaji na wachambuzi wengi wa kisiasa walibaki midomo wazi. Sumaye!
Sumaye na Lowassa walikuwa maadui chini ya nyumba moja. Vita yao ya kugombea ufahari ndani ya CCM haikuwahi kujificha.
Kuelekea uteuzi wa Mgombea Urais CCM, Sumaye alitishia kuhama chama kama kingempitisha Lowassa kuwa mgombea. Akatumia neno 'mla rushwa' kama sifa ya Lowassa.
Ajabu ni kuwa CCM walivyomkata Lowassa, Sumaye badala ya kufurahia mapenzi yake yametimizwa, akanuna. Lowassa alipohamia Ukawa naye akamfuata.
Hii ndiyo sababu uamuzi wa Sumaye kuhama CCM na kujiunga Ukawa, mpaka leo hakuna mtu ambaye ameuelewa. Naamini hata yeye mwenyewe Sumaye hajauelewa uamuzi wake.
Sumaye akawa kampeni meneja wa Lowassa. Yaani baada ya kumchafua kote na kumsiliba masizi na matope, kisha akamuombea kura, nani angeelewa?
LOWASSA MWENYEWE
Kauli za Lowassa pamoja na mashambulizi kuhusu afya yake kwa namna moja au nyingine, vimesababisha kupunguza kura.
Kauli zake akisifu kazi nzuri iliyofanywa na Rais wa Nne, Dk Kikwete na kusema ataendeleza pale atakapoishia. Baadaye, tena ndani ya mwezi mmoja kuibuka na kusema Dk Kikwete ameharibu uchumi wa nchi. Ukigeugeu huo umesababisha aonekane haeleweki.
Lowassa aliwahi kuwaambia Walutheri waombe sana ili mwaka 2015 iwe zamu ya Rais Mlutheri. Kauli hiyo ilipokelewa kwa hisia tofauti, huku akitajwa kama kielelezo cha mgombea mdini nchini.
Kuhusu afya, ilikuwa ni hoja iliyommaliza Lowassa kwa kiasi kikubwa mno. Wapo watu walikuwa na matumaini makubwa lakini walibadili gia angani kwa hofu kuwa kiongozi huyo hatabiriki.
Kingine ni kiburi na utovu wa nidhamu wake, Lowassa alipokuwa anatafuta uteuzi ndani ya CCM, alifanya makosa mengi.
Alizionesha mamlaka za chama kuwa hazina ubavu mbele yake. Akafanya anavyotaka kama vile yeye ndiye mmiliki wake. Akasema hakuna mwenye uwezo wa kumkata, hakuna wa kuzuia mafuriko yake kwa mikono.
Tabia hiyo ya Lowassa ilimuondolea baraka za viongozi wa chama. Waliona wangempitisha, ingesemwa wamemuogopa. Wakaona potelea mbali ikisemwa wamemuonea.
Hakuna mahali ambako Lowassa alikosea, kama kuhisi kuwa Dk Kikwete hakuwa na ubavu. Yaani mwenyekiti wa chama, halafu Amiri Jeshi Mkuu wa nchi, unasema hana ubavu.
Kwa JK, ni hakika kuwa Lowassa alijaribu tindikali kwenye chupa, akidhani haina makali yoyote, akajimwagia kichwani. Ameona madhara yake. Imemchoma mwili mzima.
Kwa kifupi watu ni wengi waliomnyima urais Lowassa na hoja zilizomkandamiza ni nyingi, ila kwa uchache tuishie hapo.
By Luqman Maloto
MAANDISHI GENIUS
+255 713 355 717

0 comments:
Post a Comment