KWENU
warembo wa Bongo Movies, Wema Sepetu ‘Madam’ na Kajala Masanja. Habari
zenu binafsi? Bila shaka ni wazima wa afya na mnaendelea na majukumu
yenu ya kila siku. Kitambo kidogo sijawaona lakini naamini pumzi ya bure
mnaendelea kuivuta ndiyo maana nasikia matukio yenu kwenye vyombo vya
habari.
Mkitaka
kujua afya yangu, mimi ni mzima. Namshukuru Mungu naendelea na shughuli
zangu kama kawaida. Mungu ni mwema sana, anaendelea kubariki kazi ya
mikono yangu, namuomba yeye aendelee kunibariki zaidi na zaidi.
Dhumuni
la kuwaandikia barua hii ni kutaka kuwakumbusha kwamba nyinyi kwa sasa
ni watu wazima. Umri wenu unatosha kabisa kusema haufanani na yale
matukio yasiyokuwa na kichwa wala miguu. Mara kadhaa nimewahi kuwaambia,
hata yale mashindano yenu ya kumwaga fedha ukumbini, nyakati hizi si
zake.
Mambo
ya kuibiana mabwana kama yalishatokea, itoshe sasa kusema ulikuwa ni
ujana. Kwa kuwa ilitokea, hakuna namna zaidi ya kuyasahau na
kuchapakazi. Soko lenu la filamu bado haliridhishi, lakini mnapaswa
kukomaa ili angalau mtengeneze fedha kupitia kazi zenu na si kuhongwa.
Binafsi
sikufurahishwa na tukio lenu la kukutana ukumbini na kuzinguana mbele
ya kadamnasi lililoripotiwa wiki iliyopita na magazeti Pendwa. Lilikuwa
tukio linaloonesha kwamba bado hamjakua kitu ambacho sitaki kukiamini.
Kama
nilivyotangulia kusema hapo awali, huu siyo wakati wa nyinyi kuoneshana
ubabe wa fedha. Kwamba eti kwa kuwa mwenzako kaenda kutunza msanii
jukwaani, na wewe lazima utunze nyingi zaidi ili uonekane wewe ni zaidi.
Ndugu
zangu, bahati nzuri maisha yetu tunajuana. Kwa kiasi kikubwa natambua
maisha ya wasanii wetu nchini hususan warembo. Wengi wenu hamtegemei
sanaa kuendesha maisha yenu. Wengi mnategemea mapedeshee au ‘mabwana’
kutamba mjini.
Niwashauri
hizo fedha mnazozipata ni bora mngewekeza kwenye sanaa yenu.
Mkajizatiti vizuri ili ziweze kuzaliana. Mnapigana ili iweje?
Mnatambiana mbele za watu inawasaidia nini. Wenzenu wanapigana siku hizi
wanaingiza fedha.
Nyinyi
kazi yenu si ubondia. Kazi yenu ni uigizaji. Igizeni kwelikweli na
Watanzania wawaunge mkono kwa kununua kazi zenu. Sanaa yenu ina
changamoto nyingi, mnawezaje kuzishughulikia ikiwa hamna umoja.
Mtawezaje
kutatua changamoto hizo ikiwa hamna upendo kati yenu? Si rahisi kutatua
changamoto hizo wakati mna chuki. Ili mfanikiwe, mnahitaji
kushirikiana. Shirikianeni ili muweze kuisogeza sanaa mbele, acheni vita
ya kipuuzi mnayoendelea kuifanya.
Mkizingatia
hayo niliyowaambia, hakika tutaona mabadiliko kwenu na sanaa kwa
ujumla. Nina imani nyinyi ni watu wazima na mtajipanga upya na mtaanza
kuchapa kazi kama kauli mbiu ya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dk. John Pombe Joseph Magufuli, ‘Hapa Kazi Tu’.
Ni mimi mtu wenu,
Erick Evarist.
Rushwa, uonevu, njoo kesho na mambo mengine mengi ndio yana tufanya tusi rudi nyumbani.
ReplyDelete